Sura ya 01 : Dhana na chimbuko la fasihi

Utangulizi

Fasihi inatuwezesha kufikiri kwa kina na kufahamu tamaduni na masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na kuwasiliana kwa ufasaha. Katika sura hii, utajifunza juu ya dhana ya fasihi, mitazamo mbalimbali ya dhana hiyo ya fasihi, na chimbuko la fasihi. Umaheri utakaojenga katika sura hii utakusaidia kukuza uelewa na kutathmini maarifa hayo.

Maisha bila Fasihi

Shughuli ya 1.1

Kwa kutumia vyanzo vya maktabani, mtandaoni, au vinginevyo, bainisha matini ambazo unadhani ni fasihi, na eleza kwa nini unadhani hivyo.

Dhana ya fasihi

Wataalamu mbalimbali wameielezea dhana ya fasihi kwa namna tofauti. Kwa ujumla wanakubaliana kuwa fasihi ni sanaa bunifu ya lugha inayosawiri hali mbalimbali za maisha. Hali hizi ni pamoja na mahusiano, hisia za watu, mazingira, migogoro na mengineyo. Sanaa ya fasihi inajidhihirisha katika tanzu kama vile tamthiliya, riwaya, ushairi, semi na nyinginezo.

Shughuli ya 1.2

Kwa kutumia mifano ya fasihi unayoifahamu, toa maoni yako kuhusu dhana ya fasihi.

Shughuli ya 1.3

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, fafanua mitazamo kuhusu dhana ya fasihi. 

Mitazamo mbalimbali kuhusu dhana ya fasihi

Kuna mitazamo mbalimbali inayojadili dhana ya fasihi. Mtazamo wa kwanza unajiegemeza kwenye kisawe cha neno fasihi kwa Kiingereza, yaani literature. Mtazamo huu unadai kuwa literature ni jumla ya maandishi yote yaani kila kitu kilichoandikwa ni fasihi. Mtazamo huu umeelezwa na Wellek na Warren (1986). Hata hivyo, dhana hii inapingwa na baadhi ya wanazuoni wa fasihi. Kwa mfano, Mulokozi (2017) anadai kuwa dhana ya literature inatofautiana na dhana ya fasihi. Katika lugha ya Kiingereza, maana moja wapo ya literature ni maandishi yoyote, ilhali katika Kiswahili, dhana ya "fasihi" inazingatia fasihi kama sanaa na aina zote za fasihi.

Mtazamo wa pili unadai kuwa fasihi ni hisi ambazo zinajifafanua kwa njia ya lugha. Wafuasi wakuu wa mtazamo huu ni Sengo na Kiango (1975). Wataalamu hawa wanasema kuwa ili mwanafasihi aweze kuandika au kueleza jambo kifasihi lazima aguswe na hisia fulani. Wataalamu hao wanasema kuwa hisi ni kama kusikia njaa, baridi, joto, uchovu au kuumwa. Mtazamo huu pia umekosolewa na baadhi ya wanazuoni. Kwa mfano, Mulokozi (2017) anaeleza kuwa mtazamo huu unachanganya mambo matatu ambayo ni fasihi yenyewe, mambo yaelezwayo na fasihi, na mtindo wa kifasihi. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fasihi inaweza kuelezea hisi lakini fasihi yenyewe si hisi. Kwa mfano, fasihi huweza kuelezea hisi za mapenzi lakini fasihi yenyewe si mapenzi.

Mtazamo wa tatu unaitazama fasihi kama sanaa ya lugha yenye ubunifu bila kujali kama imeandikwa au la. Mtazamo huu unaafikiwa na Kirumbi (1975), Mutembei (2006) na Senkoro (2011). Kwa mujibu wa mtazamo huu, hata nyimbo na masimulizi ya kisanaa ni fasihi, ijapokuwa hayakuandikwa. Kirumbi anasema kuwa fasihi ni taaluma ya sanaa inayowasilishwa kwa njia ya lugha katika muundo wa maandishi au matamshi. Senkoro (2011) ana mtazamo sawa na wa Kirumbi anapoieleza fasihi kuwa ni "sanaa itoayo maudhui yake kwa kutumia lugha ya maneno ambayo hutamkwa ama huandikwa."

Mtazamo wa nne unadai kuwa fasihi ni maandiko bora ya kisanaa yenye manufaa ya kudumu. Akizungumzia mtazamo huu, Summers (1989) anasema kuwa fasihi ni sanaa inayojumuisha zaidi maneno yaliyoandikwa. Mtazamo huu unaupa uzito ufundi wa kubuni lakini unafinya mawanda ya fasihi kwa kuhusisha mawazo yaliyo bora tu ambayo, hata hivyo, ni vigumu kuyaainisha.

Mtazamo wa tano unaeleza kuwa fasihi ni matokeo ya matumizi ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili kuleta athari maalumu. Miongoni mwa waasisi wa mtazamo huu Roman Jakobson. Mtazamo huu huona kuwa fasihi hukiuka taratibu za kawaida za matumizi ya lugha katika sarufi, maana na sauti ili kumvutia na kumuathiri msikilizaji au msomaji. Mtazamo huu humfanya msomaji aitafakari lugha yenyewe badala ya kuutafakari ujumbe unaowasilishwa na lugha hiyo. Vilevile, fasihi inaonekana kuelemea zaidi upande wa fani na kupuuza maudhui, maana na muktadha wa kazi za fasihi.

Kutokana na mjadala huu, tunaweza kusema kuwa mitazamo hii yote inahusisha fasihi, maisha na jamii. Yaani, fasihi ni sanaa inayotumia lugha kuwasilisha hali mbalimbali zinazomhusu mwanadamu na maisha yake. Tunaposema "lugha" hatuna maana ya usemaji wa kutumia sauti tu, bali hata mawasiliano ya kutumia ishara na vitendo.

Shughuli ya 1.4

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, jadili ubora na upungufu wa kila mtazamo kuhusu dhana ya fasihi.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi 

1. Ni kwa vipi si kila andiko ni fasihi?

2. Eleza ni kwa namna gani fasihi ni sanaa.

3. Jadili umuhimu wa fasihi katika maisha ya mwanadamu.

NADHARIA ZA CHIMBUKO LA FASIHI

Nadharia za chimbuko la fasihi ni mitazamo inayojaribu kueleza namna fasihi ilivyoanza katika jamii za binadamu. Hakuna nadharia moja inayokubalika kuwa ndiyo chanzo pekee, kwa sababu fasihi huenda ilitokana na shughuli mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

1. Nadharia ya kazi

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilitokana na shughuli za kazi. Watu walipokuwa wakifanya kazi kama kulima, kuvua, kuwinda au kusukuma mashua, waliimba nyimbo ili kuleta moyo wa pamoja, kupunguza uchovu na kuratibu mwendo wa kazi.

Mfano: Wakulima wanaweza kuimba kwa pamoja wanapolima ili kuhimiza bidii na kurahisisha kazi.

2. Nadharia ya matambiko na dini

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilitokana na ibada, matambiko na imani za jamii. Watu waliimba, kucheza, kughani na kusimulia hadithi wakati wa kuomba mvua, kutoa sadaka au kuwasiliana na mizimu.

Mfano: Nyimbo za kuomba mvua au maghani ya kuwasifu wahenga yanaweza kuwa chanzo cha fasihi.

3. Nadharia ya mchezo

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilianza kutokana na michezo ya binadamu. Watoto na watu wazima walicheza, kuigiza, kuimba na kushindana kwa maneno, hivyo kuibua aina mbalimbali za fasihi.

Mfano: Michezo ya watoto yenye nyimbo, majibizano na uigizaji inaweza kuzaa maigizo, mashairi na hadithi.

4. Nadharia ya uigaji

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilitokana na tabia ya binadamu kuiga mazingira, wanyama, watu na matukio. Kupitia uigaji huo, binadamu aliunda maigizo, hadithi na nyimbo.

Mfano: Wawindaji waliweza kuiga mienendo ya wanyama au matukio ya uwindaji na kuyawasilisha mbele ya wenzao.

5. Nadharia ya lugha

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilianza baada ya binadamu kupata lugha. Lugha ilimwezesha kueleza hisia, matukio, hofu, furaha na tajriba zake kwa njia ya masimulizi na nyimbo.

Mfano: Binadamu alipoweza kueleza tukio la uwindaji kwa maneno, masimulizi hayo yalikuwa msingi wa hadithi.

6. Nadharia ya hisia

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilitokana na haja ya binadamu kueleza hisia zake kama furaha, huzuni, mapenzi, hofu na hasira.

Mfano: Nyimbo za maombolezo zilitokana na huzuni, wakati nyimbo za harusi zilitokana na furaha.

7. Nadharia ya burudani

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilianza kutokana na hitaji la binadamu kujiburudisha baada ya kazi au wakati wa mapumziko. Watu walisimulia hadithi, kuimba, kucheza na kutambiana.

Mfano: Wazee walikusanya watoto jioni na kuwasimulia ngano kwa ajili ya burudani na mafunzo.

8. Nadharia ya mawasiliano

Nadharia hii inaeleza kuwa fasihi ilitokana na haja ya binadamu kuwasiliana na wengine. Masimulizi, ngomezi, nyimbo na ishara zilitumika kupeleka taarifa na ujumbe.

Mfano: Ngoma maalumu ilipigwa kuonya kuhusu hatari au kuita watu kwenye mkutano.

Hitimisho: Chimbuko la fasihi linaelezwa na nadharia mbalimbali kwa sababu fasihi imefungamana na shughuli nyingi za maisha ya mwanadamu. Kazi, dini, michezo, lugha, hisia, burudani na mawasiliano yote yanaweza kuwa vyanzo vya fasihi.

Nadharia za chimbuko la fasihi

Shughuli ya 1.5

Soma matini mbalimbali zinazopatikana mkondoni na maktabani zinazohusu nadharia za chimbuko la fasihi, kisha zielezee kwa ufupi.

Dhana ya nadharia

Wataalamu wanaeleza kuwa nadharia ni maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani. Nadharia za chimbuko la fasihi ambazo Senkoro (1987) na Mulokozi (2017) wanazitaja ni nadharia za kidhanifu na kiyakinifu.

Nadharia ya kidhanifu

Msingi wa nadharia hii ni mawazo ya kudhani, yasiyotokana na uhalisi. Waasisi wa nadharia hii ni wanafalsafa wa Kiyunani, wakiwamo Plato na Sokrate. Wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa fasihi na sanaa vimetoka kwa Mungu. Hivyo, mwanafasihi huipokea sanaa ikiwa tayari imeivishwa na Mungu.

Wachambuzi wengine wenye mtazamo wa kidhanifu ni Felician Nkwera na John Ramadhan. Katika insha yake kuhusu fasihi, Nkwera (1976) anasema "Fasihi ni sanaa ambayo huanzia kwa Muumba, humfikia mtu katika vipengele mbalimbali... (ni) hekima ambayo mtu ameshirikishwa apate kumtambua Muumba wake". Akiunga mkono mtazamo huo, Ramadhan (1975) anasema kwamba, ingawa fasihi ni hisi, kitendo cha mtu kuibuni kazi ya sanaa ni uigaji wa Mungu ambaye ndiye mfalme wa sanaa zote. Mawazo ya wafuasi wa nadharia hii hayana uthibitisho wowote zaidi ya kumtenga msanii na jamii yake kwa kumkweza na kuonekana yuko karibu na Mungu kuliko wanajamii wengine. Aidha, wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa mwanafasihi hawezi kubuni kitu chochote zaidi ya kuiga sanaa ambayo tayari Mungu ameitengeneza.

Nadharia ya kiyakinifu

Kwa mujibu wa Senkoro (1987), chimbuko la sanaa na fasihi ni mazingira halisi ya jamii, hususani sanaa ya mwanzo iliyofungamana na kazi za uzalishaji mali. Hii inamaanisha kwamba chanzo cha fasihi na sanaa ni binadamu (jamii) na mazingira yake. Katika harakati za kukabili mazingira yake, ilimlazimu binadamu kufanya kazi. Binadamu wa mwanzo aliishi katika mazingira yasiyo rafiki. Hivyo, ilimlazimu kutumia silaha ili apambane na mazingira hayo. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kutafuta njia za kurekebisha silaha zake (mawebutu) kwa kuyachonga ili yawe na ncha kali. Uchongaji huo ndio ulikuwa sanaa yenyewe. Kwa hiyo, hisia za kisanaa zimefungamana na maendeleo ya mtu katika kupambana na mazingira yake na katika kufanya kazi. Nadharia hii ina mwelekeo wa kukubalika zaidi, kwani inakubaliana na fikra kuwa wanadamu walianza mawasiliano kupitia kazi zao. Kwa mantiki hiyo, chimbuko la sanaa ni kazi.

Kadiri binadamu alivyozidi kuendelea, alikuwa na mahitaji mengine zaidi ya mahitaji ya msingi. Mahitaji hayo yaliamsha hisia za kuchora vielelezo vya shughuli zake za kujikimu. Michoro ya mapangoni iliyopo Kondoa (Tanzania) ni mifano mizuri ya vielelezo hivyo. Kuzuka kwa lugha kuliongeza aina nyingine ya sanaa ambayo ni fasihi.

Fasihi, kama zilivyo sanaa nyingine, ilitokana na kazi alizofanya binadamu katika kupambana na mazingira yake. Fasihi ilianzia katika wimbo wa kazi. Baadaye, tanzu nyingine za fasihi zilitungwa na kusimuliwa kwa madhumuni ya kufunza, kukosoa, kuadibu, kuchokoza fikra na kuliwaza jamii baada ya kazi. Kadiri maendeleo ya uzalishaji mali yalivyoongezeka, binadamu akapata muda wa kupumzika na kustarehe kwa njia ya sanaa. Fasihi ilianza kutengana na kaziza uzalishaji na kuanza kuwa shughuli maalumu ya kijamii ambapo ilitendwa katika matukio mbalimbali, kama vile sherehe na ibada.

Nadharia nyingine inayoelezwa na Mulokozi (2017) ni ya mwigo au uigaji. Nadharia hii inazingatia ubunifu wa mwanadamu katika kuiga maumbile na mazingira yaliyomzunguka kwa kusawiri vitu vilivyomo katika hali mbalimbali. Akigusia dosari kuu ya nadharia hii, Mulokozi anasema kuwa katika kusisitiza mno uigaji, suala la ubunifu wa kisanaa na kifasihi linasahauliwa.

Shughuli ya 1.6

Jadili ubora na upungufu unaojitokeza katika nadharia za chimbuko la fasihi.

www.learninghubtz.co.tz

Tamrini

1. Kwa kutumia mifano, fafanua maana ya dhana zifuatazo:

  1. Fasihi
  2. Mtazamo
  3. Nadharia
  4. Chimbuko

2. Dhana ya fasihi inaelezwa kwa mitazamo mbalimbali. Jadili mitazamo hiyo.

3. "Ujifunzaji wa fasihi hauna umuhimu wowote." Jadili hoja hii.

4. Chunguza fasili za dhana ya fasihi zifuatazo kisha, eleza zinafanana na kutofautiana katika vipengele vipi?

  1. Fasihi inahusisha ufundi wa matumizi ya lugha katika kuwasilisha dhana na matukio mbalimbali yanayomhusu binadamu na mazingira yake (Ponera, 2014).
  2. Fasihi ni sanaa ya lugha yenye ubunifu inayosawiri vipengele vya maisha, mahusiano, mazingira na hisia za watu katika muktadha fulani (Mulokozi, 2017).
  3. Fasihi ni sanaa itumiayo lugha ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa na unaoendana na jamii husika (Mlaga, 2017).

5. “Mitazamo mbalimbali kuhusu dhana ya fasihi imechangia kupanua uelewa wa fasihi, lakini kila mtazamo una ubora na upungufu wake.” Jadili kauli hii kwa kutumia mifano mwafaka.

6. Kwa kurejelea nadharia za kidhanifu, kiyakinifu na mwigo (uigaji), chambua namna kila nadharia inavyoeleza chimbuko la fasihi, kisha eleza ni nadharia ipi ina mashiko zaidi katika kueleza chimbuko la fasihi. Toa sababu za msimamo wako.

7. “Fasihi ni sanaa bunifu ya lugha inayosawiri maisha ya jamii.” Thibitisha kauli hii kwa kujadili sifa za fasihi zinazoitofautisha na maandiko mengine yasiyo ya kifasihi. (Alama 15)

8. Kwa kutumia mifano, linganisha na kulinganisha mitazamo ya Wellek na Warren (1986), Sengo na Kiango (1975), Kirumbi (1975), Senkoro (2011), Summers (1989) na Roman Jakobson kuhusu dhana ya fasihi, kisha eleza mapungufu ya kila mtazamo.

9. “Kazi za uzalishaji mali ndizo zilikuwa msingi wa kuzuka kwa fasihi.” Jadili hoja hii kwa kurejelea Nadharia ya Kiyakinifu, ukionesha jinsi maendeleo ya binadamu yalivyochangia kukua kwa sanaa na fasihi.

10. Kwa kutumia hoja zenye mashiko, tathmini umuhimu wa kujifunza dhana ya fasihi na nadharia za chimbuko la fasihi katika kuelewa maendeleo ya fasihi na nafasi yake katika jamii ya sasa.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256