Sura Ya 02: Mchango wa historia na urithi katika maendeleo

Utangulizi

Historia na urithi ni hazina muhimu katika maendeleo ya taifa. Katika sura hii, utajifunza dhana ya historia na urithi wa taifa, maeneo mbalimbali nchini yenye historia na urithi wa taifa, na mchango wa historia na urithi katika maendeleo ya taifa. Vilevile, utajifunza uhusiano uliopo kati ya maadili na urithi katika kuchochea na kuleta maendeleo ya taifa na njia bora na endelevu za uhifadhi wa historia na urithi ili kuleta maendeleo endelevu ya taifa. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuenzi historia na urithi wa taifa, kutumia urithi uliopo kuleta maendeleo yako binafsi na jamii pamoja na kutumia njia bora kuihifadhi historia na urithi wa taifa.

Fikiri

Nafasi ya historia na urithi katika kuleta maendeleo ya taifa.

Dhana ya historia na urithi wa taifa

Kila taifa duniani lina historia na urithi wake. Kuna uhusiano kati ya historia na urithi wa taifa. Urithi ni vitu vyenye thamani vinavyotunzwa na kuthaminiwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vya baadaye. Vitu vinavyohusika katika urithi ni kama vile majengo ya kihistoria ambayo yalitumiwa na vizazi vilivyotangulia, vitu na vifaa vya kiutamaduni vilivyofaa kuhifadhiwa pamoja na vitu visivyoonekana kama vile mila na desturi. Kwa maana nyingine, kuna urithi wa aina mbili: urithi unaoshikika na urithi usioshikika. Aina zote hizo mbili huhusu vitu vinavyorithiwa na taifa ambavyo vina thamani ya kihistoria au utamaduni.

Historia ya taifa

Historia ya taifa ni kumbukumbu za matukio na mabadiliko muhimu katika maendeleo ya taifa linalohusika. Historia ya taifa hutuwezesha kuifahamu misingi na hatua za uanzishwaji wake. Pia, hutuwezesha kuelewa matukio mbalimbali katika taifa na jinsi matukio hayo yalivyochangia kupata maendeleo au kukwamisha maendeleo. Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zenye historia ndefu iliyosheheni utajiri wa urithi. Historia ya taifa hili inajumuisha mfumo wa maisha kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni wa Wajerumani na baadaye Waingereza na kipindi cha harakati za kupigania uhuru. Pia, historia ya taifa hili inajumuisha mageuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yaliyofanyika baada ya uhuru mwaka 1961, chini ya waasisi wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Sheikh Abeid Amani Karume na wengineo. Historia hiyo inaendelea katika vipindi tofauti baada ya uhuru kama vile kipindi cha siasa ya ujamaa na utekelezi wake na baadaye kipindi cha uliberali mpya mpaka wakati wa utandawazi. Kupitia kumbukumbu za matukio haya, tunajifunza taifa la Tanzania lilikotoka, lilipo sasa, na linakoelekea.

Urithi wa taifa

Urithi wa taifa ni mkusanyiko wa mali, kumbukumbu za kihistoria, utamaduni, na maadili ambayo ni muhimu kwa utambulisho na maendeleo ya taifa. Urithi wa taifa hujumuisha maeneo ya asili kama vile mbuga za wanyama, milima, mito, maziwa na bahari. Pia, unajumuisha urithi wa utamaduni kama vile majengo ya kihistoria, lugha, ngoma za asili, mavazi ya asili na vyakula. Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye utajiri mkubwa wa urithi ambao ni utambulisho muhimu wa taifa hili. Baadhi ya mifano ya urithi wa kihistoria wa taifa la Tanzania ni pamoja na majengo ya kale yaliyopo Zanzibar, Bagamoyo, na Kilwa Kisiwani na michoro ya mapangoni iliyopo Kondoa-Irangi, na Isimila, pamoja na ufundi chuma na kilimo huko Engaruka.

Historia na urithi wa taifa katika maeneo mbalimbali nchini

Kazi ya kufanya 2.1

Tafuta taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwemo mitandao, kisha fafanua historia na urithi wa taifa unaopatikana katika maeneo mengine nchini Tanzania.

Tanzania ni nchi yenye utajiri wa historia na urithi uliotawanyika katika maeneo mbalimbali. Historia na urithi huo vimekuwa vikitambuliwa na kutunzwa kwa miaka mingi iliyopita. Historia yenyewe ni urithi wa kipekee unaopatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi na umekuwa chanzo muhimu cha maarifa na ufahamu kuhusu utamaduni na harakati za maisha za jamii za Kitanzania katika nyakati na maeneo tofauti. Maeneo maarufu ya kihistoria na yenye urithi wa taifa ni pamoja na Oldupai Gorge, Bagamoyo na Kilwa Kisiwani pamoja na Nyumba ya Maajabu huko Zanzibar.

Oldupai Gorge

Oldupai Gorge iko katika bonde la Ngorongoro mkoani Arusha. Sehemu hii ni miongoni mwa maeneo yenye kuibeba historia kubwa ya nchi na ni miongoni mwa urithi muhimu wa taifa la Tanzania. Pia, eneo hili ni miongoni mwa maeneo muhimu zaidi duniani kutokana na historia yake ya kugundulika kwa mabaki ya mtu wa kale zaidi duniani. Oldupai Gorge imekuwa ikifanyiwa tafiti tangu miaka ya 1930 ambako yamegundulika mabaki ya binadamu wa kale yaliyobadilisha uelewa wetu juu ya asili ya binadamu.

Bagamoyo

Bagamoyo ni mji mkongwe uliopo katika mkoa wa Pwani. Ni mahali ambapo alama za historia ya biashara ya utumwa zinaonekana wazi. Bagamoyo ilikuwa kituo muhimu cha biashara ya utumwa katika Afrika Mashariki kati ya karne ya 18 na 19. Pia, eneo hili lilikuwa njia kuu ya kusafirishia watumwa kwenda Zanzibar na sehemu nyingine duniani kama vile Amerika, Uarabuni na Madagaska. Katika mji huu, kuna mabaki mbalimbali ya kale ikiwa ni pamoja na majengo ya zamani, makaburi ya watumwa na watawala wa Kiarabu pamoja na maeneo mengine ya kihistoria. Vilevile, mji huu umesheheni historia ya ukoloni wa Wajerumani ambao katika majengo mengi walirithi usanifu wa Kiarabu na kuongeza aina yao ya usanifu. Aidha, katika mji wa Bagamoyo kuna mabaki ya misikiti miwili, kanisa na makaburi ya Washirazi kutoka karne ya 13 ya zama za sasa katika eneo la Kaole.

Kilwa Kisiwani

Kilwa Kisiwani ni kisiwa katika wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi. Ni moja ya maeneo ya urithi wa Tanzania unaotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni. Kilwa Kisiwani ulikuwa moja ya miji muhimu zaidi ya pwani ya Afrika Mashariki katika karne za 13 hadi 16. Mji huu ulikuwa kituo kikubwa cha biashara na utamaduni wa Kiswahili. Pia, mji wa Kilwa ulitengeneza fedha yake iliyokuwa inatumika katika biashara kati yake na fedha zingine. Aidha, Kilwa Kisiwani ilikuwa na makao makuu ya Sultani. Leo hii, mabaki ya kale ya mji wa Kilwa Kisiwani yanaweza kutembelewa ili kujua historia ya eneo hilo na namna lilivyoathiri Tanzania kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Kielelezo 2.1 kinaonesha sarafu zilizokuwa zinatumika katika mji wa Kilwa.

Kielelezo 2.1: Sarafu za dhahabu zilizotumika katika mji wa Kilwa

Ngorongoro na Serengeti

Haya ni maeneo ya hifadhi za mbuga za wanyama. Ngorongoro iko mkoani Arusha na Serengeti iko mkoani Mara. Hifadhi ya Ngorongoro inajulikana kwa kuwa na kreta kubwa zaidi duniani ambayo ni makazi ya wanyama mbalimbali kama vile simba, tembo, na twiga. Hifadhi hii imekuwa maarufu duniani tangu kuanzishwa kwake katika kipindi cha utawala wa Wajerumani kisha utawala wa Waingereza hadi sasa. Hali kadhalika, hifadhi ya Serengeti inajulikana kwa kuwa na uhamaji mkubwa wa wanyama pori duniani, ikiwa ni pamoja na nyumbu na pundamilia. Pia, hifadhi hii imekuwa kivutio kwa watalii kote duniani na chanzo kikubwa cha mapato kwa taifa la Tanzania.

Nyumba ya Maajabu

Visiwa vya Zanzibar vina historia na urithi ambao unaotambulika kitaifa na kimataifa. Kwa mfano, Jengo la Beit El Ajaib (Nyumba ya Maajabu) linapatikana katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Jengo hili lilijengwa mwaka 1883 na Sultani Said Barghash. Pia, katika eneo hili kuna Ngome Kongwe ambayo ilijengwa na Wareno katika karne ya 16 kwa ajili ya kujilinda dhidi ya maadui. Aidha, katika kisiwa cha Pemba kuna Ngome Kongwe nyingine ambayo nayo ilijengwa na Wareno kwa ajili ya kujilinda. Maeneo haya na majengo mengine ni mojawapo ya historia na urithi wa taifa letu. Historia na urithi huu vimekuwa kivutio kwa watalii na wageni mbalimbali na kutoa ufahamu wa utamaduni na maisha ya zamani ya maeneo hayo.

Maeneo ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika

Kwa kuwa nchi mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, Tanzania ilipewa hadhi ya kuanzisha Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika. Pamoja na kuwa na kituo hiki, nchini Tanzania kuna maeneo mbalimbali yaliyobeba historia ya harakati za urithi wa ukombozi wa Afrika. Maeneo hayo yako zaidi ya 200 ambayo ni pamoja na Kongwa mkoani Dodoma, Mazimbu mkoani Morogoro, Nachingwea mkoani Lindi na Kaole mkoani Pwani. Katika maeneo haya kulikuwa na kambi ambazo wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika walizitumia ili kupata mafunzo ya kupambana na wakoloni katika nchi zao. Kielelezo 2.2 kinaonesha watu wakitembelea handaki lililotumika kuhifadhia silaha na kujificha katika kambi ya FRELIMO iliyokuwa Kongwa, Dodoma.

Kielelezo 2.2: Watalii wakitembelea handaki katika kambi ya FRELIMO, Kongwa Dodoma

Kazi ya kufanya 2.2 

Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu maeneo yenye urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika nchini Tanzania na kisha chambua vitu vinavyopatikana katika maeneo yanayohusika.

1. Chambua maeneo yenye historia na urithi nchini Tanzania.

2. Andaa mpangokazi wa kuelimisha jamii kuhusu maeneo yenye historia na urithi nchini Tanzania. Kwa ufupi, Tanzania ina historia na urithi mwingi ambao umekuwa kivutio kwa watalii na wageni kutoka ndani na nje ya nchi, ambao kwa njia ya utalii na utafiti wameweza kufahamu utamaduni na maisha ya zamani ya Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.

Mchango wa historia na urithi katika maendeleo ya taifa

Historia na urithi wa taifa umekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa, hususani katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, na kijamii.

Kiuchumi

Historia na urithi wa taifa vina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi ya taifa letu. Historia imetuwezesha kuelewa fursa, mafanikio na changamoto za kiuchumi ambazo taifa letu limepitia katika nyakati mbalimbali. Hii ni muhimu kwani imesaidia kuelewa upungufu na kutafuta njia sahihi za utumiaji fursa na utatuzi wa changamoto zilizojitokeza katika nyakati mbalimbali. Historia na urithi wa taifa letu vimekuwa muhimu katika maendeleo ya kiuchumi kwani vimeendelea kuvutia uwekezaji wa ndani na wa kimataifa. Uwekezaji huo umechangia kuendeleza miundombinu na ukuaji wa teknolojia, ujuzi, na mitaji. Ukuaji wa nyanja hizo umesaidia maendeleo ya kiuchumi ya taifa letu kwa kutoa fursa za ajira, kuboresha maisha ya raia na ukuaji wa pato la taifa. Aidha, historia na urithi vimeimarisha sekta ya utalii ambao huvutia watalii na wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja Tanzania na kununua bidhaa na huduma mbalimbali; hivyo, vimesaidia kuingiza fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kisiasa

Kisiasa, historia na urithi wa taifa vimejenga msingi imara wa demokrasia na utawala bora kwa taifa la Tanzania. Kwa mfano, kihistoria Tanzania imekuwa ikifanya uchaguzi huru na za kidemokrasia tangu uhuru. Historia hii imeweza mifumo ya kisiasa kuboreshwa kwa uhuru na uwazi ili kuhakikisha kuna usawa, haki, na uwajibikaji katika jamii na serikalini. Historia ya Tanzania, kupitia harakati za ukombozi na mapambano ya kisiasa, imesaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa kujitolea, kushirikiana na kuvumiliana ambao umekuwa nyenzo muhimu katika maendeleo ya taifa. Vilevile, historia inasaidia katika kuelewa na kujua jinsi matukio kama vile vita au jinsi mabadiliko ya utawala yalivyotokea na madhara yake. Hapa historia inatoa somo si tu kueleza jinsi hali ilivyokuwa bali inatujengea uwezo wa kutoweza kufanya makosa na kutafuta njia nzuri zaidi kwa maendeleo ya jamii zetu na taifa letu kwa ujumla. Mathalani, tunaona kuwa vita haikuwa njia yetu ya kupigania ukombozi wa taifa letu au kutatua migogoro mingine. Hiyo haikuwa njia yetu ya kutatua matatizo. Jambo hili ni somo tulilojifunza kutoka katika matukio ya vita kama ile ya Maji Maji ya mwaka 1905-1907. Kutumia diplomasia kumekuwa njia bora sana katika nchi yetu na kuleta faida nyingi zaidi za kimaendeleo.

Kijamii

Kijamii, historia na urithi wa Tanzania vimesaidia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi. Kwa mfano, utamaduni kama vile mila na desturi, lugha na imani za kidini vimekuwa msingi madhubuti wa kuhamasisha upendo na umoja wa kitaifa. Aidha, historia ya mapambano ya ukombozi dhidi ya ukoloni, changamoto na harakati za pamoja za kijamii baada ya uhuru zimejenga msingi imara wa mshikamano, amani na utulivu imara miongoni mwa wananchi na kusaidia kukua kwa maendeleo na ustawi wa jamii imara. Aidha, historia na urithi vimesaidia kukuza ufahamu wa jamii juu ya utamaduni wetu na kusaidia kuenzi na kudumisha mila na desturi zetu za jadi. Hali hii imejenga na kudumisha utambulisho na heshima ya jamii zetu kama taifa. Pia, historia na urithi wa taifa letu vimekuwa na athari chanya katika ukuaji wa sekta ya elimu. Kupitia kujifunza historia na kufanya tafiti kuhusu urithi wa taifa, jamii imeweza kuvumbua maarifa mapya, kukuza ufahamu na kuzalisha wasomi wabobezi katika nyanja mbalimbali za kijamii. Kwa ujumla, historia na urithi vimesaidia kuleta maendeleo ya taifa letu kwa kuwatambulisha Watanzania kama wamoja katika taifa moja na kufanya washirikiane katika kuleta maendeleo ya taifa kama wamoja.

Kazi ya kufanya 2.3

Fanya utafiti mdogo katika jamii inayokuzunguka, kisha bainisha aina mbalimbali za urithi wa asili na mchango wake katika maendeleo ya jamii hiyo.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

1. Linganisha urithi unaotokana na majengo ya kihistoria na ule unaotokana na maliasili nchini Tanzania.

2. Eleza urithi uliotokana na biashara ya utumwa.

3. Ni kwa jinsi gani historia na urithi wa taifa vinaweza kuathiri maendeleo?

4. Jadili namna urithi wa kitamaduni unavyoweza kusaidia kuondoa umasikini katika jamii inayokuzunguka.

5. Fafanua jinsi historia ya taifa imekuwa nguzo ya umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania.

6. Eleza ni kwa namna gani unaweza kutumia historia na urithi wa taifa lako kama chanzo cha kujifunza na kuboresha maendeleo ya jamii yako.

7. Ni kwa njia gani kijana wa Kitanzania anawezaA kuhakikisha kwamba historia na urithi wa taifa vinatunzwa na kuheshimiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo?

Uhusiano kati ya maadili na urithi katika kuleta maendeleo ya taifa

Maadili na urithi ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa taifa imara na lenye mafanikio. Maadili ni kanuni, miiko na miongozo inayosimamia tabia na mwenendo inayokubalika katika jamii. Urithi wa taifa nao ni jumla ya vitu au mambo ya kiutamaduni, kihistoria, sanaa, lugha, na maadili yanayojenga utambulisho wa taifa fulani. Uhusiano kati ya maadili na urithi huchangia katika kuleta maendeleo ya taifa kwa namna mbalimbali kama inavyoelezwa hapa chini:

(a) Maadili ni sehemu ya utamaduni ambao pia ni urithi wa taifa. Hivyo, maadili huchangia maendeleo ya taifa kwa kusaidia kuudumisha na kuuendeleza urithi huo. Kwa mfano, uwajibikaji, heshima, utu, uadilifu, kuzuia na kupambana na rushwa na ushirikiano kama sehemu ya maadili ya Kitanzania ni urithi unaosaidia kuudumisha utambulisho wa taifa la Tanzania na kuchangia maendeleo ya taifa katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

(b) Maadili ni sehemu ya urithi wa taifa ambayo husaidia kutoa mwongozo katika kufanya uamuzi sahihi na kujenga heshima, uaminifu, na uadilifu katika masuala mbalimbali ya kifamilia, kijamii na kitaifa. Hali hii hujenga msingi imara wa haki, usawa, amani na utulivu katika jamii na hatimaye kuchangia maendeleo endelevu ya mtu binafsi na ya taifa kwa ujumla. Hivyo basi, Watanzania tunapaswa kuyaheshimu na kuyadumisha maadili katika jamii pamoja na kushiriki kuzuia na kupambana na rushwa ili kuudumisha urithi huo unaochochea maendeleo ya taifa letu. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kusaidia kuijenga na kuilinda nchi yetu kwa masilahi mapana ya vizazi vya sasa na vijavyo.

(c) Kuishi kwa kufuata maadili ni moja ya hatua muhimu katika kuujenga urithi imara wa taifa lenye heshima, ukarimu, utu na uvumilivu. Watu wanaoishi kwa kufuata maadili na kuviepuka vitendo vya rushwa wana uhusiano mzuri na wenzao na husaidia kujenga taifa lenye kuheshimu maadili na haki za raia wake. Taifa lenye kuyaheshimu maadili hujenga uhusiano mzuri miongoni mwa raia wake na kuidumisha amani na utulivu. Uhusiano mzuri, amani na utulivu ni vichocheo vikubwa vya maendeleo ya taifa.

(d) Maadili ni urithi wa kiutamaduni ambao umejengwa kihistoria katika taifa letu. Hii ina maana kuwa maadili yamejengwa kutokana na historia ambayo imerithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Urithi huu hutusaidia kuielewa, kuithamini na kuidumisha asili yetu kama taifa. Pia, husaidia kuujenga utu na utambulisho wetu kiutamaduni. Hivyo, ni jukumu la kila mwananchi kuyadumisha na kuyalinda maadili yetu kwani ni urithi ambao unachochea maendeleo katika taifa letu.

(e) Maadili yetu huchangia sana katika kuuendeleza na kuuimarisha urithi wa taifa letu. Maadili hutujengea uadilifu katika matumizi ya urithi wa rasilimali zetu. Jamii yenye maadili hufuata taratibu za kuyahifadhi na kuyalinda mazingira na rasilimali zake. Pia, huepuka ufisadi na kuulinda utamaduni wa taifa kwa gharama yoyote. Kupitia maadili haya tunajenga urithi endelevu wenye manufaa kwa maendeleo ya taifa letu. Kwa upande mwingine, utunzaji wa urithi wetu huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuyaimarisha na kuyaendeleza maadili yetu ya kiutamaduni kama taifa.

(f) Maadili na urithi vinachangia ujenzi wa jamii imara na iliyo tayari kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujiletea maendeleo. Maadili yanapokuwa msingi wa maisha yetu ya kila siku husaidia jamii kuona fahari na kulinda na kuutumia urithi kwa uadilifu mkubwa. Kwa kufanya hivyo, tunathibitisha thamani yetu ya kuhifadhi utajiri huu wa kiutamaduni na kihistoria kwa manufaa ya vizazi na vizazi, jambo ambalo linaleta maendeleo endelevu kwa taifa.

(g) Utamaduni na historia kama sehemu ya urithi wetu vina jukumu muhimu katika kuyaimarisha maadili yetu. Kupitia maarifa tunayoyapata kutokana na urithi huu, tunaweza kuihamasisha na kuielimisha jamii yetu kuhusu maadili. Kwa mfano, kupitia makosa kutoka katika utamaduni na historia yetu, taifa limeweza kuunda miongozo sahihi ya maadili inayotumika kama hazina ya zana za maendeleo ya taifa letu.

(h) Maadili ni urithi unaojenga misingi ya utawala bora na umoja katika taifa. Taifa lenye viongozi na wananchi wenye maadili hupata maendeleo kwa kusimamia haki na uwajibikaji katika kuihifadhi historia na urithi kwa maendeleo ya taifa. Urithi wa utamaduni na historia kama rasilimali zilizosimamiwa kwa kuzingatia maadili huchochea maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwani huondoa chuki na migogoro katika taifa.

Kazi ya kufanya 2.4

Uliza watu mbalimbali katika jamii unamoishi jinsi urithi wa kiutamaduni unavyoweza kuchangia maendeleo ya jamii.

Uhifadhi wa urithi kwa maendeleo endelevu ya taifa

Urithi wa taifa ni rasilimali muhimu katika kuyaleta maendeleo endelevu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa taifa lolote lile duniani. Tanzania ni miongoni mwa mataifa yenye utajiri mkubwa wa urithi wa kihistoria. Hivyo, uhifadhi wa urithi huo ni hatua muhimu ya kuudumisha ili kuchangia katika mchakato wa kuleta maendeleo. Uhifadhi wa urithi wa taifa ni shughuli za kuyalinda na kuyatunza maeneo muhimu ya kihistoria, utamaduni, nyaraka za kihistoria, lugha na maliasili za taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo. Hivyo, kila raia au Mtanzania anapaswa kushirikiana na serikali katika kuuhifadhi urithi wa taifa kama wajibu wake.

Wajibu wa raia mmoja mmoja katika uhifadhi wa urithi wa taifa

Kila raia wa Tanzania ana jukumu na wajibu wa kushirikiana katika kuuhifadhi urithi wa taifa kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo:

(a) Kuuhifadhi urithi wa taifa kwa kuheshimu na kuuenzi utamaduni, mila na desturi za taifa. Pia, kushirikiki katika matamasha na mashindano ya kiutamaduni, kudumisha lugha za asili, na kuhifadhi maeneo ya kihistoria.

(b) Kuihamasisha jamii na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa urithi, madhara ya uharibifu wa urithi wetu na njia sahihi za kuuhifadhi urithi wa taifa letu. Raia anaweza kutumia njia mbalimbali kama sanaa, kampeni na vyombo vya mawasiliano katika kuwaelimisha na kuwahamasisha watu kuhusu umuhimu na njia za kuhifadhi historia na urithi wa taifa.

(c) Kuzuia na kupambana na rushwa, dawa za kulevya na kulipa kodi kwa wakati ili kuwezesha ulinzi na uendelezaji wa uhifadhi wa urithi au kuzuia vitendo vinavyoweza kusababisha uharibifu wa urithi wa taifa.

(d) Kuzuia na kupambana na rushwa katika shughuli mbalimbali za uhifadhi wa urithi au vitendo vinavyoweza kusababisha uharibifu wa urithi wa taifa. Raia anatakiwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwenye ofisi za serikali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupitia njia zifuatazo: (i) Kufika ofisi za TAKUKURU zilizopo kila wilaya nchini; (ii) Kupiga simu ya bure au kuandika ujumbe (sms) kwenda namba 113 au kupiga *113# kisha kufuata maelekezo; na (iii) Kutumia simu ya kiganjani kupakua programu tumizi ya TAKUKURU (TAKUKURU APP) kwenye Playstore kisha kuitumia kupiga picha, kuzirekodi sauti au nyaraka na kuzituma kupitia programu tumizi hiyo au kujaza na kuituma fomu iliyopo kwenye tovuti ya TAKUKURU (www.pccb.go.tz). Aidha, kila raia awe na ujasiri wa kukubali kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya watuhumiwa watakaofikishwa mahakamani kutokana na vitendo vya rushwa na kuhusu uharibifu wa historia au urithi wa taifa.

Wajibu wa jamii katika uhifadhi wa urithi wa taifa

Jamii ina jukumu kubwa la kuuhifadhi urithi wa taifa kwa sababu urithi huo ni sehemu muhimu ya historia na utambulisho wa taifa. Katika kutekeleza jukumu hili, jamii ina wajibu ufuatao:

(a) Kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa urithi kwa kuchangia nguvukazi katika shughuli za upandaji miti pamoja na ujenzi na ukarabati wa maeneo ya urithi. Ushiriki katika shughuli hizi utasaidia kuyafanya maeneo ya urithi yaendelee kuwa katika hali ya ubora na kuvutia utalii wa ndani na nje. Pia, ni wajibu wa jamii kujitolea kuchangia rasilimali zao kwa ajili ya kuendeleza miradi ya uhifadhi katika maeneo yao. Aidha, ni wajibu wa viongozi wa kijamii kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutoa elimu kwa wanajamii kuhusu njia na umuhimu wa uhifadhi wa maeneo ya kihistoria na urithi. Hii itawasaidia wanajamii kutambua na kuongeza uelewa juu ya urithi na umuhimu wake katika kuleta maendeleo endelevu. Elimu ya uhifadhi wa urithi wa taifa itamwezesha kila mwanajamii kuutamini na kuuenzi urithi huo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

(b) Kuyalinda na kuyahifadhi maeneo ya urithi kwa kuchukua hatua mbalimbali. Miongoni mwa hatua hizo ni kushiriki katika shughuli za usafi na ulinzi wa maeneo ya urithi. Vilevile, jamii inapaswa

Kushiriki katika kuzuia vitendo vya uhalifu au uharibifu wa maeneo ya urithi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwenye mamlaka za ulinzi na usalama. Kwa kufanya hivyo jamii itakuwa imetimiza wajibu wake katika kulinda, kuendeleza na kuudumisha urithi wa taifa.

Ili kulifanikisha jukumu hili, ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya jamii, asasi au taasisi zinazohusika na uhifadhi wa maeneo ya urithi pamoja na serikali. Ushirikiano kati ya jamii, taasisi na serikali utasaidia kubadilishana ujuzi na uzoefu juu ya namna bora ya kulinda urithi wetu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

(c) Kuuhifadhi urithi wa taifa kwa kuhakikisha unasambaza maarifa ya urithi kwa vizazi vijavyo. Katika kufanikisha hili jamii inapaswa kuzikusanya, kuzihifadhi na kuzisambaza taarifa na maarifa juu ya urithi wa taifa toka kizazi kimoja na kingine. Upatikanaji wa taarifa na maarifa hayo kwa watu wote kutatoa fursa kwa kila mwanajamii kujifunza na kufahamu kwa kina juu ya urithi wa taifa kupitia vyanzo kama vile vitabu, mitandao ya kidijiti, na njia nyingine za kiteknolojia. Kwa kufanya hivyo, jamii itakuwa nguzo muhimu katika kuuhifadhi urithi wa taifa kwa vizazi vijavyo.

(d) Kuwaclimisha vijana kuanzia ngazi ya familia ili wafuate maadili ya kujali na kutunza urithi wa taifa na kutojihusisha na vitendo vya kiharifu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na ukwepaji kodi. Pia, wawe tayari kuzuia na kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotishia uharibifu wa urithi wa taifa kwenye ofisi za serikali ngazi ya kijiji au mtaa, wilaya au ofisi za TAKUKURU zilizopo katika kila wilaya hapa nchini. Pia, wanaweza kuripoti kwa kupiga simu ya bure au kuandika ujumbe mfupi (sms) kwenda namba 113 au kupiga *113# kisha kufuata maelekezo.

Wajibu wa serikali katika uhifadhi wa urithi wa taifa

Kama wadau wengine, serikali ina wajibu mkubwa sana katika uhifadhi wa urithi wa taifa. Miongoni mwa wajibu wa serikali katika uhifadhi wa urithi wa taifa ni pamoja na:

(a) Kutunga sera na sheria za kuulinda na kuutunza urithi wa taifa. Serikali ina wajibu wa kuzitunga sera kuhusu namna ya kuyahifadhi maeneo ya urithi wa taifa. Kupitia sera hizo jamii na wadau wanapata miongozo inayowawezesha kuweka mikakati madhubuti ya kusimamia uhifadhi wa urithi wa taifa. Aidha, kuwepo kwa usimamizi wa utekelezaji wa sheria za uhifadhi ni hatua muhimu sana katika kuyalinda maeneo ya urithi. Sheria hizi zitatoa kanuni na taratibu za kuzingatia katika matumizi ya rasilimali na zinaainisha adhabu mbalimbali kwa mtu au watu wataokiuka au kuvunja taratibu za kisheria zinazohusiana na uhifadhi wa urithi wa taifa.

Mfano wa sheria na sera za uhifadhi wa urithi zilizotungwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na Sheria ya Malikale na Sera ya Malikale ya mwaka 2008. Kwa minajili hii, wizara, kupitia Idara ya Mambo ya Kale, ina wajibu wa kutambua, kulinda, kutunza na kuhifadhi Kumbukumbu na Urithi wa Taifa na Urithi wa Dunia kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya 2008, Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333 (R.E 2002) na Mkataba wa Kimataifa ya 1972 wa UNESCO. Kumbukumbu na Urithi huu unatokana na rasilimali za utamaduni zinazoshikika na zisizoshikika; zinazohamishika na zisizohamishika kama zinavyoainishwa katika Sera ya Malikale (2008) na Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333. Malengo mahususi ya Sera ya Malikale 2008 ni pamoja na kufafanua dhima na majukumu ya serikali za mitaa, jamii, watu binafsi, mashirika na asasi mbalimbali katika kuhifadhi na kusimamia malikale; kuweka ufafanuzi sahihi wa kulinda, kusimamia, kutunza, kuhifadhi, kuendesha na kuendeleza malikale; kuweka Kumbukumbu za Urithi wa Taifa kwa ujumla, na kuainisha namna bora ya kusimamia utafiti na uhifadhi wa malikale.

(b) Kupanga mikakati ya uhifadhi na kusimamia utekelezaji wake. Serikali ina wajibu wa kupanga na kusimamia utekelezaji wa mikakati madhubuti ya kuulinda na kuutunza urithi wa taifa. Mikakati hiyo ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhifadhi wa urithi kwa ufanisi. Kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikakati iliyowekwa kwa kiwango kinachohitajika ni hatua muhimu katika uhifadhi wa urithi kwa manufaa ya vizazi vijavyo na ustawi wa taifa kwa ujumla.

(c) Kuunda taasisi na vyombo maalum vya kusimamia uhifadhi wa urithi wa taifa. Serikali inapaswa kuunda taasisi na vyombo maalum vya kusimamia uhifadhi wa urithi wa taifa letu. Katika kutekeleza jukumu hili muhimu, serikali imefanikiwa kuunda taasisi mbalimbali ikiwemo Makumbusho ya Taifa ambayo ni taasisi ya kielimu na kiutamaduni yenye wajibu wa kukusanya, kutunza na kufanya utafiti wa vifaa vya kiutamaduni na kisayansi vinavyohusu urithi wa kiutamaduni na asili wa Tanzania. Pia, kuna Idara ya Malikale yenye jukumu la kuzisimamia na kuzihifadhi rasilimali za utamaduni, zinazoshikika na zisizoshikika pamoja na zile zinazohamishika na zisizohamishika zilizo nchi kavu na majini zenye umri wa miaka mia moja (100) na kuendelea. Taasisi nyingine ni pamoja na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lenye wajibu wa kuikuza lugha ya Kiswahili na Baraza la Sanaa la Tanzania (BASATA) lenye wajibu wa kuongeza uhifadhi na maendeleo ya uzalishaji wa kazi tofauti za sanaa.

(d) Kutenga bajeti ya kufanikisha utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa urithi wa taifa. Serikali ina wajibu mkubwa wa kutenga fedha ili kuhakikisha kuwa shughuli za uhifadhi zinafanyika kwa ufanisi. Fedha hizo zitatumika katika shughuli za uhifadhi kama vile ukarabati wa miundombinu iliyoweza kwenye maeneo ya urithi, kuhakikisha utunzaji wa rasilimali na kumbukumbu za kihistoria, na kuwezesha shughuli za utafiti kuhusiana na urithi wa taifa. Aidha, fedha zinatumika katika utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu faida za kuuhifadhi urithi wa taifa letu.

(e) Kuielimisha jamii kuhusu uhifadhi wa urithi wa taifa. Serikali ina jukumu muhimu la kuhakikisha kuwa jamii inapata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu na njia mbalimbali za uhifadhi wa urithi wa taifa. Serikali inatakiwa kutekeleza jukumu hili kupitia mikutano ya hadhara, semina, taasisi za elimu na vyombo vya habari. Elimu na mafunzo ni nyenzo muhimu katika uhifadhi kwani husaidia kujenga jamii yenye kuutamini na kuuenzi urithi kwa manufaa ya taifa.

(f) Kufanya na kusaidia kufanyika kwa tafiti mbalimbali zinazohusu urithi wa taifa. Kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali, serikali inatakiwa kufanya tafiti au kuziwezesha taasisi na wadau mbalimbali wa uhifadhi kufanya tafiti kuhusu urithi wa taifa. Hii itasaidia kubaini maeneo mapya ya urithi, changamoto za uhifadhi na njia sahihi za kuuhifadhi urithi wa taifa. Serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba tafiti zinakamilika na matokeo ya tafiti hizo yanatolewa, yanatunzwa na kutumika ipasavyo kwa maendeleo endelevu ya urithi wa taifa letu. Tafiti hizi ni pamoja na zile za kihistoria, kiakiolojia na kitamaduni ambazo zitatoa mwelekeo bora wa kuuhifadhi na kuutunza urithi wa taifa.

(g) Kuutekeleza kikamilifu Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji (National Anti-Corruption Strategy and Action Plan) ili kuweka mifumo imara ya ndani inayoimarisha uadilifu na kuzuia rushwa katika taasisi zinazohusika ikiwemo kuunda Kamati za Kusimamia Maadili (Integrity Committees), kutengeneza miongozo ya kuyasimamia maadili na mapambano dhidi ya rushwa na kuchukua hatua kwa watumishi wanaokiuka maadili na kuhusika na vitendo vya rushwa.

Njia bora za uhifadhi wa urithi wa taifa kwa maendeleo endelevu

Katika kufikia maendeleo endelevu nchini Tanzania, uhifadhi wa urithi wa taifa ni jambo lisilofepuka. Taifa linahitaji njia bora za uhifadhi wa urithi ili kuyaleta maendeleo yenye tija. Kuna njia mbalimbali za uhifadhi wa urithi wa taifa. Kila njia ina umuhimu na mchango wake katika kuendeleza urithi wa taifa. Hata hivyo, zifuatazo ni miongoni mwa njia bora zinazotumika kuhakikisha kunakuwapo na uhifadhi madhubuti wa urithi wetu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

(a) Kuyatangaza maeneo ya kihistoria: Kupitia njia hii, serikali inayateua na kuyatangaza maeneo yote yenye historia na urithi wa kipekee kuwa maeneo ya urithi wa taifa. Njia hii inahusisha hatua muhimu za uhifadhi kama vile kuiweka mipaka na ulinzi ili kuzuia uvamizi na uharibifu wa maeneo yanayohusika. Pia, kuhakikisha upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu maeneo hayo kunawezesha utunzaji wake. Miongoni mwa maeneo yaliyotangazwa na serikali ya Tanzania ni majumba ya kale ya Bagamoyo na Zanzibar, Olduvai Gorge na michoro ya mapangoni ya Isimila na Kondoa Irangi. Njia hii imechangia sana katika kuhifadhi na kulinda urithi wetu kwa maendeleo endelevu.

(b) Kuzikuza na kuzihifadhi lugha za asili na tamaduni zake: Kuzikuza na kuzihifadhi lugha zetu za asili na utamaduni wa jamii zetu ni moja ya njia bora ya kuuhifadhi urithi wa taifa. Lugha za asili ni muhimu katika kujenga na kuudumisha utambulisho wa taifa na kuzuia kupotea kwa utamaduni wa jamii yetu. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanzisha mipango ya kuzikuza na kuzidumisha lugha na tamaduni za asili. Mipango hiyo ni pamoja na kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa lugha na tamaduni zao. Aidha, jamii imekuwa ikihamasishwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kitamaduni kama vile matamasha ya kiutamaduni. Pia, jamii zinahamasishwa kuzirekodi na kuzihifadhi lugha na tamaduni za asili. Aidha, serikali imeitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa katika shughuli za kiserikali, kijamii na kielimu.

(c) Kuhifadhi makumbusho na nyaraka za kihistoria: Uhifadhi wa makumbusho na nyaraka za kihistoria ni njia bora ya kuuhifadhi historia na utamaduni wa taifa letu. Makumbusho na nyaraka hutoa fursa kwa jamii kujifunza na kuielewa historia, mila na desturi zao. Pia, hutoa fursa adhimu kwa watafiti na wataalamu mbalimbali kupata taarifa za kihistoria na kitamaduni. Njia hii inachangia kikamilifu katika kuulinda urithi wa taifa letu na kuleta maendeleo endelevu katika sekta za elimu na utamaduni. Mifano ya njia hii ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi ya Nyaraka za Taifa Tanzania (Tanzania National Archives) iliyoko mkoani Dar es Salaam, Kituo cha Nyaraka za Taifa kilichopo Dodoma na Arusha pamoja na Idara ya Nyaraka za Taifa (Makavazi) za kikanda kama Mbeya na Mwanza.

(d) Kuvihifadhi vitu vya kale: Hii ni miongoni mwa njia bora ya uhifadhi wa urithi wa taifa. Njia hii inahusisha utunzaji wa vitu vyenye thamani kubwa kihistoria, kitamaduni na kisanaa. Vitu hivyo ni pamoja na majengo ya kihistoria, kazi za sanaa za asili za mababu na mabibi zetu, na vitu vingine vya kale vinavyouonesha utajiri wa tamaduni zetu za asili. Mojawapo ya njia za uhifadhi wa vitu vya kale ni kuvifanyia ukarabati bila kubadilisha muundo wake wa asili. Hii husaidia kuhakikisha kuwa vitu vya kale (turathi) kama makaburi na majengo yanabaki imara na yanadumu na kuendelea kuwa ukumbusho kwa vizazi vijavyo. Mbali na ukarabati, ni muhimu pia kuweka mfumo wa hali ya juu wa ulinzi wa vitu vya kale vyenye thamani ili visiharibiwe au kuibwa na wahalifu na kutoweka. Kuhifadhi vitu vya kale ni uwekezaji muhimu katika maendeleo endelevu ya taifa kwani hutoa fursa za kiuchumi kupitia utalii wa utamaduni.

Kazi ya kufanya 2.5

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa, ikiwamo mitandao, bainisha vituo vingine ambako malikale (turathi) zimehifadhiwa. Katika kila kituo, bainisha malikale zilizohifadhiwa.

Zoezi

1. Fafanua maadili na urithi ambao hutoa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya jamii.

2. Eleza jinsi uadilifu katika matumizi ya urithi wa rasilimali zetu unavyoweza kuleta maendeleo ya taifa.

3. Fafanua jinsi kuwapo kwa vitendo vya rushwa kunavyoweza kuathiri urithi wa taifa.

4. Je, unafikiri ni kwa jinsi gani serikali, taasisi za utamaduni na jamii huweza kushirikiana katika kuboresha uhifadhi wa urithi wa taifa?

5. Pendekeza mikakati ya kuyahifadhi maeneo ya kihistoria na urithi yanayopatikana katika mkoa unaoishi.

MAJIBU YA ZOEZI

1. Kama raia wa Tanzania una jukumu gani katika kuhakikisha kwamba maadili na urithi wa taifa vinachangia maendeleo yetu?

  1. Kuzingatia na kuendeleza maadili mema kama vile uadilifu, uzalendo, uwajibikaji, heshima na mshikamano.
  2. Kulinda na kuhifadhi maeneo ya kihistoria, vitu vya kale na urithi wa taifa.
  3. Kuwafundisha vijana na jamii kuhusu umuhimu wa historia, utamaduni na urithi wa taifa.
  4. Kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu, kuiba au kuhatarisha vitu na maeneo ya urithi wa taifa.
  5. Kushiriki katika shughuli za maendeleo zinazotumia utamaduni na urithi wa taifa kwa njia endelevu.
  6. Kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu vitendo vya uharibifu, wizi au biashara haramu ya vitu vya urithi wa taifa.
  7. Kutumia rasilimali za urithi kwa njia endelevu ili ziwanufaishe wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

2. Pendekeza mikakati mitano ya kutumia maadili na urithi wetu ili kuleta maendeleo endelevu katika taifa letu.

  1. Kuendeleza utalii wa kiutamaduni na kihistoria kwa kutangaza maeneo ya kihistoria, makumbusho, sanaa, mila na desturi za Tanzania.
  2. Kutoa elimu kuhusu maadili na urithi wa taifa kupitia shule, vyombo vya habari na programu mbalimbali za kijamii.
  3. Kukuza sanaa na kazi za mikono za Kitanzania ili kuongeza ajira, kipato na fursa za kiuchumi kwa wananchi.
  4. Kuhifadhi maeneo na vitu vya kihistoria kwa kutumia sheria, teknolojia na ushiriki wa jamii.
  5. Kukuza matumizi endelevu ya urithi wa taifa kwa kuhakikisha kwamba shughuli za kiuchumi haziuharibu urithi wala mazingira yanayouzunguka.

3. Eleza jinsi wananchi wanavyoweza kushirikiana na serikali katika kuuhifadhi na kuendeleza urithi wa taifa.

  1. Kutoa taarifa kwa serikali kuhusu uharibifu, wizi au biashara haramu ya vitu vya urithi wa taifa.
  2. Kushiriki katika kampeni za usafi, ukarabati na uhifadhi wa maeneo ya kihistoria.
  3. Kuzingatia sheria na kanuni zinazolinda urithi wa taifa.
  4. Kushiriki katika shughuli za utalii wa kiutamaduni na kihistoria.
  5. Kuhifadhi na kurithisha mila, desturi, lugha, sanaa na maarifa ya jadi kwa vizazi vijavyo.
  6. Kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa urithi wa taifa.
  7. Kushiriki katika miradi ya maendeleo inayohusiana na urithi wa taifa bila kuharibu maeneo ya kihistoria.
  8. Kulinda mali za urithi zinazopatikana katika jamii na kuzifikisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya uhifadhi.

4. Pendekeza mikakati ya kuyahifadhi maeneo ya kihistoria na urithi yanayopatikana katika mkoa unaoishi.

  1. Kuweka na kutekeleza sheria kali dhidi ya uharibifu, wizi na uuzaji wa vitu vya kihistoria.
  2. Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maeneo ya kihistoria na urithi wa taifa.
  3. Kuweka alama na mipaka inayoonyesha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi.
  4. Kufanya ukarabati na matengenezo ya mara kwa mara ya maeneo ya kihistoria.
  5. Kushirikisha jamii inayozunguka maeneo hayo katika ulinzi na usimamizi wa urithi.
  6. Kukuza utalii katika maeneo ya kihistoria ili kuongeza mapato yatakayosaidia shughuli za uhifadhi.
  7. Kutumia teknolojia kurekodi, kuhifadhi na kutangaza taarifa kuhusu maeneo ya kihistoria.
  8. Kudhibiti ujenzi na shughuli nyingine za kibinadamu zinazoweza kuharibu maeneo ya kihistoria na urithi.

5. Pendekeza mikakati ya kuyahifadhi maeneo ya kihistoria na urithi yanayopatikana katika mkoa unaoishi.

  1. Kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa maeneo ya kihistoria na urithi wa taifa.
  2. Kuimarisha ulinzi wa maeneo ya kihistoria dhidi ya uharibifu na uvamizi.
  3. Kutekeleza sheria na kanuni za uhifadhi wa urithi wa taifa.
  4. Kushirikisha wananchi katika kulinda na kutunza maeneo ya kihistoria.
  5. Kufanya ukarabati na matengenezo ya maeneo yaliyoharibika.
  6. Kutumia teknolojia katika kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za maeneo ya kihistoria.
  7. Kuendeleza utalii wa kiutamaduni na kihistoria kwa manufaa ya jamii na taifa.
  8. Kudhibiti shughuli za kiuchumi na ujenzi zinazoweza kuharibu maeneo ya kihistoria.

Hitimisho

Uhifadhi wa maadili na urithi wa taifa ni jukumu la wananchi wote kwa kushirikiana na serikali. Ushirikiano huo husaidia kulinda historia, utamaduni na utambulisho wa taifa, pamoja na kutumia urithi huo katika kuleta maendeleo endelevu.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi la marudio

1. Kama raia wa Tanzania una jukumu gani katika kuhakikisha kwamba maadili na urithi wa taifa vinachangia maendeleo yetu?

2. Pendekeza mikakati mitano ya kutumia maadili na urithi wetu ili kuleta maendeleo endelevu katika taifa letu.

3. Eleza jinsi wananchi wanavyoweza kushirikiana na serikali katika kuuhifadhi na kuendeleza urithi wa taifa.

4. Eleza changamoto angalau tano zinazoukabili uhifadhi wa urithi wa taifa na njia ya kuzitua.

5. Eleza mchango wa teknolojia katika uhifadhi wa urithi wa taifa.

6. Jamii ya Kitanzania inawezaje kuitumia historia na urithi kama chanzo cha kujenga utambulisho wa kitaifa?

7. Ni kwa namna gani tunaweza kutumia historia na urithi wa taifa kama chanzo cha kujenga uchumi imara na endelevu?

8. Eleza namna unavyoweza kuhamasisha jamii katika kuulinda na kuuhifadhi urithi wa kitamaduni ili uweze kuchangia katika maendeleo ya taifa.

9. Kwa uzoefu wako, unadhani mabadiliko katika maadili yameathiri kwa kiasi gani uhifadhi wa urithi wa taifa?

10. Unadhani vijana wanaweza kuchangia kwa njia zipi kukuza maadili na kuhifadhi urithi wa taifa kwa ajili ya maendeleo endelevu?

11. Linganisha uhifadhi wa urithi wa taifa kwa njia za jadi na njia za kisasa huku ukizingatia faida na changamoto za kila njia.

12. Pendekeza njia nyingine za uhifadhi wa historia na urithi ambazo hazijaelezwa katika sura hii.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256