Sura Ya 01 : Lugha na Utamaduni
| Utangulizi Mawasiliano hufanyika miongoni mwa wanajamii kupitia lugha. Aidha, watu wenye utamaduni mmoja hutambulika kupitia lugha wanayoitumia. Katika sura hii, utajifunza namna Kiswahili kinavyofungamana na jamii na utamaduni. vilevile, utajifunza namna Kiswahili kinavyoweza kutumika kama kielelezo cha utamaduni wa Mtanzania pamoja na umuhimu wa kujifunza Kiswahili. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuwasiliana kwa kutumia Kiswahili fasaha katika miktadha mbalimbali kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania. Pia, utaweza kujenga Labia ya udadisi na ubunifu katika masuala mbalimbali ya lugha ya Kiswahili na matumizi yake. |
| Fikiri Lugha na utamaduni vinavyohusiana |
Matumizi ya lugha ya Kiswahili kama utambulisho wa Mtanzania
Soma habari kuhusu Kijiji cha Safina, kisha jibu maswali yanayofuata.
Kijiji cha Safina kilikuwa na wakazi wenye makabila anuai. Wakazi wa kijiji hicho hawakuweza kuwasiliana kwa sababu walitumia lugha tofauti. Mwaka fulani kulitokea ukame katika kijiji hicho, hali iliyodumu kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, iliwalazimu wanakijiji hao kuhamia karibu na chanzo cha maji ili waweze kupata huduma ya maji. Wanakijiji hao walikaa kwa pamoja kwa kipindi chote cha ukame, hali iliyofanya kuwa na msamiati unaofanana kutokana na baadhi ya maneno kutumika mara kwa mara miongoni mwao.
Baada ya muda kupita, wanakijiji hao walijikuta wana mfumo mmoja wa mawasiliano ambao ulieleweka miongoni mwa wanakijiji wote. Kuanzia hapo, watu wa Kijiji cha Safina wakakubaliana kutumia mfumo huo wa mawasiliano. Muda ulivyozidi kwenda, walijikuta wanaujua na kuutumia mfumo huo bila mafunzo rasmi. Mfumo huo ulioibuka kinasibu ulikuuwa na mpangilio maalumu wa sauti, silabi, maneno na sentensi ambao unaleta maana. Waliendelea kuongeza maneno katika lugha hiyo kadiri walivyokutana na dhana mpya katika mazingira yao kwa kufuata mfumo wa lugha hiyo. Majina yao na ya maeneo yao yaliendana na maana na dhana kama zilivyokubaliwa katika jamii yao. Hivyo, maana za maneno yao zilitambulisha jamii yao kupitia mfumo wao wa mawasiliano. Aidha, mfumo huo uliwafanya wanakijiji hao waanze kuelewana katika mazungumzo yao na kufanya shughuli mbalimbali kwa pamoja. Walianza kuwasiliana kwa kutumia mfumo wao kwa kuzungumza kisha wakajifunza kuandika. Wakazi wa kini hicho waliunganishwa pamoja kupitia mfumo huo wa mawasiliano kwani ulitumiwa na watu wote. Hivyo, jamii ya Safina haikuwa na namna nyingine ya kueleza masuala yake pasipo kutumia mfumo huo wa mawasiliano. Kwa hakika, wakazi wa Kijiji cha Safina walijenga uhusiano mzuri miongoni mwao kama wanajamii moja.
Sanjari na hayo, mfumo wa mawasiliano wa Kijiji cha Safina uliwawezesha wanakijiji hao kufikiri, kuhifadhi na kurithisha maarifa na amali zao kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Vilevile, kupitia mfumo huo wa mawasiliano, watu wa kijiji cha Safina waliweza kutambulika kila walipokwenda kwani walijitofautisha na wazungumzaji wa mahali pengine kutokana na uzungumzaji wao. Pia, waliweza kuendeleza utamaduni wao na kuongeza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mfumo wa mawasiliano walioutumia. Hivyo, Kijiji cha Safina kilifanikiwa kukua na kuwa na maendeleo makubwa sana.
| Maswali 1. Unafikiri mfumo uliotumiwa na wanakijiji wa Safina katika kuwasiliana unaitwaje? 2. Umejifunza nini kuhusu dhana ya lugha kutokana na habari uliyoisoma? 3. Vipengele gani vya lugha hujenga mpangilio wa mfumo wa mawasiliano kwa mujibu wa habari uliyoisoma? 4. Kuna uhusiano gani kati ya lugha na jamii kulingana na habari uliyoisoma? 5. Kutokana na habari uliyoisoma, lugha ina dhima zipi? |
Zingatia
Lugha ni mfumo au mpangilio maalumu wa sauti za nasibu wenye kuleta maana, uliokubalika kutumika katika kuwasiliana miongoni mwa wanajamii wenye utamaduni mmoja. Mfumo huo unahusisha kipengele cha sauti, silabi, maneno, sentensi na maana. Sauti katika maneno na maneno katika sentensi hupangwa kwa utaratibu maalumu kulingana na lugha inayohusika ili kuleta maana. Hivyo, mpangilio huo hutofautisha lugha moja na nyingine. Lugha na jamii hufungamana kwa kuwa lugha ndiyo huwawezesha wanajamii kufahamiana, kubadilishana mawazo, kupashana habari, na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii. Aidha, lugha hukua kadiri inavyotumika katika shughuli hizo anuai za kijamii. Sanjari na hayo, maana na dhana mbalimbali zinazobebwa na maneno ya lugha hutokana na utamaduni wa jamii inayohusika pamoja na mazingira yao. Kwa hiyo, lugha ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano katika jamii yenye utamaduni mmoja. Aidha, lugha hukua kadiri inavyotumiwa na hufa isipotumiwa. Vilevile, kila lugha inajitosheleza katika mawasiliano ya jamii husika kwa sababu huweza kueleza yaliyopo, yaliyopita, yajayo na yanayofikirika.
| Shughuli ya 1.1 Fikiria umeshiriki katika kongamano linalowahusisha wanafunzi wenye tamaduni tofauti na utamaduni wako. Je, utatumia vipengele gani vya lugha kuutambulisha utamaduni wako? |
Hadhi ya Kiswahili
Soma shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.
Nataka nena na wewe, upate kunielewa,
Wengi washikwa kiwewe, kwa kushindwa nielewa,
Yapaswa unielewe, nimekwishakubaliwa,
Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha,
Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.
Huwezi kuwazuia, waliokubaliana,
Mimi wananitumia, wapate kuelewana,
Kanuni wazingatia, ili kuwasiliana.
Malengo pate fikia, wote kushirikiana,
Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.
Majina pia mavazi, vyote vyanitegemea,
Shughuli jamii hizi, lugha hii zatumia,
Kiswahili ni mzizi, kuunganisha jamia,
Ondokana na simanzi, kubali kunitumia,
Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.
Mimi nimekubalika, katika hii dunia,
Rasmi ni kutumika, kote kule Tanzania,
Duniani na Afrika, nimeweza kuendelea,
Kiswahili chasifika, lugha ya kimataifa,
Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda.
Maswali
1. Shairi ulilolisoma linazungumzia nini?
2. Sifa gani za Kiswahili zimebainishwa katika shairi hilo?
3. Unafikiri Kiswahili kina sifa gani nyingine tofauti na alizozieleza mwandishi?
4. Mstari unaosema, "Kiswahili ninatamba, hakuna wa kunishinda" una maana gani?
Zoezi la 1.1
Zingatia
Nchini Tanzania Kiswahili ndiyo lugha inayotumiwa na takribani Watanzania wote. Aidha, ni lugha inayowaunganisha Watanzania wote kama lugha kuu ya mawasiliano kwa kuwa hutumika katika shughuli kama vile; za kijamii za kila siku, za kiserikali, kisiasa, kidini na kibiashara. Pia, hutumika kutaja majina ya vitu vinavyowazunguka wasemaji wake na masuala mbalimbali ya utamaduni wao kama vile vyakula na mavazi. Vilevile, hutaja majina ya watu, mathalani; Pili, Lukasa, Juma, Furaha, Upendo na Amani. Hivyo, lugha ya Kiswahili ni utambulisho wa Mtanzania.
Matumizi ya lugha ya Kiswahili kama kielelezo cha utamaduni wa tanzania
Soma dayolojia ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.
Bibi: Hamjambo wajukuu zangu?
Wajukuu: Hatujambo. Shikamoo bibi.
Bibi: Marahaba wajukuu zangu. (Anaitikia akiwa anatabasamu.)
Wajukuu: Bibi ...! Tumeshamaliza kula, tumeshaosha vyombo, sasa tuko tayari kukusikiliza ili utueleze kuhusu maadili ya Watanzania kama ulivyotuahidi jana.
Bibi: Hahaaaa! Wajukuu zangu hamjasahau? (Aliuliza.)
Wajukuu: (Walijibu kwa pamoja.) Hatujasahau bibi.
Bibi: Sawa! Na mimi niko tayari kuwaeleza kuhusu suala hilo.
Wajukuu: Sawa bibi (Huku wakijiweka tayari kusikiliza.)
Bibi: Maadili ni suala muhimu kwa kila jamii. Kila jamii inatakiwa kuzingatia maadili kulingana na mila na desturi za jamii husika. Wakubwa kwa wadogo, wote wanatakiwa kuheshimiana na kuthaminiana. Mila na desturi za jamii hurithishwa na kuenziwa kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine. Hata ninyi wajukuu zangu mnapaswa kuishi kulingana na mila na desturi zetu.
|
|
Mjukuu wa 1: Mh! Kwani bibi tunatakiwa tufanyeje ili tuwaheshimu wengine?
Bibi: Swali zuri mjukuu wangu. Watoto wanatakiwa kuwaheshimu wakubwa. Mdogo akikutana na mkubwa, mdogo huanza kumsalimia mkubwa. Hata watu wa rika moja wanapokutana wanatakiwa kusalimiana kwa salamu inayoendana na rika lao. Kwa hiyo, salamu hutofautiana kulingana na rika.
|
|
Mjukuu na 2: Sasa bibi ...! Kwa nini salamu zinatofautiana? Salamu si salamu tu?
Bibi: Swali zuri sana. (Bibi alisema huku akitabasamu.) Salamu ni utaratibu ambao watu wamejiwekea na kukubaliana kuutumia kama sehemu ya maisha yao.
Mjukuu wa 3: Ahaaa, kumbe ...! Bibi, je kama wanatofautisha salamu, hutofautisha na maneno ya kutumia?
Bibi: Wajukuu zangu mu wadadisi sana. (Alisema huku akitabasamu.) Ndiyo! Katika kutumia lugha, kuna miiko katika matumizi ya baadhi ya maneno. Lengo la miiko hiyo ni kuleta heshima katika mazungumzo miongoni mwa wanajamii. Kuna baadhi ya maneno ambayo huwezi kuyatamka waziwazi. Pia, katika lugha yetu ya Kiswahili kuna utajiri huo wa kiutamaduni. Hivyo, katika mila na desturi zetu, hatutamki baadhi ya maneno waziwazi. Kwa mfano, mwanamke anapopata mtoto hatusemi amezaa mtoto badala yake tunasema amejifungua. Vilevile, mtu anapokwenda chooni, badala ya kusema kile anachotaka kwenda kufanya huko anasema ninakwenda kujisaidia au ninakwenda haja.
Mjukuu wa 4: Bibi, maneno hayo yalitamkwa kwa kificho tangu zamani?
Bibi: Ndiyo mjukuu wangu. Mila na desturi zinarithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Kiswahili kimesheheni maneno hayo ya kificho ambayo hujulikana kama tafsida.
Mjukuu na 4: Ahaaa! Sasa nimeelewa.
Mjukuu na 5: Bibi, hivi mtu akiumwa au kupatwa na matatizo tunatakiwa tufanyeje?
bibi: Swali zuri mjukuu wangu. Kwa hakika, tunapaswa kuishi kwa kujaliana na kufarijiana. Kujaliana na kufarijiana huonesha hali ya kuthaminiana. Kwa mfano, mtu anapougua au kupata changamoto yoyote ile katika jamii yetu, lugha yetu ina maneno kama vile pole ambayo hutumika katika kumfariji. Pia, katika kuonesha kujaliana, maneno kama asante na shukurani hutumika pale mtu anapokupa kitu au msaada fulani. Aidha, unapotaka kuomba kitu au msaada fulani shalt kutumia maneno yanayoonesha upole. Maneno hayo ni pamoja na samahani, tafadhali, ninaomba na mengine yanayofanana na hayo
Mjukuu wa 1: Kwa kweli leo nimejifunza mambo mengi kuhusu utamaduni wetu, hususani kuhusu maadili. Ninatamani uendelee kutueleza mengine zaidi.
Bibi: Safi! Ngoja niwajuze mengine wajukuu zangu. Katika maisha ni muhimu kusaidiana. lkitokea mdogo amekutana na mkubwa akiwa na mzigo, mdogo anapaswa kumsaidia mkubwa kubeba mzigo huo. Hata hivyo, si wadogo tu wanaotakiwa kuwasaidia wengine; hata watu wazima husaidiana. Hii ni alama ya ukarimu. Ukarimu ni sifa muhimu sana kwa kila Mtanzania.
|
|
Mjukuu wa 1: Bibi ...! Inaonekana katika lugha kuna hazina kubwa sana ya utamaduni wetu.
Bibi: Kabisa! Kabisa! (Bibi alivuta pumzi kidogo.) Kwa mfano, Lugha ya Kiswahili ni alama ya utambulisho wa utamaduni wetu. Kupitia lugha yetu ya Kiswahili tunaweza kuutambua, kuutunza na kuurithisha utamaduni wetu. Wageni pia hutambua utamaduni wetu kupitia lugha yetu.
Mjukuu wa 1: Bibi, leo umetufundisha mambo mengi sana. Tumejua namna utamaduni na lugha vinavyofungamana Pia, tumejua namna lugha yetu ya Kiswahili ilivyo kielelezo cha utambulisho wa utamaduni wa Mtanzania.
Bibi: Yapo mambo mengi yanayohusiana na lugha yetu ya Kiswahili na utamaduni wetu. Haya machache yanatosha kwa leo. Siku nyingine nitawaeleza mambo mengine yanayohusu lugha yetu. Twendeni tukalale ili kesho muweze kuwahi shuleni.
Wajukuu: Asante bibi. Kwaheri. (Wanaondoka kwenda kulala.)
Bibi: Kwaherini wajukuu zangu.
Maswali
1. Dayolojia uliyoisoma inahusu nini?
2. Kutokana na dayolojia uliyoisoma, kwa nini tunatumia tafsida?
3. Kwa nini ni muhimu kuishi kwa kufuata mila na desturi za jamii husika?
4. Utamaduni hurithishwa kwa njia gani?
5. Umejifunza nini kutokana na dayolojia uliyoisoma?
| Shughuli ya 1.2 Kusanya vitu mbalimbali vyenye maandishi ya lugha ya Kiswahili, kama vile misemo katika kawa na kanga, vinavyoweza kutambulisha utamaduni wa Mtanzania na kueleza namna lugha iliyotumika inavyotambulisha utamaduni wa Mtanzania. |
Zingatia
Utamaduni ni mfumo wa maisha ambao watu wa jamii fulani wamejiwekea katika kuendesha maisha yao ya kila siku. Lugha ni miongoni mwa vitambulisho vya utamaduni wa jamii husika. Mathalani, utamaduni wa Mtanzania huweza kutambulishwa na lugha ya Kiswahili. Hii hudhihirika katika mambo mbalimbali ambayo hufanywa na Watanzania kama sehemu ya utamaduni wao kupitia lugha ya Kiswahili. Aidha, vipengele mbalimbali vya kiutamaduni huelezwa kwa lugha; mathalani, majina ya vyakula. Vilevile, matumizi ya maneno ya lugha na maana zake hufungamana na utamaduni. Hivyo, lugha ni chombo na nyenzo inayobeba utamaduni wa wazungumzaji wa lugha husika.
| Shughuli 1.3 Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, vikiwemo vya mkondoni vinavyoaminika, sikiliza masimulizi yenye maudhui ya utamaduni wa Mtanzania, kisha bainisha vipengele vya utamaduni vilivyobainishwa. |
Umuhimu wa kujifunza Kiswahili
Soma mahojiano baina ya Mwandishi wa habari na Mwalimu, kisha jibu maswali yanayofuata.
Siku moja, mwandishi wa habari alifanya mahojiano na Mwalimu wa somo la Kiswahili kuhusu umuhimu wa kujifunza Somo la Kiswahili. Katika mahojiano hayo, mambo mbalimbali yalizungumziwa ambayo ni zao la kujifunza Somo la Kiswahili. Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwalimu: Habari ndugu mwandishi!
Mwandishi: Nzuri mwalimu!
Mwalimu: karibu sana.
Mwandishi: Asante. Mwalimu, baadhi ya watu hawaoni umuhimu wa kujifunza Kiswahili. Wewe una maoni gani?
Mwalimu: Kwa kweli, hayo ni mawazo potofu. Tuelewe kuwa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania hutumika kufundishia masomo yote katika shule za msingi na vyuo vya ualimu vinavyotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Pia, Kiswahili hufundishwa kama somo katika elimu ya sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu. Hii ina mchango mkubwa sana kwa wajifunzaji kwani inawasaidia kuwa mahiri katika lugha ya Kiswahili.
Mwandishi: Mbali na umuhimu huo, kuna umuhimu mwingine?
Mwalimu: Ndiyo. Lugha ya Kiswahili inatumika kuwaunganisha Watanzania wote. Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni sitini wenye makabila tofauti lakini wanaunganishwa na lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao. Aidha, Kiswahili kinachangia katika kukuza uchumi, amani, na utulivu nchini Tanzania na katika nchi za jirani. Isitoshe, wakati wa kupigania uhuru, lugha ya Kiswahili ilitumika kama chombo muhimu cha umoja na mawasiliano.
Mwandishi: Ooh! Hakika mwalimu. Kuna kingine zaidi?
Mwalimu: Ndiyo ndugu mwandishi. Lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi pia. Inatumika katika shughuli mbalimbali za kielimu, kiuchumi na kiserikali katika taasisi na vyombo vya Bola kama vile mahakama na bunge. Vilevile, Kiswahili kama lugha ya taifa hutumika kama utambulisho wa taifa letu. Kwa hiyo, Kiswahili kina nafasi kubwa katika nyanja zote za maendeleo ya taifa.
Mwandishi: Kiswahili kina hadhi gani kimataifa?
Mwalimu: Kiswahili kimepata hadhi ya kutumika kimataifa. Hadhi hii imekifanya Kiswahili kuwa lugha pekee ya Kiafrika iliyotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kupewa siku maalumu ya tarehe 07/07 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani. Aidha, hii ndiyo lugha pekee ya Kiafrika ambayo imesambaa zaidi kuliko lugha zingine. Hivyo, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuleta umoja barani Afrika. Vilevile, Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika iliyopendekezwa kutumika katika vikao vya Umoja wa Afrika sanjari na lugha zingine za kimataifa. Aidha, Kiswahili kinatumika kama lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mwandishi: Ni fursa zipi ambazo Watanzania wanafaidika nazo kutokana na kupanda hadhi kwa lugha ya Kiswahili?
Mwalimu: Kiswahili hutoa fursa za ajira; kwa mfano, baadhi ya Watanzania wenye taaluma ya kufundisha Kiswahili hujipatia fedha kutokana na kufundisha Kiswahili ndani na nje ya nchi. Aidha, kupitia taaluma ya ukalimani na tafsiri Watanzania huweza kupata ajira. Vilevile, kutokana na umuhimu wa Kiswahili kutumika nje ya nchi, baadhi ya nchi kama vile Afrika Kusini, Nigeria na Sudani Kusini zimekuwa zikihitaji wataalamu wa Kiswahili kwenda kukifundisha katika nchi hizo. Hizo zote ni fursa.
Mwandishi: Sasa turudi kwa wanafunzi. Je, wanafunzi wanapojifunza somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari wanapata manufaa gani?
Mwalimu: Mwanafunzi akijifunza kikamilifu somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari, ataweza kuwasiliana kwa Kiswahili fasaha katika nyanja mbalimbali za maisha na kukithamini Kiswahili kama sehemu muhimu ya utamaduni wa Mtanzania. Vilevile, husaidia kujenga tabia ya udadisi na ubunifu katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiswahili pamoja na kuelewa, kuthamini na kutumia kazi za fasihi katika maisha. Aidha, ataweza kutumia lugha hii katika miktadha mbalimbali, kuikuza, kuieneza na kukuza matumizi yake katika mawasiliano ya kitaifa na kimataifa. Vilevile, atajenga uwezo wa kujisomea maandiko mbalimbali ya Kiswahili. Pia, atapata msingi bora na imara wa kujifunza na kujiendeleza katika taaluma za Kiswahili kama vile uhariri, ukalimani na tafsiri na kukitumia kupata maarifa, mwelekeo, na stadi za kijamii, kitamaduni, kiteknolojia, na kitaaluma kwani lugha ni kibebeo cha maarifa.
Mwandishi: Mwalimu, ninakupa nafasi ya kumalizia suala hili muhimu, kama una lolote la kuongezea ili tuhitimishe.
Mwalimu: Ndugu mwandishi, ninapenda kumalizia kwa kueleza kwamba, lugha ya Kiswahili, kama zilivyo lugha zingine, inaweza kutumika kutolea maarifa na ujuzi wa taaluma mbalimbali kama vile habari na mawasiliano, historia, sayansi na teknolojia. Hivyo, tuithamini na kuitumia zaidi.
Mwandishi: Asante sana mwalimu kwa maelezo yako ya kina kuhusu umuhimu wa kujifunza Kiswahili.
Mwalimu: Asante na karibu tena.
Mwandishi: Shukurani.
Maswali
Zoezi la marudio la 1
1. Jibu maswali kwa kuandika herufi ya jibu sahihi.
(i) Ipi kati ya tungo zifuatazo si dhima ya lugha katika mawasiliano?
(ii) Vipengele vipi vya lugha kati ya vifuatavyo hubainisha utamaduni wa Mtanzania?
(iii) Ni jambo gani muhimu katika kufasili lugha kati ya mambo yafuatayo?
(iv) Ipi kati ya zifuatazo ni sababu ya kuzingatia lugha na utamaduni wake?
(v) Ipi kati ya zifuatazo ni fursa itolcanayo na lugha ya Kiswahili?
2. Oanisha dhana zilizopo katika Orodha A na maelezo yaliyopo katika Orodha B kwa kuchagua herufi ya jibu sahihi.
| Orodha A | Orodha B |
|
|
3. Eleza umuhimu wa kulinda na kuheshimu utamaduni wa Kitanzania.
www.learninghubtz.co.tz