Sura ya 01 : Wajibu na haki za mtoto katika jamii na Taifa
Utangulizi Wajibu na haki za mtoto ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto katika jamii na Taifa.Ulipokuwa Darasa la Tatu,uljifunza kuhusu wajibu na haki za mtoto shuleni na nyumbani.Katika sura hii,utajifunza kuhusu wajibu na haki za mtoto katika jamii na Taifa.Umahiri utakaoupata utakuwezesha kutambua wajibu na haki za mtoto katika jamii na Taifa.Hivyo,kukuwezesha kutekeleza wajibu wako ili kurahisisha kupata haki zako katika jamii na Taifa kwa ujumla. |
Fikiri Wajibu na haki za mtoto katika jamii na Taifa |
Dhana ya wajibu na haki za mtoto
Kazi ya kufanya namba 1 Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali,ikiwamo maktaba mtandao kuhusu wajibu na haki za mtoto katika jamii na Taifa. |
Wajibu ni mambo ya lazima ambayo mtu hupaswa kuyatenda li kukabili mazingira yanayomzunguka.Wajibu huambatana na sheria za jamii na Taifa ambazo ni lazima kuzitekeleza na kuzitimiza.Hii ina maana usipotimiza wajibu,utaonekana kuwa mtu wa tofauti.Ibara ya 25-28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuhusu wajibu wa Watanzania wote na hata ambao siyo Watanzania lakini wanaishi Tanzania. Vilevile, kuna sheria zinazofafanua wajibu wa mtu mzima na watoto. Wajibu huo umezingatia umri, jinsi, na madaraka ili kurahisishia utekelezaji wake kulingana na matarajio ya jamii na Taifa. Hivyo, mtu asipotimiza wajibu fulani, anawajibishwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusika.
Haki hutofautiana na wajibu. Haki hujumuisha matendo au vitu vya msingi ambavyo mtu anastahili kupata na kutendewa katika jamii inayohusika. Mtoto huzaliwa na hulelewa katika jamii, ambayo hujumuisha familia, ukoo, kabila, Kijiji/Mtaa, Kata, Tarafa na Taifa. Mazingira haya ni msingi wa mtoto kupata haki zake. Aidha, kutokana na msisitizo wa haki za binadamu, haki za mtoto zimewekwa kisheria zikieleza ni kipi ambacho mtu mzima, jamii na Taifa hupaswa kutimiza kwa mtoto kama haki zake. Haki hizo zinalenga kueleza namna jamii inavyopaswa kumpa mtoto ulinzi, mahitaji muhimu na nafasi za ushiriki katika kujenga jamii na Taifa. Kimsingi, mahitaji ya mtoto ndiyo hutafsiri haki za mtoto kuanzia katika ngazi ya familia, jamii na Taifa.
Haki za mtoto katika jamii na Taifa
Kazi ya kufanya namba 2 Jadili haki za mtoto katika jamii na Taifa kama zilivyotafisiriwa katika sheria ya mtoto, sura ya 13 ya mwaka 2009 na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. |
Haki za mtoto zimetafsiriwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mataifa mbalimbali. Kwa mfano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya Kwanza, Sehemu ya Tatu, Ibara ya 12-24, inaeleza kuhusu haki za binadamu akiwa mtoto katika jamii na Taifa. Pia, haki za mtoto zimeelezwa katika sheria ya mtoto, Sura ya 13 ya Mwaka 2009, toleo la mwaka 2019. Haki hizo zinatambuliwa kisheria na inakatazwa mtu au mamlaka yoyote kukiuka haki hizo katika jamii na Taifa. Uwapo wa haki hizo, unatoa nafasi kwa mtoto kulindwa dhidi ya ukiukwaji wa haki za mtoto kunakoweza kusababisha unyanyasaji, ukatili na udhalilishaji wa mtoto. Mtoto si wa familia peke yake, bali ni mali ya jamii na Taifa kwa ujumla, ndiyo maana haki za mtoto, zimetafsiriwa katika ngazi ya jamii na Taifa. Kielelezo namba 1, kinaonesha baadhi ya haki za mtoto katika jamii na Taifa.
Kielelezo namba 1: Haki za mtoto katika jamii na Taifa |
 Kupata elimu na kujielimisha
Familia inajukumu la msingi la kumpa mtoto elimu. Aidha, jamii na Taifa wana wajibu wa kumwendeleza mtoto kwa kumpa elimu. Hii ni pamoja na kumpa elimu ya mila na desturi za jamii na Taifa. Pia, haki hii humpa mtoto nafasi ya kupata habari na elimu ya kutosha ili aweze kujitambua na kuchangia katika maendeleo ya jamii na Taifa. Aidha, mtoto ana wajibu wa kusoma kwa bidii ili kupata elimu iliyokusudiwa. Kielelezo namba 2, kinaonesha watoto wakiwa darasani wakipata elimu.
Kielelezo namba 2: Watoto wakiwa darasani wakipata elimu |
Serikali imeweka programu za kutoa elimu bila malipo katika shule zinazo milikiwa na serikali nchini kote. Pia, imeimarisha miundombinu katika shule hizo, na kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuwapatia watoto elimu kama haki yao ya msingi. Hii inafanyika ili kuweka fursa sawa ya kupata elimu kwa kila mtoto ambaye ni haki stahiki. Haki ya elimu huwezesha kila mtoto kupata maarifa na ujuzi utakaomwezesha kuchangia katika maendeleo yake, ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Kuheshimiwa, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake
Mtoto ana haki ya kuheshimiwa, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Hii ni pamoja na kutohusishwa katika aina yoyote ya udhalilishaji utakaomvunjia heshima mtoto. Haki hii ni ya msingi ili kumpa mtoto haki ya faragha na usalama dhidi ya vitendo vya ukatili, unyonyaji, unyanyasaji na udhalilishaji.
Kazi ya kufanya namba 3 Jadili na andika matendo yanayoashiria mtoto kuheshimiwa, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake katika jamii. |
Kulindwa na kupata haki sawa
Kila mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya mateso, vitisho na kupewa adhabu zinazomdhalilisha. Kimsingi, haki hii inahusu ulinzi wa mtoto dhidi ya ukatili, unyanyasaji, uonevu na udhalilishaji wa aina yoyote katika jamii yake na Taifa. Vyombo vya ulinzi kuanzia ngazi za Mtaa/Kijiji, Kata hadi Taifa vimewekwa kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mtoto. Aidha, endapo mtoto atafanyiwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji, uonevu na udhalilishaji, ana wajibu wa kutoa taarifa katika vyombo vya usalama ili kupata msaada.
Kazi ya kufanya namba 4 Chunguza na andika zilipo ofisi za Mtaa/Kijiji, Kata na Taifa maeneo yanayokuzunguka ambapo mtoto anaweza kutoa taarifa iwapo haki zake zitakiukwa. |
Kusikilizwa kwa ukamilifu
Mtoto ana haki ya kushiriki na kujadili masuala yanayomhusu katika mikutano na vikao katika jamii inayomzunguka. Hivyo, ana haki ya kutoa mawazo yake bila kuathiri sheria za nchi katika jamii na Taifa. Haki hii humpa mtoto nafasi ya kushiriki katika kutoa uamuzi wa masuala yanayohusu ustawi wake. Mtoto ni raia kama walivyo raia wengine katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
KUTOKUBAGULIWA KWA NJIA YOYOTEÂ
Mtoto ana haki ya kutobaguliwa kwa njia yoyote iwe kwa rangi, jinsi, hali ya maisha, dini au hali itakayomfanya kuwa dhaifu na duni. Mtoto ana haki ya kutambua ndugu na jamaa zake katika familia, ukoo na jamii inayohusika. Haki hii kimsingi inazuia mtoto kubaguliwa na kutoa nafasi kwake ya kupata huduma za kijamii na kisheria ili kumlinda dhidi ya ubaguzi na unyanyasaji katika jamii inayomzunguka.
ZOEZI NAMBA 1Â
1. Eleza matendo yanayoashiria kubaguliwa kwa mtoto.
2. Anisha huduma anazostahili kupata mtoto katika jamii na Taifa kwa ujumla.
KUPATA HIFADHI YA MAISHA KATIKA JAMII NA TAIFAÂ
Mtoto ana haki ya kuishi kama mtu huru katika jamii na Taifa. Haki hii inakataza mtoto kutungiwa ndani, kuhamishwa kwa nguvu, au kunyanyaswa kwa nguvu uhuru wake kutoka katika familia, jamii au Taifa lake. Aidha, mtoto anaweza kupata hifadhi katika sehemu nyingine nje ya familia yake pale itakapothibitika kuwa anateseka akiwa ndani ya familia yake.
HAKI YA KUJUA UTAMADUNI WA JAMII NA TAIFA LAKEÂ
Mtoto ana haki ya kujua utamaduni wa jamii na Taifa lake. Haki hii humpa mtoto nafasi ya kufahamu lugha ya jamii yake, vyakula, mavazi na michezo katika jamii na Taifa lake. Pia, utamaduni humpa mtoto nafasi ya kumbua miko na imani za jamii yake yanayokubalika na yasiyokubalika katika jamii na Taifa lake. Vilevile, humpa mtoto nafasi ya kupata matendo na elimu ya malezi na maadili bora yanayoendana na mila na desturi za jamii na Taifa kwa ujumla.
Kazi ya kufanya namba 5 Jadili umuhimu wa mtoto kutambua utamaduni wa jamii na Taifa lake wakati huu wa usasa na utandawazi. |
Haki hizi za mtoto zinapaswa kulindwa na watu wote kuanzia katika ngazi ya familia, jamii na Taifa. Aidha, serikali kwa kutambua hilo, imeweka maofisa wanaosimamia utekelezaji wa haki za mtoto katika ngazi za Mitaa, Vijiji, Kata, Wilaya, Mikoa na Taifa. Pia, vituo vya usalama, mfano polisi vina dawati la masuala ya jinsia na ulinzi wa watoto. Dawati hili husimamia utekelezaji wa haki za mtoto. Vilevile, ofisi za Kata na Mtaa/Kijiji zina maofisa wanaosimamia haki za watoto. Aidha, viongozi wa asasi za kidini husimamia utekelezaji wa haki za mtoto katika jamii na Taifa. Walimu katika ngazi zote za elimu wana wajibu wa kulinda na kusimamia haki za mtoto. Watu hawa wote wana wajibu wa kusimamia ulinzi na usalama wa mtoto ili kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa ipasavyo. Hivyo, kuwezesha katika ukuaji wa mtoto kiakili, kimwili, kisaikolojia, kimaono na kiroho.
Kazi ya kufanya namba 6 Jadili changamoto zinazoweza kuwakabili watoto katika upatikanaji wa haki zao na jinsi ya kuzitatua katika jamii inayokuzunguka. |
Wajibu wa mtoto katika jamii na Taifa
Sheria ya mtoto ya mwaka 2009, toleo la mwaka 2019 imeeleza wazi wajibu wa mtoto katika jamii na Taifa lake.
Kazi ya kufanya namba 7 Jadili wajibu wa mtoto katika jamii na Taifa kama ilivyotafsiriwa katika sheria ya mtoto ya mwaka 2009, toleo la mwaka 2019 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. |
Kimsingi,watoto wana wajibu wa kutekeleza katika jamii na Taifa.Sheria ya mtoto na Katiba vinaeleza wajibu wa mtoto katika familia,jamii na Taifa.Hii ni kwa sababu mtoto ni sehemu ya jamii na Taifa.Kielelezo namba 3,kinaonesha watoto wenye mabango yenye baadhi ya wajibu wa mtoto
Kielelezo namba 3:Wajibu wa mtoto katika jamii na Taifa |
Kupenda kufanya kazi
Mtoto ana wajibu wa kufanya kazi katika jamii na Taifa kulinganana umri na uwezo wake.Mtoto anapofanya kazi hujenga mshikamano na jamii na Taifa lake.Pia,humfanya mtoto kukubalika katika jamii yake.Jamii zote hukemea uvivu na kutokupenda kufanya kazi.Hivyo,ni wajibu wa mtoto kupenda na kufanya kazi ili kuwa na tabia zinazokubalika katika jamii na Taifa.Kielelezo namba 4,kinaonesha watoto wakishiriki kusafisha mazingira katika jamii.
Kazi ya kufanya namba 8 Fanya uchunguzi,kisha andika kazi ambazo mtoto anaweza kushiriki katika jamii inayomzunguka. |
Kielelezo namba 4: Watoto wakishiriki kusafisha mazingira |
Kutii sheria na kanuni za nchi na za jamii
Utii wa sheria na kanuni huwezesha watu kuishi kulingana na maadili ya jamii na Taifa husika.Mtoto ana wajibu wa kutii sheria na kanuni zilizopo katika jamii na Taifa lake.Mtoto asipotii sheria za nchi,huweza kufikuta katika matatizo na vyombo vinavyosimamia sheria hizo.Aidha,utii wa sheria na kanuni za nchi ni muhimu kwa usalama wa mtoto mwenyewe.
Kazi ya kufanya namba 9 Soma matini kuhusu sheria za nchi,kisha andika wajibu wa mtoto katika kuzitii sheria hizo. |
Kutunza,kuheshimu na kulinda mali za umma na za jamii
lbara ya 27(1)na 27(2)ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania ya Mwaka 1977,inaeleza wajibu wa kulinda mali asilia za Taifa,mali za mamlaka ya nchi na mali zinazomilikiwa kwa pamoja na wananchi.Pia,inaelezea wajibu wa kuheshimu mali ya mtu mwingine.Watu wote wanatakiwa kupiga vita uharibifu na ubadhirifu wa mali za umma na za jamii na kuendesha uchumi wa Taifa kwa umakini kwa ajli ya kizazi cha sasa na kijacho. Hivyo,mtoto ana wajibu wa kutunza na kulinda maliasili za Taifa,mali za umma na za jamii na kutokushiriki vitendo vya uharibifu wake.Pia,mtoto ana wajibu wa kushiriki katika kutoa elimu na kuandaa kampeni za kutunza mali za umma katika jamii.Mfano,mtoto anaweza kufanya kampeni kwa kushiriki shughuli za kutunza mazingira katika jamii.Kielelezo namba 5, kinaonesha watoto wakishiriki kazi za kupanda miti.
Kazi ya kufanya namba 10 Andaa klabu ya utunzaji na ulinzi wa mali zilizopo katika jamii kwa kuonesha mikakati na utekelezaji wake. |
Kielelezo namba 5:Watoto wakishiriki kupanda miti |
Kuonesha heshima na utii katika jamii
Mtoto ana wajibu wa kuheshimu watu waliomzidi umri,pamoja na watoto wenzake bila ya kujali rangi,hali ya maisha au jinsi. Heshima inaweza kuoneshwa kwa kusalimia watu wengine, kukubali kutumwa na kufanya kazi bila kuonesha kiburi.Pia, mtoto anaweza kuonesha heshima kwa kuwasaidia wazee, watu wenye mahitaji maalumu na watu wengine katika jamii yake na Taifa kwa ujumla.Aidha,mtoto kuonesha unyenyekevu na kukubali kuelekezwa katika mambo halali na ya msingi ni sehemu ya kuonesha heshima na utii katika jamii.Wajibu huu ni muhimu kwa mtoto ili kukubalika katika jamii.Licha ya kuonesha heshima kwa watu wengine,mtoto ana wajibu wa kujiheshimu.
Kazi ya kufanya namba 11 Jadili na orodhesha matendo yanayoonesha kujiheshimu na ya kutojiheshimu katika jamii inayokuzunguka |
Matendo ya kujiheshimu kwa mtoto ni yale yanayokubalika na jamii yake.Matendo ya kutojiheshimu ni yale yasiyokubalika na jamii yake.Mtoto hapaswi kuiga na kutenda matendo yaliyo kinyume na maadili ya jamii na Taifa lake.Pia,mtoto ana wajibu wa kukubali na kufuata kanuni na sheria ambazo jamii imejiwekea ili kuishi salama katika jamii yake.
Zoezi namba 2
1.Eleza umuhimu wa mtoto kujiheshimu katika jamii yake.
2.Je,kuna umuhimu gani wa mtoto kuwaheshimu watu wengine katika jamii?
Kuzingatia maadili ya jamii
Ni wajibu wa mtoto kuzingatia maadili ya jamii na Taifa.Maadil hayo ni pamoja na kuonesha uaminifu na uadilifu katika uhusianc wake na watu wengine.Pia,ana wajibu wa kutojihusisha ne vitendo vya rushwa na uhalifu mwingine kama vile matumiz ya dawa za kulevya.Kwa kufanya hivyo,mtoto anaendeleze maadili katika jamii yake na Taifa.
Kaziya kufanya namba 12 Waulize wazazi au walezi kuhusu maadili ya jamii inayokuzunguka na andika wajibu wako katika kuyatekeleza. |
Kushiriki katika shughuli za jamii na Taifa lake
Ni wajibu wa mtoto kushiriki katika shughuli za jamii na Taifa lake.Mtoto anaweza kushiriki katika shughuli za jamii.Kwa mfano,shughuli za mazishi,ibada,harusi,sherehe za kitaifa, na shughuli zingine za maendeleo kulingana na umri wake.Pia, mtoto anaweza kushiriki katika kazi mbalimbali katika jamii na Taifa.Vilevile,anaweza kushiriki katika vikao vya maendeleo ya jamii yake.Ushiriki huu,humjenga mtoto kimaadili na huonesha kuwajibika katika jamii na Taifa.Pia,ushiriki humjengea mtoto tabia ya kujali,kuhudumia na kuwajibika kwa wengine.Kielelezc namba 6,kinaonesha ushiriki wa watoto katika kikao cha maendeleo ya jamii.
Kielelezo namba 6:Watoto wakishiriki kikao cha maendeleo ya jamii |
Kulinda,kuhifadhi na kudumisha uhuru na umoja wa kitaifa Umoja wa kitaifa ndiyo nguzo ya mshikamano wa kindugu baina ya wanajamii.Umoja huu hutafsiriwa katika namna ambayo watu huungana na kushirikiana katika mambo ya kitikadi,kimani na kiutamaduni.Watu wenye kukubaliana katika itikadi,imani na utamaduni ni rahisi kuwa na umoja kijamii na kitaifa.Umoja wa kitaifa huweka mazingira salama ya watu kuhusiana na kushirikiana katika kazi ambazo ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na Taifa.Ukosefu wa umoja wa kitaifa,huondoa amani na huleta ugomvi,migogoro na mpasuko.Hivyo,ni wajibu wa watoto kulinda,kuhifadhi na kudumisha uhuru na umoja wa kitaifa na katika jamii inayomzunguka.
Kazi ya kufanya namba 13 Jadili namna ambavyo mtoto anaweza kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru na umoja wa Taifa. |
Mtoto anaweza kulinda,kuhifadhi na kudumisha uhuru na umoj: wa jamii na Taifa kwa kuonesha upendo kwa watu wengine kushirikiana na kuthamini utu wa binadamu wenzake.
Kulinda usalama na amani ya jamii na Taifa
Pamoja na Taifa kuwa na vyombo vya kusimamia usalame wa raia na mali zao,mtoto ana wajibu wa kulinda usalama ne amani ya jamii na Taifa lake.Wajibu huu humpa mtoto nafas ya uwajibikaji katika ulinzi na usalama wa jamii na Taifa lake.
Kazi ya kufanya namba 14 Jadili namna mtoto anavyoweza kushiriki katika kulinda usalama na amani ya jamii na Taifa. |
Mtoto ana wajibu wa kutoa taarifa kwenye ofisi za Mtaa/Kijiji au polisi,iwapo ataona mazingira hatarishi ya uvunjaji wa sheria na kanuni za jamii au nchi ili kulinda usalama na amani ya jamii na Taifa lake.Pia,ni wajibu wa mtoto kutoa taarifa za vitendo viovu kama vile wizi,ugomvi,udhalilishaji,ukatili na unyanyasaji.
Kujifunza utamaduni wa jamii na Taifa
Mtoto ana wajibu wa kujifunza mambo mema ya utamaduni wa jamii na Taifa lake.Jamii ina mila na desturi zinazoongoza wanajamii ili kuishi kulingana na mahitaji yao.Mila na destur hizi hueleza namna jamii inavyopaswa kuishi,kushirikiana na kuhusiana.Pia,huelezea mienendo ya jamii kiimani,kielimu, kimaadili na maarifa na ujuzi wa jamii inayohusika.Vilevile: hueleza malezi,tabia njema na jinsi ya kujifunza.Kwa ujumla mila na desturi hubeba utambulisho wa jamii,ambao hutofautisha jamii moja na nyingine.Hivyo,ni wajibu wa mtoto kujifunza mambo mema ya utamaduni wa jamii yake na Taifa lake,ili kuishi kulingana na mahitaji ya jamii yake na Taifa lake.
Kazi ya kufanya namba 15 Waulize wazazi au walezi kuhusu mila na desturi za jamii yako,kisha andika wajibu wako katika kuzitekeleza. |
Kimsingi,mtoto ana wajibu wa kujifunza na kuendeleza utamaduni wa jamii inayomzunguka.Hivyo,mtoto anapaswa kujifunza utamaduni wa jamii yake kutoka kwa wazazi,walezi na watu wengine katika jamii.Aidha,mtoto ana wajibu wa kujifunza na kuheshimu mila na desturi zinazoendeleza amani,utulivu, utu na heshima.
Kujilinda na kujijali
Mtoto anao wajibu wa kujlinda na kujijali.Kujilinda ni kujikinga dhidi ya mazingira hatarishi kwa kuepuka kuwa katika maeneo hatarishi.Mfano,kutokutembea usiku,kutokwenda katika vilabu vya pombe au magenge ya wavuta bangi na dawa za kulevya.Mtoto hapaswi kuangalia picha chafu kwenye mitandao ya kijamii au kujihusisha katika urafiki wa kimapenzi akiwa na umri mdogo.Mtoto anatakiwa kuwa katika maeneo salama na kuepuka maeneo ya uficho na kujitenga na watoto wengine. Pia,mtoto hapaswi kuiga vitendo viliyo kinyume na maadili ya jamii na Taifa lake.
Kaziya kufanya namba 16 Jadili namna mtoto anavyoweza kujilinda na kujijali katika mazingira yake. |
Kuwaheshimu viongozi wa serikali
Mtoto ana wajibu wa kuwaheshimu viongozi wa serikali katika ngazi zote za uongozi.Hii ni kuanzia ngazi za Mtaa/Kijiji,Kata, Wilaya,Mkoa na Taifa.Mtoto ana wajibu wa kuwaheshimu, kushirikiana nao na kuwatii katika matendo yaliyo mema ili kuwezesha utekelezaji wa kazi za ustawi wa jamii na Taifa zima. Heshima kwa viongozi,humsaidia mtoto kupata msaada na haki zake.
Zoezi namba 3
1. Â Eleza umuhimu wa mtoto kuheshimu na kushirikiana na viongozi wa serikali katika matendo yaliyo mema.
2.Orodhesha matendo yanayoashiria mtoto kujilinda na kujijali.
Kupinga vitendo dhidi ya rushwa
Mtoto anao wajibu wa kupinga vitendo vya rushwa kwani vinadhoofisha maendeleo ya jamii na Taifa.Vitendo vya rushwa huwanyima watu kupata haki na huduma bora katika jamii na Taifa.Pia,husababisha ufujaji na ubadhilifu wa rasilimali za umma.Hivyo,mtoto ana wajibu wa kupinga vitendo vya rushwa na kushiriki kwa vitendo kulinda rasilimali za umma.Hii ni pamoja na kutoa taarifa za matumizi mabaya ya rasilimali za umma na kutumia vizuri miradi ya maendeleo kama vile miundombinu ya reli,barabara,majengo ya shule,miradi ya maji,visima, mabomba na vinginevyo katika jamii inayomzunguka.Pia,wajibu huu,unaweza kutekelezwa kwa kutoa elimu ya namna ya kuzuia na kupambana na rushwa na madhara ya rushwa.Mfano,kutoa elimu kupitia nyimbo,ngonjera,vipindi maalumu katika redio, runinga na matamasha ya kitaifa.Vilevile,mtoto ana wajibu wa kutoa taarifa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)akigundua vitendo vya rushwa katika jamii yake. Kielelezo namba 7,kinaonesha watoto wenye mabango ya kupinga vitendo vya rushwa.
Kielelezo namba 7:Watoto wakishiriki kupinga rushwa |
Kazi ya kufanya namba 17
Orodhesha miradi ya maendeleo inayotekelezwa naserikali,kisha:
1.Andika faida ya jamii kushiriki katika kuzuia vitendovya rushwa katika miradi hiyo.
2.Andika madhara ya vitendo vya rushwa katika miradihiyo.
Kushirikiana na watoto wengine katika jamii na Taifa Watoto ndio tegemeo la jamii na Taifa.Hivyo,ni wajibu wa mtoto kushirikiana na watoto wengine katika jamii na Taifa ili kujenga misingi ya maendeleo ya jamii zao.Ushirikiano na watoto wengine katika jamii na Taifa huwajengea uwezekano wa kufanya kazi pamoja sasa na baadaye.Pia,hujenga umoja wa watoto kitaifa.Hivyo,ni wajibu wa watoto,kushirikiana na watoto wengine ili kujenga uhusiano na umoja kati yao kwa maendeleo ya jamii na Taifa.
Kazi ya kufanya namba 18
Jadili namna mtoto anavyoweza kushirikiana na watoto wengine katika jamii na Taifa.
Wajibu huu wa mtoto,umeambatana na sheria,hivyo,mtt anapokiuka wajibu anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kazi ya kufanya namba 19
Jadili mambo uliyojifunza kuhusu wajibu wa mtoto katika jamii na Taifa.
Umuhimu wa wajibu na haki za mtoto katika jamii na Taifa
Kazi ya kufanya namba 20
Jadili umuhimu wa haki na wajibu wa mtoto katikajamii na Taifa.
Wajibu na haki za mtoto ni muhimu kwa mtoto binafsi,jamii naTaifa.Haki na wajibu wa mtoto ni muhimu kwani husaidia kuleta ulinzi,heshima na fursa kwa watoto katika jamii na Taifa.Pia, mtoto anayetambua haki na wajibu wake,hutekeleza wajibu wake,na hudai haki zake.Hivyo,kumwezesha kupata haki zake katika jamii na Taifa.Aidha,jamii inayotambua haki na wajibu wa mtoto inaweza kumsaidia mtoto kutimiza wajibu wake.Hivyo, kupata haki zake.Kwa ujumla haki na wajibu humsaidia mtoto:
(a)Kujikinga dhidi ya ukatili,unyanyasaji na udhalilishaji kwa mtoto;Â Mtoto anayetambua haki zake katika jamii na Taifa ni rahisi kufahamu vitendo vilivyo kinyume na haki zake.Hivyo,kuchukua hatua za kujilinda kwa kudai haki zake.Pia,huweza kutoa taarifa katika vyombo na mamlaka zinazohusika au mashirika yanayoshughulikia masuala ya watoto.Vilevile,anaweza kuwasaidia watoto wenzake kutambua haki zao kama watoto.Kimsingi,hii humsaidia mtoto kujilinda na ukatili,unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya watoto.
(b)Kujitambua na kuchukua hatua stahiki za usalama; Mtoto anayefahamu haki zake,huweza kujitetea katika mazingira yanayomzunguka.Pia,huweza kujisimamia dhidi ya vitendo vya unyanyasaji,udhalilishaji na ukatili katika jamii.Aidha,mtoto anayetekeleza wajibu wake,huweza kuishi maisha salama na kupata fursa mbalimbali katika jamii na Taifa.
(c)Kujenga uhusiano katika jamii na Taifa;Â Mtoto anayejua haki zake na kutekeleza wajibu wake,ni rahisi kujenga uhusiano mwema na kushirikiana na watu wengine katika jamii na Taifa.Kwa mfano,mtoto anayejua haki ni rahisi kushiriki katika mijadala ya kijamii na kisiasa kuhusu masuala yanayohusu watoto.Hivyo,humwezesha kujenga uhusiano na watu wengine katika jamii na Taifa.
(d)Kuwa raia mwema;Â Mtoto anayefahamu haki zake na wajibu wake,ni rahisi kuwa raia mwema katika jamii na Taifa.Utekelezaji wa haki na wajibu wa mtoto katika jamii na Taifa,huwezesha watoto kujitambua na kuishi katika misingi ya maadili,haki na usawa katika jamii.
(e)Kujenga maadili;Â Kujua haki zake,humsaidia mtoto kutenda vitendo vyenye maadili.Pia,humwezesha kufanya uamuzi wenye maadili kuhusu tabia zake na kutambua jinsi ya kuwatendea mema watu wengine.
(f)Kuimarisha ustawi wake katika jamii na Taifa; Mtoto kufahamu haki zake na kutekeleza wajibu wake,huimarisha ustawi wake kijamii na kitaifa.Haki na wajibu wa mtoto huongeza ushiriki wa mtoto katika shughuli za kijamii na Taifa.Hivyo,humwezesha kuimarisha usalama na ulinzi wa mtoto Kimsingi,wajibu na haki za mtoto katika jamii huweka mazingira ya mtoto kushiriki katika ujenzi wa jamii na Taifa bora,na hivyo, kujipatia mahitaji yake.Pia,husaidia mtoto kupata ulinzi,na kuwa salama katika jamii.Jamii inayozingatia haki za mtoto na yenye watoto wanaotimiza wajibu wao,huwa ni mahali salama pa kuishi.
Msamiati
Katiba ni sheria na kanuni zinazoainisha jinsi nchi itakavyoendeshwa
Kanuni mwongozo au taratibu zinazotumika kuelekeza tabia au shughuli za kundi fulani kanuni au taratibu zilizowekwa na mamlaka fulani
Sheria kwa ajli ya kuelekeza au kuthibiti tabia za kikundi au jamii Fulani
www.learninghubtz.co.tz
Zoezi la Marudio
1.Andika neno NDIYO mbele ya sentensi ambayo ni kweli na neno HAPANA mbele ya sentensi ambayo si kweli.
(i)Mtoto hana haki ya kusikilizwa kwa ukamilifu katika jamii yake .
(ii)Haki za mtoto ni kinga dhidi ya ukatii,unyanyasaji na udhalilishaji kwa mtoto .
(ii)Wajibu na haki za mtoto katika jamii ni muhimu katika kuimarisha ustawi wa kijamii na Taifa .
(iv)Ni haki ya mtoto kuonesha heshima na utii katika jamii .
(v)Ni wajibu wa mtoto kuheshimu viongozi wa serikali .
2.Eleza kwa kifupi wajibu wa mtoto katika jamii.
3.Fafanua umuhimu wa mtoto kutimiza wajibu wake katika jamii na Taifa.
4.Taja mahali pa kutoa taarifa iwapo haki zako na za watoto wengine zitavunjwa.
5.Je,jamii ina nafasi gani katika kukuza na kulinda haki za mtoto?
6.Hatua zipi mtoto anapaswa kuchukua iwapo haki zake zitakiukwa katika jamii na Taifa?
7.Eleza muhimu wa jamii na serikali katika kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kutekelezwa kwa ufanisi.
8.Andika hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia ukatili na unyanyasaji wa watoto katika jamii inayomzunguka.
9.Eleza namna mtoto anavyoweza kushiriki kupinga vitendo vya rushwa katika jamii na Taifa.