Sura Ya 02: Fasihi simulizi na fasihi andishi

Utangulizi

Fasihi simulizi na fasihi andishi ni sanaa muhimu ambazo mtu huzitumia kwa malengo ya kujiburudisha, kuelimisha na hata kuhifadhi utamaduni wa jamii. Katika sura hii, utajifunza kuhusu tanzu na vipera vya fasihi simulizi na fasihi andishi na pia utajifunza uhusiano uliopo baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi. Aidha, utajifunza kuhusu mchango wa fasihi simulizi katika maendeleo ya fasihi andishi na mchango wa fasihi kwa jumla katika maendeleo ya jamii. Umahiri utakaoujenga katika sura hii utakusaidia kuchambua na kutathmini vipengele mbalimbali katika maisha.

Nyenzo ya kuwasilisha mawazo katika miktadha mbalimbali

Shughuli ya 2.1

Kwa kutumia vyanzo vya mkindoni na maktabani, chunguza tanzu na vipera vya fasihi simulizi kisha jibu maswali yafuatayo:

  1. Nini tofauti ya utanzu na kipera?
  2. Kuna tofauti gani kati ya utani na majigambo?
  3. Kuna tofauti gani kati ya utanzu wa hadithi na semi?
  4. Sanaa za maonesho zina sifa zipi?
  5. Nini tofauti ya misemo na misimu?

Tanzu na vipera vya fasihi simulizi

Wataalamu mbalimbali (kwa mfano Mulokozi na Wamitila) wamegawanya fasihi simulizi katika tanzu na vipera mbalimbali ambavyo vimeoneshwa katika Kielelezo namba 2.1.

Kielelezo namba 2.1: Tanzu na vipera vya fasihi simulizi

Yafuatayo ni maelezo ya tanzu na vipera hivyo:

Shughuli ya 2.2

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya maarifa, fafanua utanzu wa hadithi na vipera vyake.

Hadithi

Hadithi ni utungo unaotumia lugha ya mjazo (nathari) ili kueleza kisa fulani kwa mpangilio wa matukio. Mpangilio huo hutumia wahusika ambao ndio watendaji wa matukio hayo. Vilevile, hadithi huwa na kisa kinachofululiza tangu mwanzo hadi mwisho ili kukamilisha muundo wake.

Hadithi huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira katika mandhari maalumu kama vile chini ya mti mkubwa, sebuleni, darasani au uwanjani. Vilevile, huweza kuwasilishwa kwa njia za kidijiti. Aghalabu, simulizi hufanyika katika muda maalumu, khususani baada ya kazi. Kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 2.1, utanzu wa hadithi una vipera vitano ambavyo ni ngano, tarihi, visasili, vigano, na soga.

(a) Ngano

Ngano ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu. Ni kipera cha mwanzo kabisa katika utanzu wa hadithi. Kwa kawaida, mtunzi wa ngano hajulikani. Ngano hupokezanwa na kuendelezwa kutoka kizazi hadi kizazi. Maudhui yake hujikita katika maadili, uhusiano na mwenendo mzuri katika jamii. Aghalabu, ngano ni hadithi za burudani ambazo husimuliwa katika mazingira ya starehe na mapumziko. Ngano ina vipera vidogo kadha. Baadhi ya vipera hivyo ni kisasuli, hurafa, hekaya na istiara.

Kisasuli

Kisasuli ni hadithi ya kisanaa yenye kueleza usuli na sababu za jambo, tukio au hali. Mathalani, zipo hadithi zinazoeleza kwa nini mnyama fulani anapenda kushirikiana na wanadamu au ameumbika kwa namna fulani. Tazama mfano wa kisasuli cha hadithi ya "Kwa nini nyoka hana miguu?"

Kwa nini nyoka hana miguu?

Siku moja Nyoka pamoja na wanyama wengine walialikwa kwenye sherehe nyumbani kwa mfalme. Kule walikula na kunywa! Baadaye mfalme aliwaita ili wapewe zawadi. Kwa sababu ya uroho wake, Nyoka hakusikia wito. Alipozinduka, alikuta miguu yote, hata ile hafifu ya Tandu na Buibui, imeshatolewa; akabakia anajiburuza kwa tumbo lake. Mpaka leo hii nyoka hana miguu (Balisidya, 1987).

Hurafa ni ngano zenye wahusika wanyama tu. Wanyama hao huwakilisha tabia na matendo ya binadamu kwa kurejelea masuala yanayopatikana katika jamii. Maudhui katika hurafa hueleza kuhusu tabia nzuri au mbaya za binadamu, kama vile woga, ulafi na tamaa. Katika hurafa, wanyama wanaotumiwa ni kama vile sungura, fisi na kobe. Sungura huwakilisha ujanja, kutokata tamaa na kutochoka. Fisi huwakilisha tamaa, ulafi, woga, uzembe na ujinga. Kobe huwakilisha ukimya, busara na utulivu. Aidha, ni mhusika ambaye hufanya vitu kimyakimya lakini huibuka mshindi. Ufuatao ni mfano wa hurafa:

Sungura na Fisi

Siku moja Sungura alipokuwa matembezini alikutana na Fisi. Fisi alimwangalia Sungura na kumuuliza, "Wewe unayekodoa macho hivi unaenda wapi, au kuila nyama yako?" Sungura akamwangalia Fisi na kumwambia, "Nimeambiwa na Simba nimsubiri hapa ndipo tuandamane hadi kwake nikamtayarishe ini la Fisi analolitamani sana." Fisi akamwangalia Sungura na kumwuliza, "Huyo Simba yuko wapi?" Sungura akaita kwa sauti ya juu, "Simbaaaaaa!"Baada ya kuita kwa sauti hiyo, Sungura alijigeuza kidogo, akapiga mluzi na kusema kwa sauti nzito, "Naja sasa hivi. Naandama nyayo za Fisi aliyepita hapa. Natamani kumkamata ili nipate ini lake nikuletee ukanitayarishie kama tulivyoagana. Mara tu Fisi alipoyasikia hayo, aligeuka na kutimua mbio kuelekea kichakani. Sungura alibaki alikokuwa na kuangua kicheko.

Hekaya ni ngano zenye visa visivyo vya kawaida vinavyoambatana na masaibu na pengine hata ujanja wa mhusika mkuu ambaye huweza kuwa mtu au mnyama. Hekaya hujengwa na visa vingi vinavyotofautiana. Mhusika mkuu katika hekaya hupitia misukosuko mingi hadi kukaribia kushindwa. Hata hivyo, katika hatua za mwisho kabisa, mhusika huyu huweza kuibuka mshindi kwa namna isiyotarajiwa.

Lengo la hekaya ni kumtia mtu moyo asikate tamaa anapopitia changamoto za aina mbalimbali. Kimsingi, kinachohimizwa ni kutumia akili kutatua matatizo ya maisha. Kwa kumtumia mhusika sungura, kwa mfano, tunahimizwa kuwa wajanja na kutokujidharau hata kama ni wadogo. Umbile dogo linaweza kuwakilisha pia uwezo wa kiuchumi kama vile kuwa na mtaji mdogo. Mtu anaweza kutumia mtaji mdogo kufanya biashara mpaka kufikia kiwango cha kuwa mfanyabiashara mkubwa. Ufuatao ni mfano wa hekaya:

Mfanyabiashara na Wakeze

Hapo zamani, kulitokea mfanyabiashara mmoja aliyekuwa na mali nyingi sana. Basi alioa mke, baadaye akaongeza mke wa pili (Bi mdogo). Wakaishi hivyo. Alitokea kumpenda zaidi Bi. Mdogo na kumnyanyasa Bi. Mkubwa (mke wa kwanza).

Siku moja, alikuwa na safari ya kwenda kununua bidhaa za duka lake. Basi akamwambia Bi. Mdogo ataje mahitaji yote ambayo ungependa aletewe kama zawadi. Bi. Mdogo akataja vitu vingi. Naam, kwa kuwa mfanyabiashara yule alikuwa akimpenda sana, hakusita kumhakikishia kwamba angemletea. Kwa shingo upande, alimwendea vilevile Bi. Mkubwa na kumwambia ataje zawadi ya kumletea. Yule Bi. Mkubwa akamwambia mumewe asisumbuke ila amletee pete na kipande cha akili. Basi, kwa dharau yule bwana akakubali.

Basi tajiri yule akafunga safari akafika huko, akanunua vifaa vyake vyote alivyovihitaji kwa ajili ya duka lake. Vilevile, akanunua vitu vyote kama vile nguo ambazo Bi. Mdogo alimtuma, pamoja na pete ya Bi. Mkubwa. Sasa akakwama wapi apate kipande cha akili. Akazunguka maduka yote, asipate. Mwishowe, akaona ni upuuzi kuendelea kutafuta kipande hicho.

Basi, katika ghadhabu yake, akawa akimtukana huyo Bi. Mkubwa, jinsi alivyokuwa mpumbavu. Ikatokea kwamba Bi. Kizee mmoja akamsikia alivyolalamika na kuapiza. Yule Bi. Kizee akamuuliza kwa nini alikuwa akilalamika. Yule bwana akamsimulia kisa chote. Bi. Kizee akamwambia yule bwana kuwa asipate taabu kwani kipande hicho anacho nyumbani. Wakafuatana kuelekea nyumbani kwa huyo Bi. Kizee. Kufika karibu na kule nyumbani, Bi. Kizee akamweleza kwamba kipande hicho kiko nyumbani kwa yule bwana, ila tu akitaka kukipata sharti atakapokaribia nyumbani kwake ajipake kinyesi, halafu aone jinsi wake zake watakavyompokea.

Basi tajiri akafanya kama alivyoagizwa. Alipokaribia nyumbani kwake, akajipaka kinyesi mwili mzima, akawa hovyo kabisa kisha akabisha hodi kwanza nyumbani kwa Bi. Mdogo. Bi. Mdogo kufungua mlango katika harakati za kumlaki, akaona mumewe kajaa kinyesi mwili wote. Bi. Mdogo akafoka sana na kumwambia asithubutu kuingia mle ndani hadi awe ameoga vizuri.

Basi yule bwana katika hali hiyohiyo, akaenda kwa Bi. Mkubwa. Bi. Mkubwa akamwona mumewe katika hali ile, akasikitika sana. Akamvua nguo zenye kinyesi, akamwosha, na kumvika nguo nyingine.

Ndipo yule bwana akamwambia mke wake, "Pete na kipande cha akili vyote nimepata. Isipokuwa kipande cha akili nimekipata hapahapa." Akachukua zawadi zote, hata zile za Bi. Mdogo, akampa yule Bi. Mkubwa, na kumfukuza Bi. Mdogo.

Wakaishi raha mustarehe.

Riwaya ya Kiswahili (Madumulla, 2009: 94 - 95)

Istiara ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana iliyofichika. Kwa hiyo, maana huwasilishwa kwa njia ya mafumbo. Kwa mfano, hadithi mashuhuri ya zimwi linalovamia kijiji na kuwameza wanakijiji wote isipokuwa mwanamke mmoja mjamzito ni istiara. Katika hadithi hiyo, mama huyo mjamzito baadaye anajifungua mtoto na kumlea akiwa mafichoni. Mtoto anapokua anamuuliza mama yake kwa nini wako peke yao kijijini, wakazi wengine walikwenda wapi. Mama yake anamweleza kuwa watu wote walimezwa na zimwi ambalo linaishi katika msitu ulio karibu na kijiji hicho. Mtoto anaamua kwenda kupambana na zimwi hilo hadi analiua. Baada ya kuliua analipasua tumbo na kuwatoa watu wote waliomezwa wakiwa bado hai. Watu wanafurahi na kumfanyamtoto huyo kuwa kiongozi wao. Kiistiara, hadithi hii huweza kuwakilisha ukoloni na mapambano ya kujikomboa. Zimwi linamwakilisha mkoloni, na mtoto ni mkombozi. Pia, hadithi hii inaweza kuwa ishara ya kupigania haki ya aina yoyote (Thomas, 2011)

Kwa kawaida, ngano huwa fupi kwa sababu ya muundo wake wa kuwa na kisa kimoja. Wahusika wa ngano ni bapa kwa maana kwamba mhusika akiwa mwema ni mwema mwanzo hadi mwisho wa hadithi, hivyo hivyo kwa mhusika mwovu. Lengo kuu la ngano, mbali na kuburudisha, ni kuadibu, kuadili na kuelimisha jamii. Hujaribu kujenga utu bora kwa kueleza wema na ubaya.

(b) Tarihi

Tarihi ni hadithi zinazohusu matukio muhimu ya kihistoria. Msingi wa hadithi hizi ni matukio ya kihistoria. Matukio haya yanaweza kuwa ya kweli au ya kubuni au mchanganyiko wa ukweli na ubunifu. Aghalabu, wahusika wa hadithi hizi ni binadamu. Miongoni mwa mifano maarufu ya tarihi ni Tarihi ya Kilwa. Tazama mfano ufuatao:

Mji wa Kilwa na Watawala Wake

Hapo awali, Mji wa Kilwa ulikuwa ukitawaliwa na Waswahili wenyewe. Kiongozi wa mwisho kabla ya ujio wa wageni alijulikana kwa jina la Mndimbo. Alitawala mpaka karne ya saba. Watawala waliofuata walikuwa wenye asili ya Kiarabu. Sultani wa kwanza, Ali bin-Hasan, alianza kutawala mwaka 1200BK. Inasemekana alitengeneza sarafu ya kwanza. Utawala wake ulifuatiwa na al-Hasan bin Daudi, ambaye alikuwa mukuu wa Ali, lakini wengine walipinga kwa kuwa alikuwa mpwa wake na utawala wake ulikoma miaka ya 1300BK. Utawala mwingine ulianza mwaka 1300 ambapo al-Hasan bin Talut alianza kutawala. Al-Hasan bin Talut alikuwa mtawala wa kwanza katika ukoo wa tawala za Abu' l-Mawahibu. Alikuwa na sarafu chache sana zinazoashiria kipindi kifupi cha utawala wake. Mtoto wake aliyeanza kutawala alijulikana kwa jina la Sultani Sulaiman bin al-Hasan. Isivyo bahati, mtawala huyu haoneshwi katika orodha za Masultani katika fasili ya Kiarabu ingawa kuna sarafu nyingi ambazo zinasemekana zilikuwa zake. Alishika madaraka kwa miaka miwili tu. Mwaka 1320 al-Hasan bin Sulaiman alianza kutawala. Mtawala huyu alitembelewa na Ibn Batuta mnamo mwaka 1331. Inasemekana, huyu ndiye aliyejenga husuni kubwa na alikuwa na sarafu nyingi. Kuna habari kuwa Mafia ilichukuliwa na Kilwa katika utawala huu. Mtawala aliyefuata ni Daudi bin Sulaiman; huyu alikuwa ndugu wa al-Hasan bin Sulaiman. Inasemekana alikuwa na sarafu chache sana na ndiye mtawala wa mwisho kutengeneza sarafu kabla ya ujio wa Wareno (Massamba, 2017).

(c) Visasili

Visasili ni hadithi zinazoelezea chimbuko au asili ya jamii, ukoo, au kundi fulani. Huelezea pia tamaduni mbalimbali na namna jamii fulani ilivyofika katika eneo fulani. Kadhalika, visasili hueleza na kufafanua masuala ya kimaumbile na kiimani yanayomhusu na kumsumbua binadamu kama vile maradhi na kifo. Visasili hueleza pia maana ya maisha na hatima ya mwanadamu kulingana na imani za jamii inayohusika. Kwa kawaida, visasili huheshimiwa na kuaminiwa na wanadamu, na huhusishwa na kuwa vielelezo vya miviga na ibada zao. Mfano wa kisasili ni hadithi za mataifa mbalimbali kuhusu kuumbwa kwa ulimwengu na vilivyomo. Mfano mzuri ni hadithi ya Wakikuyu ya "Gikuyu na Mumbi" ambayo inapatikana katika kitabu cha Naushangilia Mlima Kenya (Kenyatta, 1966), simulizi ya "Asili ya Jina la Wakinga" kutoka kwa Wakinga, na simulizi ya "Adamu na Hawa" kutoka Mashariki ya Kati ambayo inapatikana katika Biblia na Kurani.

Mfano wa Kisasili

Asili ya Jina la Wakinga

Wenyeji wa jamii ya Wakinga wanapatikana Nyanda za Juu Kusini katika eneo lenye vilima, uoto mzuri wa asili na vijito vinavyotiririka kama mkufu usio na mwisho. Wenyeji wa jamii hii walikuwa na shughuli mbalimbali tangu enzi za zamani. Walijishughulisha na ufuaji chuma, viazi, ngano na njegere. Palipo na ustawi hapakosekani adui. Jamii hii ilikuwa na mbinu zake za siri za ulinzi ambazo kila mwanajamii alifundishwa katika makuzi yake. Wakinga walikuwa na maadui na walipigana vita mara kwa mara na kuvishinda vita hivyo. Adui alipovamia ardhi ya Wakinga, kiongozi alijitokeza na kupiga kelele "Vakinga Vakinga!" (maana yake jihadhari) akiwa amepanda juu ya kilima. Baada ya hapo kila mwanajamii alitambua kuwa hiyo ni vita na kila mmoja aliwajibika kupambana. Wazee waliongoza jamii nzima kwa kutoa ushauri na kuombea ushindi, vijana walichukua silaha za kivita, wanawake na watoto walikimbilia kwenye mahandaki. Huo ndio mwanzo wa Wakinga kuitwa Wakinga kulikotokana na sauti hiyo ya tahadhari.

(d) Vigano

Vigano ni hadithi fupifupi za kifasihi simulizi. Mafunzo yake hutolewa kwa kutumia lugha ya picha kama ilivyo kwa methali. Hadithi hizi zina hadhi ya methali ingawa hutumia taswira pana kuliko methali. Kimsingi, hadithi za namna hii hutolewa kama vielelezo, hasa wakati wa mazungumzo au maongezi. Lengo kuu huwa ni kumkanya na kumfunza anayesikiliza.

Kwa mfano, kigano kinaweza kueleza kuhusu mzazi aliyempenda mno mtoto wake wa pekee kiasi cha kutothubutu kumkemea au kumrudi. Hatimaye, mtoto alijenga tabia mbaya. Basi, msimulizi husema kwa methali: Mchelea mwana kulia hulia mwenyewe.

Aghalabu, vigano hutokea katika mazungumzo na, wakati mwingine, hutungwa papo hapo. Kwa mantiki hiyo, vigano vingi huwa havienei kwa sababu hufungamanishwa na muktadha wa maongezi na hutungwa kwa ajili ya mada husika tu. Kwa hiyo, hupotea baada ya mada kuwasilishwa.

(e) Soga

Soga ni hadithi fupifupi za utani na ucheshi. Hadithi hizi husimuliwa kwa mfuatano wa matukio yanayochekesha. Soga hujengwa juu ya tukio moja tu. Tukio hilo, aghalabu, hulenga kuchekesha kwa kubeza na kukejeli. Pia, hueleza mambo ya ukweli unaoumiza kwa njia ya ucheshi ili kupunguza ukali wa ukweli huo. Soga hupatikana au hufanywa na watu wa jamii zenye historia ya kufanyiana utani kama vile jamii za Wanyaturu na Wakurya, Wahaya na Waha, Wachaga na Wapare. Kwa ujumla, soga hujikita katika kuburudisha na, wakati mwingine, kuelimisha jamii. Tazama mfano wa soga inayowahusu Wamakonde hapa chini:

Kisa cha Mmakonde na Ngedere

Mmakonde mmoja alikwenda shambani kwake, akamkuta ngedere akila mahindi shambani mwake. Ngedere alipomwona Mmakonde akakimbilia juu ya mti. Mmakonde akamwona kule alikojificha, akamwambia: "Wee ngedere nimechakuona; uchijifanye n'janja, telenka hapa chini nikupige nchale ili upate adhabu moja tu. Vinginevyo, n'kupige nchale ukiwa hukohuko juu ya nti, upate adhabu mbili: Adhabu ya kupigwa nchale, na adhabu ya kuanguka kutoka juu ya nti baada ya kupigwa nchale. Je, wewe ungekuwa ngedere ungefanyaje?"

Shughuli ya 2.3

Tumia vyanzo vya mtandaoni na maktabani, kufafanua semi na vipera vyake kwa kuzingatia maana na sifa.

Semi

Semi ni tungo fupifupi za fasihi simulizi, na aghalabu, hutumia picha, tamathali na ishara. Semi hutumika kutoa mafunzo, nazo zimegawanyika katika vipera mbalimbali kama vile methali, misemo, mizungu, mafumbo, na vitendawili.

(a) Methali

Methali ni semi za kimapokeo zenye hekima na busara zinazoeleza falsafa na uzoefu wa jamii fulani kwa muhtasari. Semi hizi hubeba maana pana kuliko maneno yenyewe yanayotumiwa. Methali hutumika kusisitiza, kuelimisha, kuonya au kupongeza kwa njia za busara. Aghalabu, methali hujengwa kwa sitiari. Sitiari hizo hujitokeza katika pande mbili za methali ambazo hubainishwa kwa mkato. Angalia mifano ifuatayo:

  1. Mtaka yote kwa pupa / hukosa yote.
  2. Usipoziba ufa / utajenga ukuta.
  3. Aisifuye mvua / imemnyaa.
  4. Chanda chema / huvikwa pete.
  5. Mtaka cha uvunguni / sharti ainame.

Mifano ya hapo juu inaonesha kuwa methali hubeba dhima mahususi. Kwa mfano, methali (i) inawaasa wanajamii kutofanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Ni vyema kumakinikia jambo moja ili kulifanya kwa ufanisi, ndipo uanze jambo jingine. Katika mfano wa (ii), jamii inaaswa kurekebisha tatizo katika hatua za mwanzo, yaani kabla madhara makubwa hayajatokea.

(b) Misemo

Misemo ni tungo zitumiazo picha, ishara na tamathali kueleza kitu au wazo kwa ufupi ili kuelimisha au kuadilisha. Misemo hufananisha maisha na matukio au vita. Wakati mwingine, misemo hutumika kutambulisha mazingira maalumu au kuijulisha hadhira kuhusu hali fulani ya kijamii. Angalia mifano ifuatayo:

  1. Bendera hufuata upepo.
  2. Elimu ni bahari.
  3. Ukubwa jalala.

Mfano wa (i) unaonesha hali ya maisha, kwani wapo watu ambao hufuata mkumbo bila kufikiria wala kuhoji kwa nini wanafanya jambo fulani na, hatimaye, kujikuta kwenye matatizo. Katika mfano wa (ii), elimu inafananishwa na bahari. Bahari ni kubwa, na haina mwisho, vivyo hivyo kwa elimu. Elimu hutupatia maarifa na ujuzi wa aina mbalimbali. Pia, elimu haina ukomo, kwani binadamu hujifunza kila siku. Mfano wa (iii) unalinganisha hali ya mtu kuwa mkubwa wa umri au cheo, na kutupiwa lawama hata kama hajatenda kosa, kama lilivyo jalala ambapo watu hutupa taka za aina mbalimbali.

(c) Mizungu

Mizungu ni kauli zenye mafumbo zinazoonesha ukinzani wa fikra au tukio. Mbali na vitendawili vya kawaida, kuna vitendawili vingine vijulikanavyo kama mizungu. Mizungu hii hutumia zaidi mafumbo. Kwa mfano, inaelezwa kwamba mtu hawezi kumwoa ndugu wa damu. Ukinzani huu umetumika kuonya ndugu wasiwe na uhusiano wa kimapenzi. Mizungu hutumia mafumbo ya hali ya juu, kwa hivyo hutumiwa na watu wazima katika miviga ili kueleza dhana na mawazo mbalimbali kwa maongezi au nyimbo. Mifano mizuri ya mizungu inayohusu jambo hili ni:

(i) Ua zuri sana limeota kwenye miiba; hivyo, huwezi kulichuma.

(ii) Papai limeiva nyumbani, ila siwezi kulila.

Mizungu hutumia lugha ya picha inayoonesha ukinzani wa fikra. Ukinzani husaidia kumfikirisha msikilizaji na kumpa changamoto ya kutafuta jibu. Mifano mizuri ya mizungu ni:

(i) Adui rafiki (moto)

(ii) Nimezishika lakini siwezi kuzitumia (mhasibu na fedha)

(d) Mafumbo

Mafumbo ni kauli au maelezo yanayoficha maana ambayo humtaka msikilizaji kuyafumbua. Kwa mfano, watu wanamteta mtu, ikitokea mtetwaji anakuja mahali hapo, mmoja wao anaweza kusema wifi kaja au shangazi kaja. Hii huwasaidia kubadilisha maongezi baada ya kufumbua wifi au shangazi kuwa ndiye mtu anayetetwa ingawa mtu huyo si wifi wala shangazi wa mtu yeyote katika kundi hilo.

Aidha, kwenye mazingira ambapo watu wanaongea lakini hawataki mmoja wao ajue maongezi yao, labda kwa sababu ni domokaya, mmoja wao anaweza kuwatahadharisha wenziwe kwa kusema hivi, Ooho! Mkorosho umeanguka! Inabidi waelewe kwamba "mkorosho ulioanguka" ni mmoja wao. Hivyo, wataongea kwa tahadhari kubwa. Aghalabu, mafumbo megi huwa ni kejeli dhidi ya watu wenye tabia mbaya. Mafumbo yana malengo ya kuelimisha, kuwezesha mawasiliano, kuburudisha, kukosoa na kuonya kuhusu mambo yanayotendeka miongoni mwa wanajamii.

(e) Vitendawili

Vitendawili ni semi fupifupi za mafumbo zenye kutumia lugha ya picha, tamathali na ishara kueleza jambo lililofichika. Jambo hilo ndilo jibu la fumbo. Kwa kawaida, kitendawili hupewa jibu kwa neno moja au zaidi au maelezo. Kama ilivyo katika kazi nyingine za fasihi, vitendawili hutumika kuburudisha, kukuza uwezo wa kufikiri, kupamba lugha, kukosoa au hata kukejeli. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Pango langu limejaa mawe - kinywa.

(ii) Nyumba yangu ina nguzo moja - uyoga/mwavuli.

(iii) Blanketi la babu lina chawa - mbingu na nyota.

(iv) Bibi amejitwisha machicha ya nazi - mvi.

Uundaji wa vitendawili hutegemea mazingira ambako kitendawili hicho hutumika. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Watoto wa sultani wamevaa kofia.

(ii) Nimenunua sungura nimemvika kofia.

(iii) Nikune kichwa nikupe moto.

Jibu la vitendawili hivi vyote ni njiti ya kiberiti.

Tofauti ya vitendawili vya (i), (ii) na (iii) inatokana na mazingira. Kitendawili cha (i) kimeundwa katika mazingira ambayo sultani aliwahi kuishi. Kitendawili cha (ii) kimeundwa katika sehemu yenye wafugaji au pori lenye sungura. Kitendawili cha (iii) kimeundwa katika mazingira yanayoakisi udugu, ambapo ni rahisi mtu kuomba kukunwa kichwa.

Shughuli ya 2.4

Tumia maktaba au maktaba mtandao na vyanzo vinginevyo kujadili maana, sifa na vipera vya ushairi simulizi.

Ushairi simulizi

Ushairi simulizi ni utanzu wa fasihi simulizi ambao huwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Ushairi simulizi ulianza wakati binadamu alipoanza kufanya kazi. Kupitia lugha, binadamu alibuni nyimbo za kazi. Nyimbo hizo ndizo msingi wa fasihi simulizi. Nyimbo za kazi zilitungwa kwa kuzingatia mapigo ya zana za kazi ili ziweze kukumbukwa kwa urahisi.

Ushairi simulizi hujipambanua na tanzu nyingine za fasihi simulizi kutokana na matumizi ya mizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani. Mbali na kuzingatia mambo hayo yanayohusu ushairi kwa jumla, ushairi simulizi una sifa ya kutungwa papo kwa papo na kufungamana na muktadha au tukio mahususi. Vipera vya ushairi simulizi ni nyimbo, mashairi, ngonjera, maghani na tenzi. Wakati mwingine, mashairi huambatana na ala za muziki za jadi ama za kisasa.

(a) Nyimbo

Nyimbo ni tungo za kishairi zinazowasilishwa kimuziki kwa kutumia sauti iliyo katika mpangilio fulani wa mahadhi na melodia, na inayozingatia mapigo ya kiurari. Mahadhi au tuni ni sauti mahususi ya uimbaji wa wimbo fulani, na melodia ni mpangilio na mwendo wa uimbaji wenye kuzingatia urari wa mapigo au ridhimu aghalabu hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine. Nyimbo huweza kuimbwa na kuchezwa pamoja na ala za muziki. Nyimbo huimbwa na mtu mmoja au kundi la watu. Wakati mwingine, kikundi cha waimbaji huwa na kiongozi na wafuasi wake. Kiongozi huanzisha wimbo, halafu wafuasi huitikia mkarara. Kiongozi wa nyimbo huitwa manju. Nyimbo zinaainishwa kwa kuzingatia dhima, hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana nazo. Kutokana na vigezo hivyo, tunapata baadhi ya aina kama ifuatavyo: tumbuizo, bembezi, kongozi, nyimbo za dini na wawe. Yafuatayo ni maelezo mafupi kuhusu aina hizi:

  1. Tumbuizo ni nyimbo za furaha ziimbwazo katika matukio mbalimbali kama vile harusini na ngomani.
  2. Bembezi/chombezi ni nyimbo za kubembelezea watoto.
  3. Kongozi ni nyimbo za kuaga na kukaribisha mwaka.
  4. Nyimbo za dini ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu.
  5. Wawe ni nyimbo za kilimo zinazopatikana karibu katika makabila yote ya Tanzania.
  6. Mbolezi ni nyimbo zinazoimbwa kufuatia matukio ya huzuni, hasa ya vifo.
  7. Nyimbo za watoto ni nyimbo zenye maudhui mahususi kwa ajili ya watoto.

(b) Mashairi

Mashairi ni tungo zenye kuelezea au kuonesha kwa ufupi wazo au jambo au hisi fulani kuhusu binadamu na mazingira yake. Mambo hayo huelezwa katika mpangilio maalumu wa maneno fasaha yenye muwala, aghalabu kwa lugha ya kitamathali yenye kugusa moyo. Tunaposema mpangilio wa maneno tunamaanisha kuwa mpangilio wa maneno katika shairi hufuata kanuni tofauti na ule wa nathari. Si lazima shairi kufuata kanuni za miundo ya sentensi inayotumika katika lugha husika. Mathalani, badala ya kuandika usikate tamaa maishani huweza kuandikwa maishani usikate tamaa - mpangilio ambao ni tofauti na mpangilio wa kawaida. Baadhi ya tungo za taarabu ni ushairi simulizi.

Ngonjera

Ngonjera ni neno la Kigogo lenye maana ya "twende pamoja" au "tuambatane." Kipera hiki kilikuwapo toka zamani ila kilihuishwa mwishoni mwa miaka ya 1960 na Mathias Mnyampala katika harakati zake za kuelezea siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Ngonjera ni mazungumzo au majibizano ya kishairi kuhusu mada fulani. Kwa kawaida, ngonjera haziimbwi, hughaniwa. Aghalabu, majibizano hayo huwa na washiriki wa pande mbili, upande wa wanaopinga na upande wa wanaotetea hoja. Wahusika hawa hutumia lugha ya kiishara pamoja na miondoko ya mwili kama vile mikono, macho na midomo. Kutokana na wahusika kutumia miondoko, ngonjera huitwa ushairi wa maigizo. Katika ngonjera, suluhisho hupatikana mwishoni mwa majibizano, ambapo pande mbili zinazopingana hukubaliana. Ingawa ngonjera za Mathias Mnyampala ni fasihi andishi, lakini zinaweza kutendwa jukwaani. Mfano mzuri ni ngonjera ya Mkopo wa Fedha ya Mathias Mnyampala inayopatikana katika kitabu cha Ngonjera za Ukuta. Ngonjera hiyo ni majibizano ya papo kwa papo.

Mkopaji

Hodi Bwana nimekuja, nina shida na tatizi

Nijile kutaka haja, arubani ghawazi

Tazileta kwa pamoja, siku mbili zizi hizi

Tafadhali nikopeshe, haondoe shida yangu

Mkopwaji

Nimekwisha kusikia, tuliza yako nafusi

Haja nitakukidhia, Inshallah kitu hukosi

Shida yako ni rupia, takujalia fulusi

Hebu njoo Jumamosi, bado nashauri moyo

Mkopaji

Hodi Bwana nawasili, kwa ile yetu miadi

Unihesabie mali, arubani nakidi

Muaminishe Jalali, nifanyie itikadi

Tafadhali nikopeshe, haondoe shida yangu

Mkopwaji

Moyo wangu siamini, kukuhesabia mali

Shuruti lete dhamini, ambaye msema kweli

Shilingi arubaini, kulipa huna dalili

Hebu njoo Jumapili, bado nashauri moyo

Ngonjera za Ukuta: Kitabu cha kwanza (Mnyampala, 1967:22)

(c) Tenzi

Tenzi ni tungo ndefu zinazoeleza tukio fulani linalotokea au lililowahi kutokea katika jamii; au zinazofafanua jambo au fikra fulani. Tenzi huwa na kisa kimoja kinachoelezwa kwa kina. Kisa hicho kinaweza kuwa maelezo kuhusu wasifu wa mtu fulani, jambo fulani la kihistoria au jambo lolote. Sifa ya kusimulia au kuelezea jambo kwa urefu ndio husababisha tenzi kuwa na beti nyingi kuliko mashairi au aina nyingine za ushairi.

Utendi ni utungo wenye masimulizi marefu kuhusu matendo ama matukio ya kishujaa na wasifu wa mashujaa. Utenzi na tendi huwa na muundo wenye kufungamana na mahadhi ya ala za muziki inayotumika au melodia ya uimbaji. Kwa kawaida, hazina urari wa vina na mizani. Tenzi zenye urari wa vina na mizani ni zile zenye kufuata kanuni za ushairi andishi wa Kiswahili japo chimbuko au utungaji wake ni wa kisimulizi. Mifano ya tenzi hizo ni Utenzi wa Nyakiiru Kibi (Mulokozi, 1997) na Utenzi wa Mwanakupona. Mfano wa tendi ni Utendi wa Fumo Liyongo (Kijumwa, 1913) katika Tenzi Tatu za Kale (Mh. Mulokozi, 1999). Katika tenzi hizo, mishororo haikugawanywa katika vipande viwili. Kila ubeti huwa una mistari minne; mistari mitatu ya kwanza ikiwa na vina vyenye urari na ule wa mwisho ukiwa na kina tofauti. Pamoja na vina hivyo kuwa na urari sawa, hubadilika toka ubeti mmoja hadi ubeti mwingine. Kina kinachorudiwa katika mstari wa mwisho, huitwa bahari. Ufuatao ni mfano wa beti za Utendi wa Fumo Liyongo ambao unatokana na utendi simulizi:

Niweleze kwa utungo,

Hadithi yake Liyongo,

Niweleze na mazinga,

Mambo yalomzingiya.

Liyongo kitamakali,

Akabarighi rijali,

Akawa mtu wa kweli,

Na haiba kaongeya.

Kimo kawa mtukufu,

Mpana sana mrefu,

Majimboni yu marufu,

Watu huya kwangaliya.

Ni mwanamume swahihi,

Kama simba unazihi,

Usiku na asubuhi,

Kutembea ni mamoya.

Kisa katiti kutuwa,

Mkobani akatowa,

Zitu alizotukuwa,

Nyumba ndima nisikiya.

Katowa kinu na mti,

Na jiwe na kupaza kuti,

Na zunguze si katiti,

Na mawe ya kupikiya.

Tenzi Tatu za Kale [Kijumwa, katika Mulokozi (Mh) (2009)]

Beti hizi ni sehemu ya simulizi ya kiutendi inayomhusu Fumo Liyongo. Simulizi hii inaakisi maudhui ya kipindi cha miaka ya 900-1500 BK. Hivyo, lugha iliyotumika ni ile inayoakisi kipindi hicho. Pia, simulizi katika utendi huu inahusu masuala kama vile nguvu za kimwili, kiakili, kisihiri, kivita na kiume (urijali).

Shughuli ya 2.5

  1. Tunga kazi kwa kutumia kipera kimojawapo cha ushairi.
  2. Chagua suala mtambuka mojawapo katika jamii kisha andaa majigambo.

Shughuli ya 2.6

Jadili sanaa za maonesho kwa kuzingatia maana, aina na sifa zake.

Sanaa za maonesho

Balisidya na Muhando (1976) wanadai kwamba sanaa za maonesho ni sanaa ambazo huwasilisha wazo ana kwa ana kwa kutumia usanii wa utendaji. Utanzu huu hujumuisha kipera chochote chenye mambo yafuatayo:

  1. Dhana ya kutendeka (tendo);
  2. Mtendaji (fanani);
  3. Uwanja wa kutendea (jukwaa);
  4. Watazamaji (hadhira); na
  5. Kusudio la kisanaa (maudhui).

Sanaa za maonesho huwa kwenye umbo linalotendeka. Huweza kugawanyika katika makundi mawili ambayo ni sanaa za maonesho za jadi na sanaa za maonesho mamboleo. Sanaa za maonesho za jadi ni zile zilizochipuka katika jamii za Kiafrika. Sanaa hizi hujumuisha majigambo, miviga, vichekesho, ngomezi, tambiko, utani, maigizo na michezo ya watoto. Ingawa miviga kama vile ibada, sherehe, jando na unyago ni matukio ya kijamii au kimila yenye kuvuka mipaka ya kisanaa, lakini inajumuishwa hapa kwa kuwa sanaa hutawala utendaji na uwasilishaji wa maudhui yake. Wakati wa uwasilishaji wa shughuli hizi, watu hufanya vitendo vya kisanaa kama vile uigizaji wa visasili, uchezaji ngoma, uimbaji na utongoaji mashairi, vikiambatana na matendo ya mwili. Kwa njia hii, watu huweza kuwasiliana wao kwa wao au kuwasiliana na miungu. Ijapokuwa dhima ya sanaa hizi hufanana kwa namna ya jumla, huwa kuna tofauti mahususi katika vipengele vya utendaji kati ya jamii au kabila moja na jingine.

Wakati wa ukoloni, sanaa za jadi, hasa zile zilizohusiana na imani za dini, zillipigwa vita. Hali hii ilisababisha sanaa kama vile matambiko kupotea katika baadhi ya jamii. Sanaa nyingine zimedumu mpaka leo kutokana na wito wa kitaifa wa kudumisha utamaduni wa Kitanzania na uimara wa jamii wa kutunza utamaduni wao.

Sanaa za maonesho mamboleo ni zile zilizotokana na athari za ujio wa wageni. Sanaa za namna hii ni vichekesho na maigizo.

Majigambo

Majigambo ni masimilizi ya kujisifia au kujikweza kwa mtu kuhusu mambo aliyowahi kufanya. Mambo hayo huwa ni ya kishujaa kama vile kupigana vita, kuua wanyama wakali au kufanya jambo lolote kubwa la kishujaa. Kwa kawaida, majigambo husimuliwa katika lugha ya kishairi na yanaweza kujitokeza katika fasihi andishi na fasihi simulizi, zikiwamo bongo fleva na taarabu. Mjigambi hufanya matendo mbalimbali. Aghalabu, mjigambi hubeba silaha kama vile mkuki na ngao au upinde na mishale. Kama mjigambi ametoka kuua simba, kwa mfano, ataonesha matendo ya jinsi alivyopambana na simba hadi kumshinda.

Makabila yenye sanaa za majigambo ni yale ya Ukanda wa Ziwa (kama vile Wakurya, Wasukuma na Wahaya), yale ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, hususani Wahehe, na ya Kaskazini mwa Tanzania, hasa Wamasai. Majigambo hufanyika wakati wa sherehe za harusi na za kuwapokea au kuwapongeza mashujaa. Pia, hufanyika kwenye mikutano inayoitishwa na watawala. Majigambo huambatana na ngoma na nyimbo za kusifu. Mjigambi hutokea katika kikundi kinachocheza na kujigamba. Baada ya kumaliza, mjigambi mwingine hufuata. Mara nyingi, mjigambi wa mwisho huwa yule aliyetenda jambo la kishujaa kuliko wote au yule anayeijua vizuri sana ya majigambo.

Lengo kuu la majigambo ni kujenga ari ya ushujaa, ukakamavu na ujasiri. Mtu anayefanya kitendo cha kishujaa, hushangiliwa na kupewa heshima kubwa katika jamii yake. Kwa msingi huu, vijana huhamasika kuwa wajasiri na wakakamavu ili kulinda hadhi na heshima ya jamii zao. Ijapokuwa, wajigambi wengi kwa kawaida, huonekana kuwa wanaume hasa katika ngoma za kujigamba na kwenye vikao vya pombe hata wanawake hujigamba katika miktadha tofauti ikiwamo ile ambayo inawahusisha wanawake peke yao. Mfano mzuri ni katika taarabu, hasa zile za mipasho. Kwa ujumla, majigambo hulenga kudumisha utu na heshima ya mtu katika jamii.

(a) Matambiko

Matambiko ni ibada zinazoambatana na utoaji wa sadaka kwa Mungu, miungu na mizimu. Tangu zamani, jamii mbalimbali zilifanya matambiko ili kutoa shukrani, kusifu, kuomba msamaha na kadhalika. Tambiko ni tukio halisi ambalo baadhi ya matini zinazotumika huwa na maneno ya kisanaa. Licha ya matumizi yalugha ya kisanaa kama vile tamathali za semi, taswira na lugha ya mafumbo kwa ujumla, matini za ushairi wakati mwingine husheheni nduni za ushairi ndiyo maana linaingizwa katika kundi la sanaa za maonesho. Kwa kawaida, matambiko hufanywa na watu maalumu katika jamii. Matambiko hufanyika katika maeneo maalumu. Kwa mfano, watambikaji katika baadhi ya jamii za Kanda ya Ziwa huelekeza maombi yao kwa Namhanga (Mungu Mkuu), Mugasa (mungu wa wavuvi) au Kalungu (mungu wa wawindaji). Utendaji wa tambiko hili huenda sanjari na matumizi ya maleba, vyungu na pembe maalumu. Sadaka zitolewazo na jamii ya Wakerewe hujumuisha kuku, mbuzi, kondoo, ng'ombe, vyakula vya nafaka na pombe huitwa empahe.

(b) Miviga

Miviga ni sherehe au shughuli zinazofanywa na jamii katika kipindi maalumu cha mwaka au katika muktadha maalumu. Sherehe hizo zinaweza kuwa za jando na unyago, harusi, au kutawazwa kwa Mtemi. Miviga ni sherehe zihusuzo mtu kutoka katika kundi au wadhifa fulani na kuingia katika wadhifa mwingine. Mathalani, anaweza kutoka katika rika la utoto kwenda ujana (jando na unyago) na ujana kwenda utu uzima (kuoa au kuolewa). Kadhalika, miviga ni matendo ya kimila ambayo wakati mwingine huhusisha sehemu kubwa ya jamii.

Miviga huambatana na maigizo na nyimbo zinazoendana na tukio husika. Katika harusi, nyimbo zinazoimbwa ni za ndoa; na katika mazishi nyimbo zinazoimbwa ni za maombolezo. Katika miviga, ngoma mbalimbali huchezwa. Aghalabu, wazee hutoa mafunzo na mawaidha, hususani kwa watoto na vijana.

(c) Vichekesho

Vichekesho ni aina ya sanaa ya fasihi simulizi. Katika sanaa hii, watu husimulia visa na mikasa ambavyo huwafanya wasikilizaji na watazamaji wacheke. Vichekesho vinahitaji ubunifu mkubwa ili kupata jambo litakaloibua hisia na kuvunja mbavu. Lugha inayotumika katika vichekesho ni nyepesi na iliyojaa picha ambazo watazamaji wana uwezo wa kuzitambua. Hii ni kwa sababu hutumia mifano ya vitu vinavyojulikana wazi kwa hadhira au vinavyopatikana katika mazingira yao. Aidha, vichekesho hutumia mbinu ya kejeli, dhihaka na utani.

Kama ilivyodokezwa katika maelezo ya sanaa za maonesho kwa ujumla, vichekesho ni mojawapo ya sanaa mamboleo; vichekesho vingi vimetokana na kuletwa kwa tamthiliya za kizungu zilizobeba na kuongelea utamaduni wa kimagharibi. Baadhi ziliongelea matatizo ya kijamii ya wakati wa ukoloni, mathalani suala la mgongano kati ya miji na vijiji, na uzuzu au ushamba wa Mwafrika anayetoka kijijini na kuingia mjini kwa mara ya kwanza. Maigizo hayo hayakuwa na maana kubwa kwa Waafrika zaidi ya kuwachekesha kupitia katika vitendo vilivyofanywa kwenye jukwaa. Kwa hiyo, Waafrika wakadhani kuwa jambo muhimu katika vichekesho ni kuchekesha.

Kimsingi, dhima ya vichekesho si kuchekesha tu, bali vichekesho huelimisha pia. Mifano ya vichekesho ni kama ile inayopatikana katika vipindi vinavyorushwa na vituo vya redio, mitandao ya kijamii, na runinga. Mifano ya vipindi vya kwenye runinga ni Mizengwe (ITV), Futuhi (Star TV), Vitimbi Show (Channel Ten), na Kitimtim (DSTV).

(d) Ngomezi

Hii ni sanaa ya kuwasiliana kupitia midundo ya ngoma. Baadhi ya jamii hupeana taarifa za matukio mbalimbali kupitia ngoma. Aghalabu, taarifa hizo huwa katika hali ya mafumbo, kiasi kwamba, wenyeji wa jamii husika tu huweza kubaini maana ya midundo husika. Hii yatokana na ukweli kuwa midundo katika sanaa hii hufuata kanuni maalumu zinazojulikana na wanajamii hao tu. Kanuni hizo hubebwa kupitia vipengele vya aina ya ngoma zinazotumika, muda wa kupigwa kwa ngoma pamoja na kasi au mwachano wa upigaji. Kanuni hizi huwasaidia wanajamii kupata ujumbe unaowasilishwa. Kwa mfano, katika jamii ya Wayao kuna ngoma inayojulikana kama Ngula-ntwe inayopigwa kwa ajili ya kutoa ujumbe kuhusu matukio mbalimbali ya kitanzia. Kutokana na mapigo na midundo ya ngoma, ujumbe huo huweza kufasiliwa kuwa: "Simba amevamia na kuua mifugo", "Simba amejeruhi mtu ila hajamuua", "Simba ameua mtu", au "Kesho wanaume wote wanatakiwa kwenda kwenye msako wa simba mvamizi."

(e) Utani

Ni hali ya kufanyiana mizaha au masihara baina ya watu ambapo hali hii ni tofauti na desturi za kutokuheshimiana. Wanajamii wenye uhusiano wa kutaniana, hutaniana mahali popote wakutanapo kama vile msibani, harusini, hata kwenye sehemu za kazi. Utani huweza kuwa kati ya mtu na mtu, ukoo na ukoo au kabila na kabila. Utani kati ya mtu na mtu huwa kati ya babu/bibi na wajukuu, mtu na shemeji au wifi na wifi. Kadhalika, utani kati ya kabila na kabila, aghalabu, huwa kati ya makabila yenye asili ya kuishi katika eneo moja au yaliyokuwa na maingiliano ya muda mrefu. Makabila yote ya Mkoa wa Mara, kwa mfano, ni watani wa Wanyaturu na Wanyiramba (Singida) na Wahaya (Kagera).

Utani hujenga uhusiano na ushirikiano mzuri baina ya wanajamii. Vilevile, utani hutunza historia ya jamii zinazotaniana. Aidha, utani huwafunza watoto upendo na majukumu, mathalani, utani wa mjukuu wa kike na babu anapomwita mke wake na kuomba amfanyie jukumu fulani, mtoto huyo hujifunza jukumu lake atakalolitekeleza akiwa mkubwa. Vilevile, utani hukumbusha wanajamii majukumu yao. Mathalani, katika msiba, watani hutumia tukio kukumbusha watu kujiliana hali wanapokuwa wazima na kusaidia kazi zihusuzo msiba. Kama zilivyo dhima nyingine za fasihi, utani huburudisha kwenye matukio ya furaha na huzuni. Ikumbukwe kwamba, utani unaweza kusababisha ugomvi endapo mhusika hajui kuwa anayemfanyia mzaha ni mtani wake.

(f) Maigizo

Maigizo ni sanaa inayotumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha au kutoa ujumbe fulani. Maigizo haya yanapoletwa jukwaani na kuoneshwa kwa hadhira huitwa drama. Mara nyingi, maigizo ya Kiafrika huambatana na utambaji wa hadithi, vichekesho, nyimbo, matendo ya kijadi kama vile harusi, jando na unyago. Wahusika hutakiwa kutumia lugha ya kifasihi inayoendana na hadhira. Zipo aina mbalimbali za maigizo, zikiwamo maigizo ya misibani na mivigani, maigizo ya watoto na ya burudani.

(g) Michezo ya watoto

Watoto hucheza michezo mingi yenye kuambatana na usanii. Michezo hiyo hutofautiana majina kulingana na mahali. Katika michezo hiyo, kuna kuimba, kucheza, kurukaruka, kukimbia, kughani, kujigamba na kuigiza. Baadhi ya michezo hiyo ni: kiota, ukuti, pembea (bembea), kitikiti, kibuzi na kombolela. Aghalabu, michezo hiyo huambatana na nyimbo, majibizano, vitendo na maigizo. Kwa mfano, katika mchezo wa kiota, watoto hunyanyuka pale walipoketi na kuanza kutangatanga huku na huku ilihali wakiimba mpaka kila mmoja anapopata mahali pake na kukaa. Watoto huimba hivi:

Kiota

Sisi ndege twaruka

Twatafuta kiota

Kiota

Kiota

Kiota

Ta la la la la la

Kiota

Wimbo wa mchezo huu huambatana na vitendo vya kutembea na kuzunguka. Michezo mingi ya watoto hujumuisha pamoja nyimbo na vitendo.

Maigizo ya watoto ni aina nyingine ya michezo ya watoto. Watoto huigiza michezo inayoakisi mazingira yanayowazunguka kama vile nyumbani, shuleni, shambani, hospitalini, barabarani, kanisani, msikitini na porini. Pia, watoto huigiza mambo wanayoyaona kwenye runinga, hasa watoto waishio mijini. Kwa mfano, huigiza michezo ya kivita, sherehe mbalimbali, vikundi vya nyimbo, miziki na michezo ya kuigiza.

Maigizo ya watoto, kama ilivyo kwa kazi nyingine za fasihi, yana vipengele vya fani na maudhui. Maudhui ya michezo ya watoto, kwanza, kuhusu maisha ya nyumbani kwa sababu ndiyo maisha wanayoyaona mara kwa mara. Watoto huigiza maisha ya nyumbani kwa kuakisi maisha halisi ya familia, hususani yale wanayoyaona kwenye kaya zao. Mathalani, kama baba au mama ni mkali, mtoto atakayewaigiza, ni lazima atakuwa mkali, pengine kuzidi ukali anaouona kwa wazazi wake; vivyo hivyo, kama baba au mama ni mpole na mkarimu basi muigizaji ataigiza upole na ukarimu wao. Ikiwa mzazi ni mchapakazi, basi muigizaji atakuwa na tabia hiyo. Kama ni nadhifu, mwigizaji naye atajitahidi kuwa nadhifu. Kwa hiyo watoto waigizao nafasi ya wazazi wao, huakisi tabia ya wazazi hao.

Kwa kawaida, hakuna matini inayokuwa imeandaliwa kabla ya mchezo, bali maigizo ya watoto hubuniwa papo kwa papo. Watoto wanapokutana hukubaliana aina ya mchezo na kugawana majukumu ya kila mhusika; wakati mwingine, watoto wenyewe huchagua nafasi watakazoigiza. Uigizaji wa michezo ya watoto huambatana na ubunifu ambapo kila mtoto (mhusika) hubuni uigizaji wa uhusika wake. Katika maigizo yanayohusisha wanyama, kwa mfano, kama igizo lina mhusika simba, mtoto anayeigiza kama simba ni lazima awe na sifa za ubabe, sauti nzito na nguvu. Halikadhalika, atakayeigiza kama jogoo, awe na sauti kali ili atakapowika asikike.

Aidha, watoto huchagua nafasi kulingana na uwezo wao na jinsi jamii ilivyoainisha majukumu mbalimbali kama ya udaktari, ualimu, uaskari na mengineyo. Kwa hiyo, watoto huchagua nafasi za kuigiza kutokana na kazi wanazipendazo. Wakati mwingine kupitia michezo hii, ndoto za watoto huchomoza na watoto wengine huanza kuishi na ndoto zao.

Baadhi ya sifa za maigizo ya watoto ni kuwa na muundo wa moja kwa moja na kutohitaji maleba mahususi.

Shughuli ya 2.7 Tumia vyanzo mbalimbali kuchunguza michezo mitatu ya watoto, kisha bainisha mbinu za kisanaa zilizotumika katika utunzi wa michezo hiyo.
Shughuli ya 2.8 Kwa kutumia vyanzo vya mtandaoni na maktabani eleza sifa za fasihi andishi na tanzu zake.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

1. Kwa kutumia mifano fasili dhana zifuatazo:(a) hurafa(b) soga(c) lakabu(d) istiara(e) visasuli(f) hekaya(g) ngomezi

2. Kwa kutumia mifano, eleza tofauti kati ya ngano na vigano.

3. Kwa kutumia mifano anuwai, tofautisha vichekesho na maigizo.

4. Jadili athari za utani unaofanyika katika jamii yako.

5. "Si kila mchezo wa watoto ni fasihi simulizi." Jadili kauli hii kwa hoja maridhawa.

6. Kwa kutumia mifano, tofautisha dhana zifuatazo:(a) tendi na tenzi(b) maghani na nyimbo(c) visasili na visakale(d) vitendawili na mizungu(e) visasili na visasuli

7. Chambua mbinu za kisanaa zinazojitokeza katika ngano, visasili, na soga.

8. Sikiliza ngano mbili kutoka kwa wenzako kisha andika insha fupi kueleza mafunzo yaliyomo katika ngano hizo.

Tanzu na vipera vya fasihi andishi

Kama ilivyo kwa fasihi simulizi, fasihi andishi pia ina tanzu zake. Kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama vile Wamitila (2002) na Mulokozi (2017) kuna tanzu nne za fasihi andishi ambazo ni ushairi, hadithi fupi, tamthiliya na riwaya. Kadhalika, tanzu hizo zimegawanyika katika vipera. Tazama Kielelezo namba 2.2.

Fasihi Andishi

Kielelezo namba 2.2: Tanzu za fasihi andishi

Shughuli ya 2.9Kwa kutumia vyanzo vya maktabani au vinginevyo, jadili dhana na chimbuko la ushairi wa Kiswahili.

UshairiMulokozi (2017) anaueleza ushairi kuwa ni “sanaa ya lugha ya mkato yenye ubunaji inayosawiri au kueleza jambo, hisi, hali au maono kwa namna yenye kuvutia hisia na katika mpangilio wa maneno wenye urari na wizani.” Inamaanisha kuwa ushairi husawiri mawazo, hisi au tukio kwa muhtasari katika mpangilio maalumu wa lugha teule ya kitamathali. Kwa hiyo, ushairi hutofautiana na tanzu nyingine za fasihi andishi katika umbo na matumizi ya lugha. Tanzu nyingine hutumia lugha ya mjazo ya kinathari lakini ushairi hutumia lugha ya mkato, yenyekueleza maudhui yake kimuhtasari; na aghalabu, huyaficha maudhui hayo ndani ya taswira na ishara. Kama ilivyo kwa ushairi simulizi kwamba ndio utanzu wa kwanza kabisa wa fasihi simulizi, ushairi andishi nao ulikuwa utanzu wa kwanza wa fasihi andishi.

Historia fupi ya ushairi wa Kiswahili

Tarehe mahususi za kuanza kwa ushairi wa Kiswahili, hususani umbo la ushairi linalonekana leo, ni za kukisia. Kilicho bayana ni kwamba, kabla ya karne ya 10 ushairi wa Waswahili ulikuwa ukitungwa na kughaniwa kwa ghibu bila kuandikwa. Hali ilibadilika kuanzia karne ya 10 wakati Uislamu ulipoanza kuenea Uswahilini; na hivyo, kueneza hati ya Kiarabu. Kuanzia wakati huo, baadhi ya Waswahili walianza kutunga na kuandika mashairi, hasa tenzi na tendi, kwa kutumia hati hiyo.

Wataalamu hugawa maendeleo ya ushairi wa Kiswahili katika mihula mbalimbali. Kwa mfano, Kezilahabi (1983) anabainisha mihula minne ambayo ni: muhula wa urasimi, muhula wa utasa, muhula wa urasimi mpya, na muhula wa sasa.

Muhula wa Urasimi ni kipindi maalumu kinachochukuliwa kuwa msingi wa kuwekwa kwa sheria au kanuni za jambo fulani. Urasimi wa ushairi wa Kiswahili ulipata mashiko katika karne ya kumi na nane (1700-1800). Katika kipindi hicho, kulikuwa na tungo kama vile Utenzi wa Hamziyya (bin Uthman, 1690), Utenzi wa Tambuka (Bwana Mwengo, 1728), Utenzi wa Al-Inkishafi (bin Nasir, 1800) na Utenzi wa Mwanakupona (Mwanakupona bint Mshamu, 1858). Tungo hizi zilitanguliwa na tungo zilizohusu simulizi za Fumo Liyongo na zikafuatiwa na tungo za Muyaka bin Haji. Baada ya hapo, ulifuatia ukame wa tungo kwa kipindi cha takribani miongo mitano (1885 - 1945). Kulikuwa na tungo chache; ndiyo maana muhula wa pili unaitwa muhula wa utasa. Sababu za ukame huu ni pamoja na matukio ya vita yaliyotokea ulimwenguni. Baada ya hapo, ukafuatia muhula wa urasimi mpya ambapo kulikuwa na watunzi kama vile Shaaban Robert, Kaluta Amri Abedi na Mathias Mnyampala. Huu ni muhula ulioshuhudia kuimarishwa kwa kanuni za utungaji wa ushairi wa Kiswahili kama vile Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri (Abedi, 1954). Kisha, ulifuatia muhula wa sasa. Muhula huu ulianza wakati mataifa ya Afrika Mashariki yalipopata uhuru kutoka kwa wakoloni. Hiki ni kipindi kilichokuwa na wasomi wengi wa ngazi ya chuo kikuu waliojihusisha na utungaji, uhakiki na utafiti kuhusu masuala ya fasihi, ukiwamo ushairi. Hali hii mpya ilisababisha kuwapo kwa fikra mpya katika ushairi wa Kiswahili; ndipo ulipoibuka mjadala kuhusu ushairi usiofuata urari wa vina na mizani. Mjadala huo hujulikana kama Mgogoro wa Ushairi ambao umeelezwa kwa urefu katika kitabu cha Mulokozi na Kahigi (1982).

Vipera vya ushairi andishi

Ushairi andishi umegawanyika katika vipera vitatu. Vipera hivyo ni mashairi, tenzi na ushairi wa maigizo.

(a) Mashairi

Kuna mitazamo miwili inayohusu mashairi: mtazamo wa kimapokeo na mtazamo wa kisasa.

Mtazamo wa kimapokeo

Huu ndio mtazamo wa awali kuhusu mashairi ya Kiswahili. Wafuasi wa mtazamo huu wanasisitiza mambo yafuatazo: kanuni za urari wa vina na mizani, na lugha nzito ya mkato. Urari wa vina na mizani hulifanya shairi liimbike kwa urahisi kwa mahadhi yanayofahamika. Tazama mfano wa beti zifuatazo:

Maisha

Maisha kitendawili, kitegue kwa busara,

Uitulize akili, huku ukiwa tohara,

Uhimili kila hali, yaweza kwako kung'ara,

Tukiimudu subira, maisha hayatuwengi.

Maisha kama bahari, yenda mpera mpera,

Vyovyote uwe tayari, kwa kujiweka imara,

Na kumuomba Kahari, akunyooshee dira,

Tukiimudu subira, maisha hayatuwengi.

Maisha ni kujituma, ili uipate tira,

Ushughulike kulima, au kuunda minara,

Mwiko kujiweka nyuma, utakumbwa na idhara,

Tukiimudu subira, maisha hayatuwengi.

Diwani ya Tunzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein (Juma (Mwana wa Nyasa), 2016).

Shairi hili lina mizani linganifu. Kila mshororo una mizani kumi na sita na vina vinavyofanana mwishoni mwa kila mshororo kwa shairi zima. Vina vya kati vinafanana katika kila ubeti. Kila ubeti umeundwa na mistari minne, ambapo huu ni muundo wa tarbia.

Mtazamo wa kisasa au masivina

Huu ni mtazamo wa wanamabadiliko wanaodai kwamba si lazima shairi liwe na urari wa vina wala ulinganifu wa mizani. Mtazamo huu ulianza mwishoni mwa miaka ya 1960 na kushadidijwa mwanzoni mwa miaka ya 1970. Wafuasi wa mtazamo huu ni Ebrahim Hussein, Euphrase Kezilahabi na Jared Angira. Wafuasi wengine ni Mugyabuso Mulokozi, Kulikoyela Kahigi, Said Ahmed Mohamed na Theobald Mvungi. Kulikoyela Kahigi na Mugyabuso Mulokozi wameandika Mashairi ya Kisasa (1973), Malenga wa Bara (1976) na Kunga za Ushairi na Diwani Yetu (1982), Said Ahmed Mohamed ameandika diwani kadhaa zikiwamo 'Sikate Tamaa (1983) na Kina cha Maisha (1984).

Wafuasi wa mtazamo huu wanaamini kuwa maudhui yanaweza kuwasilishwa bila kujikita katika sheria za vina na mizani. Wanadai kuwa, kama ambavyo mabadiliko yanatokea katika nyanja nyingine, ni lazima pia yatokee katika ushairi. Ikumbukwe kwamba, wenye mtazamo huu hawapingi kanuni za wanamapokeo, ila wamepanua wigo wa mashairi. Kwa mfano, zaidi ya nusu ya mashairi yaliyomo katika Diwani ya Malenga wa Bara (Kahigi na Mulokozi, 1976) ni ya kimapokeo. Wanausasa wanatilia mkazo matumizi ya lugha kuliko muundo wa shairi. Tazama mfano wa shairi la kisasa la “Kuchambua Mchele”:

Habari zilifika kutoka Arusha,

Tukaanza kuchambua mchele wa Ujamaa,

Macho mbele, macho pembeni tukitoa mchanga,

Tukafanya kaburi dogo la mchanga.

Tukaanza kutoa chenga, moja moja,

Vidole vikafanya kazi kama cherehani,

Usiku na mchana; macho yakauma,

Tukafanya kichuguu kidogo cheupe.

Kichomi (Kezilahabi, 1988)

Ukichunguza beti hizi mbili, utaona kwamba hakuna mizani linganifu wala urari wa vina. Kilichozingatiwa ni uteuzi wa maneno wenye kujenga picha na kumvutia msomaji au msikilizaji.

Wanausasa wanasisitiza mshairi awe na uhuru katika kutunga mashairi, na kueleza mawazo yake bila kubanwa na kanuni za wanamapokeo. Kitu cha msingi katika shairi ni mpangilio wa maneno, lugha ya picha au taswira, tamathali za semi, hisia za kishairi na ujumbe.

(b) Tenzi

Dhana ya tenzi imekwishaelezwa katika kipengele cha fasihi simulizi. Mambo machache ya kuyaongezea katika kipengele hiki ni kwamba, mara nyingi, tenzi huanza na dua, ambapo mwandishi humwomba Mungu amwongoze katika uandishi wake. Kwa kawaida, tenzi huwa na beti nyingi kuliko shairi la kawaida, lakini tenzi nyingi ni fupi kuliko tendi.

Beti za utenzi zinatakiwa ziwe hamsini na kuendelea. Hata hivyo, urefu wa utenzi hutegemea uzito wa maudhui na ujuzi wa mwandishi. Aghalabu, mstari wa utenzi huwa nusu ya mshororo wa shairi la kimapokeo. Hivyo, utenzi huwa na mizani minane. Vilevile, vina katika mishororo mitatu ya kwanza, hufanana lakini mshororo wa mwisho huwa na kina tofauti. Kina hiki ambacho huitwa bahari hakibadiliki katika utenzi mzima. Tazama mfano katika baadhi ya beti za utenzi ufuatao:

Utenzi wa hati

1. Leo nataka binti,

Ukae juu ya kiti,

Ili uandike hati,

Ndogo ya wasia.

2. Mimi kwako ni baba,

Hati hii ya huba,

Andika iwe akiba,

Asaa itakufaa.

3. Bado ungali kijana,

Na dunia ngumu sana,

Kukufunza kukuona,

Ni jambo welekea.

Maisha Yangu na Baada ya miaka Hamsini (Robert, 1966: 6)

Beti za hapo juu zinaonekana wazi kuwa zimeundwa na mishororo minne. Kina cha mshororo wa mwisho "a" ni tofauti na vina vya mishororo mingine mitatu katika beti zote.

Ushairi wa maigizo

Huu ni utanzu mmojawapo wa ushairi wa Kiswahili. Utanzu huu tunaweza kuuweka katika michepuo miwili ambayo ni ngonjera na ushairi wa kidrama.

(i) Ngonjera

Ngonjera ni aina ya ushairi andishi ambao huhusisha mabishano ya pande mbili. Upande unaojua na ule usiojua jambo fulani. Kwa hiyo ushairi wa ngonjera huandikwa kidayalojia ukihusisha pande mbili. Lengo kuu ni kuonesha udhaifu wa hoja kinzani kwa kuzikosoa hoja hizo ili, hatimaye, hoja zilizolengwa zionekane kuwa na ushawishi mkubwa. Tazama mfano ufuatao wa ushairi wa beti chache za ngonjera:

Ngonjera ni kitu gani?

MDADISI

Ngonjera ni kitu gani, nasikia kila mara,

Yatamkwa midomoni, tena mbele ya hadhara,

Je, maana yake nini, nami nipate busara,

Maana yake ngonjera, nambie nami nijue.

JAWABU

Ngonjera zina kiini, cha mafunzo ya busara,

Mafunzo yenye kipini, cha kuamsha fikira,

Za mawazo akilini, na kugeuza majira,

Maana yake ngonjera, ni mafunzo kwa shairi.

MDADISI

Ni mafunzo yapi hayo, ya hekima na ubora?

Yatiayo wangu moyo, kwa jitihada na ghera,

Ufanisi yaletayo, ya kugeuza majira,

Maana yake ngonjera, nambie nami nijue.

JAWABU

Mafunzo yatolewayo, kwa USEMI wa hadhara,

Mema yachangamshayo, kwa tabasamu ya sura,

Ni ghibu itumikayo, kwa fikira na busara,

Maana yake ngonjera, ni mafunzo kwa shairi.

Ngonjera za Ukuta: Kitabu cha Kwanza (Mnyampala, 1970:5)

(iii) Ushairi wa kidrama

Huu ni ushairi unaotumiwa katika baadhi ya tamthiliya kama mtindo mmojawapo wa kuandika mazungumzo ya wahusika. Hivyo, hauwezi kutenganishwa na fani ya tamthiliya (Mulokozi, 2017). Ufuatao ni mfano wa ushairi huu:

Mwanamke

Ndugu zangu, pulikeni ndugu zangu

Sasa si kama zamani

Sasa umetawala uwazi

Uwazi na utambuzi

Tusipigwe na bumbuwazi

Tusijisabilie kirahisi

Kwa ndoa yenye wasiwasi!

Mume mwenyewe kumwakisi

Bali hukufanya kisisi

Ukanipa mchumba mwenye ukakasi...

Mfalme:Mwenzako lakini kakukosa nini?

Mwenzako kakufanya nini?

Mimi bado sijaamini

Kwa kweli baya mimi sijalibaini

Basi jambo hilo lanikata maini

Na kunivunjia matumaini

Mbona unaivunja ihsani

Yake sisi tul'omwamini

OPosa za Bikisiwa (Mohamed, 2013)

Kwa jumla, kuna sifa mbalimbali za kisanaa zinazoutofautisha ushairi na tanzu nyingine za riwaya pamoja na tamthiliya.

Zoezi la 2.2

1. Soma kauli hizi mbili kisha jibu maswali (a) na (b) yanayofuata:

(a) "Katika kitabu hiki, tungo za Euphrase Kezilahabi, Kulikoyela Kahigi, Mulokozi na wengineo watungao tungo tutumbi zisizokuwa na samaa yoyote nimezitupa pembeni ... Muundo wa mashairi yote yaliyomo kitabuni humu ni ya asili ya KiBantu. Kila utungo wa shairi umefungika upande wa mistari; umefungika upande wa vina; ni lazima mistari iwe na vina; umefungika upande wa mizani; ni lazima kila mstari uwe na idadi sawa ya mizani. Mashairi yote yaimbwe; yaweza pia kusomwa au kusemwa tu. Tungo zisizotimiza yote hayo si mashairi."

Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka (Mayoka, 1986)

(b) Washairi wa mapokeo, sasa wacheza lala salama,

Katika mionzi hafifu, ya jua machweoni,

Na mahadhi yagaagaa, juu ya bahari ya utenzi,

Yameshindwa chini kuzama, kwenye kina cha urazini,

Nao wahenga vibandani, nje tena hawatoki,

Hakuna tena ngoma, ya kugeana kani,

Na ushairi umehama, umerudi upeponi,

Lakini majani makavu, sasa hayatingishiki,

Nayo madirisha ya nyumba, imara yamefungwa,

Waliomo ndani wahofu, hasira ya mizimu.

Kichomi (Kezilahabi, 1988)

(i) Toa maoni yako kuhusu hoja ya kuwa ili utungo uitwe shairi, sharti ukidhi vigezo vya kauli 1(a)

(ii) Tathmini ukweli wa kinachosemwa katika kauli (b) ukihusianisha na hali halisi ya sasa ya ushairi wa Kiswahili.

2. Soma shairi la kisasa, kisha bainisha vipengele mbalimbali vya ushairi.

3. Soma beti ishirini (20) za utenzi uupendao kisha chambua vipengele vya fani na maudhui.

4. Soma shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Amina

1. Amina umejitenga, kufa umetangulia,

Kama ua umefunga, baada ya kuchanua,

Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa,

Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua.

2. Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua,

Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua,

Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua,

Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua.

3. Majonzi hayanenek, kila nikikumbukia,

 Nawaza kile na hiki, naona kama ruia, 

Mauti sijasadi, kuwa mwisho wa dunia,

Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua.

Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (Robert, 2003:5)

Maswali(a) Andika ujumbe wa shairi.(b) Bainisha mloto wa ubeti wa pili.(c) Bainisha vina vya kati na vya mwisho vya ubeti wa pili.(d) Orodhesha utao wa ubeti wa kwanza na ukwapi wa ubeti wa tatu.(e) Orodhesha mizani ya uketo wa kibwagizo cha shairi hili.

Shughuli ya 2.10

Kwa kutumia vyanzo vya mtandaoni na maktabani, jadili dhana na historia ya hadithi fupi ya Kiswahili.

Hadithi fupiHadithi fupi ni simulizi za kubuni zinazosawiri tukio, tabia, mgogoro au kipengele cha maisha kwa ufupi. Hadithi za namna hii huwa na tukio moja au mawili na hutumia mawanda finyu. Kwa kawaida, hadithi fupi haina uchangamano mkubwa wa matukio, na hutumia wahusika wachache.

Historia ya hadithi fupiChimbuko la utanzu wa hadithi fupi ni hadithi simulizi na andishi zinazopatikana katika lugha nyingi duniani. Baadhi ya fani zilizochangia kuchipuka kwa hadithi fupi ni ngano, hekaya, visa, michapo na tendi. Kuzuka kwa fani ya hadithi fupi huko Marekani na Ulaya katika karne ya 19 kulisaidiwa sana na kuchipuka kwa utamaduni wa kusoma magazeti, kwani visa vingi vilichapishwa katika magazeti hayo. Uhusiano huu kati ya hadithi fupi na magazeti au majarida bado upo hadi leo.

Historia ya hadithi fupi haitofautiani sana na historia ya riwaya ya Kiswahili. Visa vya mwanzo vilivyochapishwa kwa Kiswahili ni mkusanyiko wa hekaya na ngano. Baadhi ya hadithi hizo ni zile zinazopatikana katika vitabu vifuatavyo:

Swahili Tales as Told by the Natives of Zanzibar (1870), Hekaya za Abunuwasi (1928) na Alfu Lela Ulela (1928). Hadithi hizi zilikuwa za kimapokeo na zenye kuingiliana na fasihi simulizi. Visa halisi vya kwanza katika hadithi za lugha ya Kiswahili vilianza miaka ya 1950 katika magazeti ya Mambo Leo, Mwafrika, Baraza, Nyota Afrika na Kiongozi. Katika miaka ya 1960, visa hivi vilianza kuchapishwa kwenye vitabu. Baadhi ya waandishi mashuhuri wa hadithi fupi za Kiswahili ni Gabriel Ruhumbika, Alex Banzi, Joseph Kiimbila, Kyallo Wadiitila na Owen Onyango. Baadhi ya mikusanyiko ya hadithi fupi iliyochapishwa ni Misingi ya Hadithi Fupi (Msokile, 1992), Mwendawazimu na Hadithi Nyingine (Mbatiiah, 2000), Mimba Ingali Mimba na Hadithi Nyingine, (MacOnyango, 2006), Mizungu ya Manabii na Hadithi nyingine (Habwe, 2010), Shingo ya Mbunge na Hadithi Nyingine (Wamitila, 2010)

Sifa za hadithi fupi

Hadithi fupi huwa na sifa au kaida zinazoitofautisha na riwaya. Nazo ni kuwa na:

  1. urefu wa kusomeka kwa mkao mmoja. Kwa kawaida hadithi fupi haizidi maneno 10,000;
  2. muundo sahili;
  3. wahusika wachache ambapo, aghalabu, mhusika mkuu huwa mmoja au wawili. Wahusika hawa hawakui kitabia wala hawakui kulingana na maendeleo ya kisa;
  4. dhamira chache ikilinganishwa na riwaya. Mara nyingi, huwa na dhamira kuu moja katika kisa kikuu kimoja; na
  5. mawanda finyu ya kiwakati na kijiografia.

Aina za hadithi fupi

Hadithi fupi huainishwa katika makundi mawili: hadithi fupi dhati na hadithi fupi pendwa. Hadithi fupi dhati huwekwa katika makundi yafuatayo: hadithi fupi za kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kifalsafa.

Hadithi fupi za kijamii huzungumzia masuala mbalimbali ya kijamii kama vile ndoa, jinsia, mapenzi na malezi. Mifano ya hadithi fupi za kijamii ni: "Uwike Usiwike Kutakucha" (Ruhumbika), na "Siri ya Bwanyenye" (Mulokozi) zote hizi zimo katika Msokile (1992). Nyingine ni "Damu Nyeusi" (Walibora, 2007) na "Kijana Yule" (Mohamed, 2010).

Hadithi fupi za kisiasa ni zile zinazohusu masuala ya kisiasa. Mifano ya hadithi hizo ni "Wali wa Ndevu" (Ruhumbika, 1974), "Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani", "Magwanda Kubilya na Vyama Vingi" na "Mayai Waziri wa Maradhi" (Kezilahabi katika Msokile, 1992).

Hadithi fupi za kiutamaduni zinahusu masuala ya mila na desturi. Mifano ya hadithi fupi za kundi hili ni Tamaa Mbele (Banzi, 1970) na "Siku ya Mganga" (Mpilipili, katika Wamitila, 2012).

Hadithi fupi za kifalsafa huzungumzia tafakuri kuhusu masuala mazito yanayomzunguka mwanadamu na ulimwengu wake. Mifano ya hadithi fupi za kifalsafa ni "Wasubiri Kifo" (Kezilahabi, katika Msokile, 1992) na "Mchakamchaka wa Maisha" (katika Komba, 1978).

Hadithi fupi pendwa ni zile ambazo huzungumzia masuala yanayosisimua kama vile mapenzi, matukio yenye ujabu ajabu, mauaji na upelelezi. Mifano ya hadithi hizo ni "Sadiki Ukipenda" (Mohamed, 2002)

Pamoja na uainishaji wa hadithi fupi uliofanywa hapo juu, ni vigumu kuwa na hadithi fupi yenye maudhui ya mwelekeo mmoja. Hivyo, hadithi fupi moja inaweza kubeba maudhui ya aina mbalimbali.

Shughuli ya 2.11 

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, soma hadithi fupi zisizopungua nne (4) kisha, bainisha aina zake na chambua maudhui ya hadithi hizo.

Shughuli ya 2.12 

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, fafanua dhana na historia ya tamthiliya.

Tamthiliya 

Tamthiliya ni mchezo ulioandikwa ili utendwe jukwaani au usomwe, kwa malengo mbalimbali. Tamthiliya hujengwa na wahusika na migogoro iliyomo katika mchezo. Migogoro ndiyo hukuza mwendo wa tamthiliya kwa kutumia visa ambavyo hutendwa na wahusika mbalimbali. Wahusika huzungumza na kutenda matendo mbalimbali kisanii.

Historia ya tamthiliya 

Tamthiliya haikuwapo nchini Tanzania kabla ya ujio wa Waingereza. Ujio wao ulileta drama ambayo ndiyo chanzo cha tamthiliya. Drama iliingizwa shuleni na Waingereza kwa lengo la kuwaburudisha na kuwakumbusha utamaduni wao, hasa baada ya saa za kazi ambapo wengi wa walimu walikuwa Waingereza. Ilikuwa rahisi kuanzisha vikundi vya drama shuleni kwa sababu shule nyingi zilikuwa za bweni; na hivyo, wanafunzi walipatikana muda wote. Vilevile, wanafunzi hao walifahamu vizuri lugha ya Kiingereza. Tamthiliya nyingi zilizoigizwa ni zile zilizoandikwa na Waingereza. Miongoni mwa tamthiliya hizo ni The Merchant of Venice (Shakespeare, 1596) na Julius Caesar (Shakespeare, 1599). (Kwa kuwa tamthiliya hizi hazikuwa na uhusiano na mazingira ya Kitanzania, Watanzania walioigiza waliona ni kiburudisho tu yaani tamthiliya hizo hazikuwa na maana kubwa kwao. Kadiri muda ulivyopita, baadhi ya Watanzania walivutiwa na sanaa ya tamthiliya. Hata hivyo, hawakuwa na ujuzi wa kuandika tamthiliya kama zile za Waingereza. Miaka ya mwanzo baada ya uhuru, maudhui hayakubadilika mpaka lilipotangazwa Azimio la Arusha mwaka 1967. Maudhui ya tamthiliya ya baada ya Azimio la Arusha yalichukua sura mpya kwa kutangaza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kuunga mkono au kukosoa.

Tamthiliya za mwanzo ziliathiriwa sana na vichekesho. Pia, ziliathiriwa na tamthiliya za Kiingereza. Watunzi walitunga tamthiliya zilizofanana kimaudhui na zile za akina Shakespeare. Kwa mujibu wa Mazrui (2007) na Mulokozi (2017), tamthiliya za mwanzo za Kiswahili zilitungwa nchini Kenya. Mifano ya tamthiliya hizo ni Mgeni Karibu (Hyslop, 1957), Nakupenda Lakini (Kuria, 1957) na Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi (Ngugi, 1961). Kwa upande wa Tanzania, miaka ya 1960, tamthiliya za Kiingereza zilitafsiriwa. Miongoni mwa tamthiliya hizo ni zile za Shakespeare za Juliasi Kaisari (Nyerere, 1964), Mabepari wa Venisi (Nyerere, 1969), Tufani (Mushi, 1969) na tamthiliya ya Kiyunani ya Mfalme Edipode (Mushi, 1969). Tamthiliya nyingine ni zile zilizoandikwa na Waafrika. Zilizotafsiriwa ni Mtawa Mweusi (wa Thiong'o, 1970), Masaibu ya Ndugu Jero (Yahaya, 1974) na Nitaolewa Nikipenda (wa Thiong'o na wa Mirii, 1982).

Kuanzia miaka ya 1960, watunzi wa Kitanzania walianza kutunga tamthiliya za Kiswahili kwa ajili ya Watanzania. Miongoni mwa watunzi waliojitokeza ni Ebrahim Hussein ambaye tamthiliya yake ya kwanza ni, Wakati Ukuta (1967), ilishinda na kupata tuzo katika mashindano. Tamthiliya nyingi zilizotungwa miaka ya 1960 ziliigizwa tu shuleni na katika kumbi za maonesho lakini hazikuchapishwa.

Tamthiliya nyingi za Kiswahili zilichapishwa kama matokeo ya kuhitimu kwa watu wengi katika fani ya sanaa za maonesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia, yalikuwa ni matokeo ya kuanzishwa kwa mashindano ya uigizaji miaka ya 1970 - 1990. Baadhi ya tamthiliya zilizochapishwa ni Kinjeketile (Hussein,1969), Mashetani (Hussein, 1971), Hatia (Muhando, 1972), Tambueni Haki Zetu (Muhando, 1973), Aliyeonja Pepo (Topan, 1973) na Pambo (Muhando, 1975). Nyingine ni Sundiata (Mbogo, 1975), Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi (Hussein, 1976), Machozi ya Mwanamke (Ngozi, 1977), Mukwawa wa Uhehe (Mulokozi, 1979), Arusi (Hussein, 1980), Tendehogo (Semzaba, 1984), na Giza Limeingia (Mbogo, 1980). Vilevile, kulikuwa na Njia Panda (Muhanika, 1981), Tone la Mwisho (Mbogo, 1981), Nguzo Mama (Muhando, 1982), Lina Ubani (Muhando, 1984), Kwenye Ukingo wa Thim (Hussein, 1988), Pungwa (Mohamed 1988), Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe (Semzaba, 1988) Kivuli Kinaishi (Mohamed 1990), na Morani (Mbogo, 1993).

Tamthiliya zimeendelea kutungwa zikiakisi mabadiliko ya mifumo ya maisha ya jamii ya wakati huo. Mathalani, tamthiliya kama Ushuhuda wa Mifupa (Ngozi, 1990) na Kilio Chetu (Medical Aid Foundation, 1995) zimejadili kuhusu maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI katika jamii.

Miaka ya karibuni, tamthiliya ya kihistoria imeanza kushamiri tena baada ya kupotea kwa takribani miongo mitatu tangu enzi za Kinjeketile na Mukwawa wa Uhehe. Mtunzi aliyejipambanua zaidi katika mkondo huu ni Emmanuel Mbogo ambaye ametoa tamthiliya nne katika miaka ya karibuni. Tamthiliya hizi zinaongeza idadi ya tamthiliya zake nyingine mbili za kihistoria alizozichapisha hapo kabla. Nazo ni Ngoma ya Ng'wanamalundi (1988), Sundiata (1994), Fumo Lyongo (2009), Sadaka ya John Okello (2015), Nyerere na Safari ya Kanaani (2015), Malkia Bibi Titi Mohamed (2016) na Shujaa Mirambo (2021). Tamthiliya hizo, mbali na kupevua mkondo wa tamthiliya ya kihistoria, zinadhahirisha namna historia ilivyoweza kutumika kisanaa kusawiri migogoro na masuala yenye umuhimu katika jamii ya leo.

Aina za tamthiliya

Tunaweza kuainisha tamthiliya kwa kutumia vigezo mbalimbali kama vile kigezo cha maudhui, kusudio, dhima, muktadha wa utendaji, hadhira lengwa na mbinu za kisanii. Kila kigezo hutupatia aina mahususi za tamthiliya. Mathalani, kigezo cha hadhira lengwa kinapotumika, huweza kutupatia aina zifuatazo: tamthiliya ya watoto, tamthiliya ya vijana, tamthiliya ya watu wazima, tamthiliya ya wanawake, tamthiliya ya wanaume, tamthiliya ya miungu na tamthiliya ya waumini wa dini fulani. Uainishaji uliotumika katika kitabu hiki umetumia kigezo cha mbinu za kisanaa. Kwa kuzingatia kigezo hicho, tunapata aina zifuatazo: tanzia, ramsa, tanzia ramsa, na melodrama.

(a) Tanzia

Tanzia ni tamthiliya yenye tukio au matukio ya kuhuzunisha; nayo huhusika na mambo yenye uzito kifikra na kihisia, katika maisha ya binadamu. Mhusika mkuu ambaye kwa kawaida ni mtu maarufu mwenye kupewa sifa nyingi zinazovutia, hukabiliwa na shida au tatizo. Tatizo hilo ni kama lile linaloweza kumkabili mtu yeyote. Ijapokuwa mhusika huyo hujitahidi kulitatua tatizo hilo, hali ya ulimwenguni na tabia ya kibinadamu humfanya asiweze kufaulu, na mwishowe hushindwa. Kwa hiyo, mwisho wa tamthiliya hizi ni masikitiko, maanguko na hasara kwa mhusika mkuu au jamii. Mfano wa tanzia ni tamthiliya ya Kinjeketile (Hussein, 1969) na Kifo Kisimani (wa Mberia, 2001).

(b) Ramsa

Ramsa, ambayo hujulikana pia kama komedia au futuhi, hukusudia kufurahisha au kuchekesha, na huwa na mwisho mwema. Sifa ya kufurahisha na kuchekesha haimaanishi kwamba tamthiliya za aina hii hazina maudhui mazito. Tamthiliya hizi hushughulikia masuala mbalimbali ya msingi kama vile uzembe, uzalishaji mali, siasa, mapenzi na ndoa. Utani, mzaha na kejeli hutumika katika kuchekesha. Kupitia uchekeshaji huo, jamii, watawala na watu binafsi hukosolewa. Mhusika mkuu wa ramsa si lazima awe mtu maarufu. Anaweza kuwa mtu wa kawaida au anaweza kuwa mtu wa nasaba duni, lakini hubeba matendo ya ucheshi yanayobeba maana nzito. Mhusika huyu akifanikiwa, wasomaji au watazamaji hufurahi. Mfano mzuri wa ramsa ni tamthiliya ya Mfalme Juha (Topan, 1971) na Aliyeonja Pepo (Topan, 1973).

(c) Tanzia ramsa

Hii ni tamthiliya yenye mseto wa maudhui ya kuhuzunisha na kufurahisha. Mifano ya tamthiliya hizi ni Kaptula la Marx (Kezilahabi, 1999), Pambo (Muhando, 1975), Masaibu ya Ndugu Jero (Soyinka, [mf.] Yahaya, 1974), Mabepari wa Venisi (Shakespeare [mf.] Nyerere, 1969), Wakati Ukuta (Hussein, 1967) na Amezidi (Mohamed, 1995).

(d) Melodrama

Melodrama ni tamthiliya yenye matumizi mengi ya muziki na uimbaji wa nyimbo. Inafanana sana na tanzia ingawa, mara nyingi, nguli wa melodrama huibuka na ushindi. Dhamira za melodrama huzungumzia mvutano kati ya wema na uovu au ubaya. Matukio yake husisimua sana na mwendo wa msuko wake huwa wa harakaharaka. Wahusika wake huvutia lakini hawana sifa za kishujaa. Aghalabu, mwishoni, mhusika mwema huweza kupata ushindi.

Tofauti baina ya michezo ya fasihi simulizi na tamthiliya za fasihi andishi

Michezo ya fasihi simulizi hutofautiana na tamthiliya za fasihi andishi kwa vipengele vifuatavyo:

(a) Utunzi wa maonesho

Mara nyingi mtungaji wa mchezo na mwigizaji wa tamthiliya huwa tofauti. Maneno ya mtunzi ni lazima yakaririwe na waigizaji jinsi yalivyo au kama madokezo ya lazima. Kwa upande wa fasihi simulizi, mara kadhaa watunzi wa mchezo ndio wachezaji. Maneno na vitendo ni vyao wenyewe na wakati mwingine hubuniwa papo kwa papo.

(b) Maandalizi

Tamthiliya hupitia maandalizi kadhaa kama vile kufanya mazoezi mengi kabla ya kuigizwa jukwaani. Pia, jukwaa na vyombo vitakavyotumika sharti viandaliwe mapema. Kwa ujumla, igizo lolote ili livutie watazamaji linapaswa kufanyiwa maandalizi mazuri. Kwa upande wa maandalizi drama zinazotokana na vitabu na zile zinazotungwa tu kichwani lazima ziandaliwe vizuri.

(c) Shabaha

Shabaha kuu katika drama na maigizo ya kawaida ni meulimisha, kuburudisha na wakati mwingine ni biashara kwa sababu watu hununua tamthiliya au huuaza kazi hizo katika vituo vya runinga na redio. Vilevile, maigizo huoneshwa ukumbini ambapo watazamaji hupaswa kulipia.

Shughuli 2.13

Kwa kutumia vyanzo vya maktabani, soma tamthiliya mbili au zaidi, kisha bainisha aina ya tamthiliya hizo.

Shughuli 2.14

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, jadili dhana na aina za riwaya.

Riwaya

Riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni itumiayo lugha ya kinathari (lugha ya mjazo) yenye uchangamani wa visa, wahusika, mandhari na dhamira. Mara nyingi vipengele hivyo huakisi maisha ya jamii inayohusika. Hivyo, riwaya huweza kutoa picha ya jumla ya maisha ya mtu kutoka nyumbani (mtu binafsi) hadi kiwango cha taifa na hata dunia nzima (Mohamed, 1995; Madumulla, 2009; na Senkoro, 2011).

Sifa za riwaya

Kuna sifa mbalimbali za riwaya. Kwa kawaida riwaya huwa:

(a) ndefu ikilinganishwa na tanzu nyingine. Urefu wa riwaya ya Mungu Hakopeshwi (Baharoon, 2021) kwa mfano, ni tofauti na ule wa hadithi fupi ya Uwike Usiwike Kutakucha (Ruhumbika, 1978);

(b) na visa changamani, yaani huwa na visa zaidi ya kimoja, ambapo kisa kikuu hujengwa na visa vidogo;

(c) na wahusika wengi na waliokuzwa. Kutokana na riwaya kuwa na visa vingi, basi huwa na wahusika wengi ambao humwezesha mwandishi kukidhi haja hii;

(d) na mandhari pana na huendelezwa kikamilifu. Kwa kuwa riwaya hushughulikia mawazo mengi, hujishughulisha na vipengele vingi vya maisha ambavyo hupatikana katika nyakati na mahali tofauti kama vile shuleni, mijini, vijijini, nyumbani na barabarani. Ili kushughulikia mazingira mapana, simulizi hutumia kipindi kirefu cha wakati ikilinganishwa na kazi kama vile za hadithi fupi ambazo huweza kuchukua kipindi kifupi tu kukamilika;

(e) na migogoro iliyokuzwa zaidi kwa sababu mwandishi ana uhuru mkubwa wa kuiibua na kuieleza kwa kina;

(f) Hutumia lugha ya kisanii ya kinathari / lugha ya mjazo; na

(g) Kwa sababu ya urefu na upana wake, riwaya huwa na uwezo wa kubeba au kutomelea tanzu nyingine (kama vile barua, insha, shairi, wimbo au igizo) bila matatizo. Mathalani, katika riwaya ya Kiu ya Haki (Mwanga, 1983) mwandishi ametumia hadithi ndani ya hadithi. Hadithi mojawapo ni ile ya Mzee Fundisha anayesimulia yaliyompata alipovamiwa na polisi nyumbani kwake na kulazimishwa kutoa rushwa ya Sh. 2,000 ingawa hakuwa na hatia. Vilevile, kuna hadithi ya Sikujua, anayesimulia yaliyompata miaka kumi iliyopita wakati yeye na Pondamali wakifanya biashara ya kubadilisha fedha.

Historia ya riwaya

Riwaya ni utanzu wa hivi karibuni zaidi ukilinganishwa na ushairi na tamthiliya. Inadaiwa kwamba riwaya ilipata umbo lilonalo hivi sasa katika karne ya 18 huko Ulaya. Riwaya ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni na viwanda. Ukoloni na "uvumbuzi" viliumba hali zilizohitaji kuelezwa kwa mawanda mapana kuliko ilivyowezekana katika ngano na hadithi fupi. Uchangamani wa maisha katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, utamaduni na uchumi ulihitaji kuwa na utanzu wa fasihi ulio na uchangamani kifani na kimaudhui pia. Kupanuka kwa usomaji, hasa wakati wa mapinduzi ya viwanda huko Uingereza, kuliwafanya waandishi waandike kazi ndefu kwa sababu walikuwapo wasomaji, hasa wanawake, waliobaki majumbani wakati waume zao wakiwa viwandani (Senkoro, 1984; Njogu na Chimerah, 1999; Madumulla, 2009).

Afrika ni miongoni mwa mabara yenye historia fupi zaidi ya riwaya, ambapo maandiko ya riwaya yalianza kujitokeza mwishoni mwa karne ya 19. Katika eneo la Afrika ya Mashariki, kazi za kinathari za kwanza hazikufidhi ubora wa usanii na ubunifu. Baadhi ya maandiko ya awali ni Habari za Wakilindi (El Ajjemi, 1885, 1907, 1962), Tulivyona na Tulivyofanya Uingereza (Kayamba, 1933), Mwaka katika Minyororo (Sehoza, 1921) na Uhuru wa Watumwa (Mbotela, 1934). Vyote hivi vinaangukia katika kundi linaloendana na tawasifu au masimulizi ya wasafiri. Kwa hakika, kiwango cha usanifu wa vitabu hivi ni cha chini.

Nchini Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazoendelea, nathari andishi ya kibunifu ni fani ambayo ilichelewa kuja. Nathari bunifu simulizi, kama vile hadithi, hekaya na ngano zilizosimuliwa kwa mdomo ndizo ambazo zilizotawala ndani ya jamii.

Kwa upande wa fasihi andishi, kwa kipindi kirefu, maandiko ya fani ya ushairi, hususani tenzi za Kiswahili katika hati ya Kiarabu, ndiyo yaliyotamba katika eneo la Pwani ya Afrika ya Mashariki. Maandiko ya kinathari yalianza baada ya ujio wa wamisionari. Nathari simulizi inayojulikana kuandikwa na wenyeji ni Habari za Muma (bin Hemed, 1880), nayo ilichapishwa mwaka 1935 katika Mambo Leo, gazeti la Kiswahili lililovuma wakati wa ukoloni wa Waingereza. Nathari nyingine ni ile ya Habari za Wakilindi iliyoandikwa na Abdallah bin Hemed bin Ali El Ajjemy mzaliwa wa Zanzibar kwa baba wa Kiarabu na mama wa Kihehe, na ambayo juzuu ya kwanza ilichapishwa mwaka 1894, ya pili mwaka 1904 na ya tatu mwaka 1907. Kitabu hiki kilihusu masimulizi ya Wasambaa. Kumbukumbu nyingine ni zile zilizohusu Lamu na ambazo zinasadikiwa kuwa ziliandikwa na Shaibu Faraji, na kuchapishwa na William Hichens (1928). Maandiko haya yalitokea wakati wa kipindi cha Wajerumani (Njogu na Chimerah, 1999).

Baada tu ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Waingereza walijishughulisha zaidi na kuandika na kufasiri vitabu vya shule vya kiada na ziada. Baadhi ya vitabu hivyo ni: Hadithi ya Allan Quartermain (Haggard [mf.] Frederick Johnson, 1934), Safari za Gulliver (Swift, [mf.] Frederick Johnson, 1932), Mashimo ya Mfalme Sulemani (Haggard, [mf.] Edwin Brenn, 1929), Alfu Lela Ulela ([Waf.] Frederick Johnson na Edwin Brenn, 1929), na Kisiwa Chenye Hazina (Stevenson [mf.] Frederick Johnson, 1929). Maandiko haya yalikuwa maarufu hadi kufikia mwaka wa 1950 ambapo waandishi wazawa walianza kujitokeza kuandika nathari za kibunifu (bunilizi) kwa mfuatano wa kimikondo (Madumulla, 2009).

Riwaya ya Kiswahili iliendelea kukua na kubadilika sambamba na vipindi mbalimbali vya kihistoria nchini Tanzania. Katika kipindi cha miaka 1940 mpaka 1970, riwaya za aina mbalimbali ziliandikwa, zikiwamo za kitawasifu, kimaadili, kiutamaduni, na za kihalifu au kikachero. Kwa mfano riwaya za kimaadili, zina sifa za kifasihi simulizi ambazo ni matumizi ya dijalojia, kutofungwa na wakati pamoja na matumizi ya balagha (chuku), ambayo hukipatia kitu sura, uwezo na nguvu isiyokuwa ya kawaida. Mifano ya riwaya hizi ni Kusadikika (Robert, 1991), Kufikirika (Robert, 1968) na Adili na Nduguze (Robert, 1952).

Riwaya za kiutamaduni zilisheheni maudhui yaliyosawiri tamaduni za jamii mbalimbali. Mfano mmojawapo ni riwaya ya Kurwa na Doto (Farsy, 1960) inayosawiri maisha ya watu wa visiwa vya Unguja na Pemba. Halikadhalika, kuna riwaya ya Mzishi wa Baba ana Radhi (Nkwera, 1967), inayoelezea maisha ya Wapangwa wa mkoa wa Njombe, wilayani Ludewa. Vilevile, kuna riwaya ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka, Ntulanalwo na Bulihwali (Kitereza, 1980) ambayo inasawiri mila na desturi za jamii ya Wakerewe kabla ya kuja kwa wakoloni.

Riwaya za kihalifu au kikachero zilibeba maudhui ya uhalifu na upelelezi. Mifano mizuri ni riwaya za Muhammed Said Abdulla ambazo ni Mzimu wa Watu wa Kale (1957), Kisima cha Giningi (1968), Duniani kuna Watu (1973), Siri ya Sifuri (1974) na Mwana wa Yungi Hulewa (1976).

Baada ya uhuru, na hatimaye Azimio la Arusha kutangazwa, ziliibuka riwaya yenye maudhui yanayohusu siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Katika kipindi hiki, makundi mawili ya waandishi yalijitokeza kuandika riwaya kuelezea Azimio la Arusha. Kundi la kwanza liliuona ujamaa kwa jicho la ujadi. Kundi hili liliandika

kazi zilizosawiri maisha yaliyopita. Mfano wa riwaya za kundi hili ni Mtu ni Utu (Mhina, 1971) na Njozi za Usiku (Seme, 1976). Kundi la pili ni lile lililouona ujamaa kwa jicho la matarajio kwamba kuna ujenzi wa jamii mpya itakayoishi vizuri kuliko jamii iliyokuwapo. Kwa hiyo, kundi hili liliandika kazi kwa shauku ya kueleza mabadiliko yatakayoletwa na kijiji vya ujamaa. Mfano wa riwaya hizo ni Shida (Balisidya, 1975) na Ndoto ya Ndaria (Ngomoi, 1976). Riwaya hizi zililenga kuonesha ubora wa maisha ya vijijini. Muundo wa riwaya hizi ni wa moja kwa moja, lugha nyepesi na wahusika wasio na utata.

Pia, katika kipindi hiki, walijitokeza waandishi walioandika riwaya kwa jicho la kiyakinifu. Riwaya za namna hii ziliyasawiri masuala ya kijamii kipembuzi. Mifano ya riwaya hizo ni Kasri ya Mwinyi Fuad (Shafi, 1978), Kuli (Shafi, 1979) na Dunia Mti Mkavu (Mohamed, 1979). Waandishi wa riwaya hizi wanaeleza mapambano dhidi ya umwinyi na ubepari. Katika riwaya ya Kasri ya Mwinyi Fuad, kwa mfano, kuna mvutano baina ya mamwinyi, watwana na watumwa. Pande hizi mbili zinakanzana na hatimaye, mikinzano inazaa mapinduzi. Kwa kiasi, waandishi hawa waliathiriwa na fikra za Ki-Marx (Senkoro, 1984).

Katika miaka ya 1980, liliibuka wimbi la uandishi wa riwaya pendwa. Riwaya hizi zilizuka kutokana na sababu za kiuchumi, ambapo uchumi wa Tanzania uliyumba kutokana na Vita vya Kagera, majanga kama ukame, pamoja na masharti magumu ya Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia. Waandishi wengi walianza kuandika riwaya pendwa kwa lengo la kujipatia fedha za haraka. Pia, zilizuka kampuni nyingi za uchapishaji nchini. Kampuni hizo zilirahisisha uchapishaji wa riwaya pendwa kwa haraka na kwa gharama nafuu. Soko la riwaya pendwa lilikuwa kubwa kutokana na maudhui yake kupendwa na watu wa rika zote. Aidha, waandishi ndio walikuwa wachapishaji na wauzaji wakuu wa riwaya hizo. Miongoni mwa riwaya hizo ni Tutarudi na Roho Zetu (Mtobwa 1987), Roho Mkononi (Rajab, 1984), Dimbwi la Damu (Mtobwa, 1984), Kikomo (Musiba, 1980) na Njama (Musiba, 1981). Nyingine ni Kijasho Chembamba (Ganzel, 1980), Ufunguo wa Bandia (Rajab, 1974), Jeraha la Moyo (Kiango, 1974) na Kwa Sababu ya Fedha (Simbamwene, 1972).

Pia, katika kipindi hiki waandishi wengi waliandika riwaya zilizohakiki jamii. Riwaya hizi zilitokana na Azimio la Arusha kutokukidhi matarajio ya Watanzania. Wasanii waliandika riwaya kueleza maoni yao kuhusu viongozi walioaminika kuwaongoza wananchi kuyafikia malengo ya vijiji vya ujamaa. Viongozi waligeuka wasaliti, waroho, na wazembe huku wakiendekeza rushwa, uvivu, ulevi na ubadhirifu wa mali ya umma. Mfano wa riwaya za kipindi hicho ni Nyota ya Huzuni (Liwenga, 1978), Njozi Iliyopotea (Mung'ong'o, 1979), Sudi ya Yohana (Chachage, 1981), Kivuli (Chachage, 1981), Harusi (Safari, 1984) na Miradi Bubu ya Wazalendo (Ruhumbika, 1992).

Riwaya hizo za kihakiki zimeendelea kuandikwa mpaka miaka ya 2000. Riwaya hizi zimejadili upokezi na athari za soko huria lililotokana na sera za ubinafsishaji. Katika mfumo huu, njia kuu za uchumi zinamilikiwa na watu binafsi, wengi wao wakiwa si wazawa. Kwa hiyo, wazawa wameendelea kuishi maisha magumu kinyume na matarajio waliyokuwa nayo, baada ya uhuru, hususani baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Mifano ya riwaya yenye maudhui yanayohusiana na ubinafsishaji na soko huria ni Almasi za Bandia (Chachage, 1991) na Makuadi wa Soko Huria (Chachage, 2002).

Ikumbukwe kwamba hakuna mpaka bayana katika vipindi vilivyotajwa hapo juu. Kuna kazi za fasihi andishi yenye maudhui yanayohusu vipindi tofauti katika kipindi kimoja. Hivyo, si ajabu kukuta riwaya za kihakiki katika kipindi cha Azimio la Arusha; hivyo hivyo, riwaya pendwa zinajitokeza katika vipindi vyote. Pia, hali hii inaweza ikatokana na mhamo wa kutoka kipindi kimoja kwenda kipindi kingine. Katika kipindi cha mpito, kunakuwa na kazi za fasihi zinazozungumzia kipindi ambacho kinaelekea kufikia mwisho na nyingine zinakuwa na maudhui ya kipindi kilichopo au hata kijacho.

Aina za riwaya

Riwaya hugawanywa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali. Vigezo vilivyo maarufu ni vya kutazama fani na maudhui. Kifani, riwaya huainishwa kwa kuzingatia jinsi vipengele vya fani vinavyojitokeza. Kadhalika, kimaudhui, mgawanyo hutazama mambo yanayoongelewa katika riwaya inayohusika. Kigezo hiki cha maudhui ndicho kinachotumika katika kitabu hiki. Kwa kutumia kigezo hiki, kuna makundi makubwa mawili ya riwaya: riwaya dhati na riwaya pendwa.

1. Riwaya dhati

Riwaya dhati ni zile zinazochambua matatizo au masuala mazito ya kijamii, kutafuta sababu zake, athari zake na ikiwezekana ufumbuzi wake. Riwaya hizi hukusudiwa kumfikirisha msomaji kuhusu masuala mazito na si kumstarehesha tu. Riwaya dhati zimegawanyika katika aina mbalimbali. Aina hizo ni: riwaya za kijamii, kisaikolojia, sira, kiistiara, kingano, teti, chuku, kihistoria, kimaadili, kimapinduzi na kifalsafa. Pia, kuna riwaya za barua, vitisho na za watoto na vijalunga.

(a) Riwaya za kijamii

Hizi ni riwaya zinazosawiri maisha na matatizo ya kawaida ya kijamii. Matatizo hayo huweza kuwa ya kifamilia, kimahusiano, kitabaka, kisiasa na kiutamaduni. Maudhui mengine ni mgongano kati ya ukale na usasa, kati ya maisha ya mjini na ya vijijini na migogoro ya kifamilia. Wahusika wake, aghalabu, huwa halisi ambao wanapatikana katika jamii. Hivyo, huifanya riwaya iwe inaishi wakati wote, yaani haichuji. Aina hii ndiyo yenye idadi kubwa ya riwaya. Mifano ya riwaya za aina hii ni Siku ya Watenzi Wote (Robert, 1968), Rosa Mistika (Kezilahabi, 1971), Titi la Mkwe (Banzi, 1972) na Nyota ya Rehema (Mohamed, 1978).

(b) Riwaya za kisaikolojia

Hizi ni riwaya zinazosaili nafsi ya mhusika. Hudodosa fikra, hisia, mawazo, imani, hofu, mashaka, matumaini na matamanio ya mhusika binafsi. Vilevile, hudadisi athari za mambo hayo kwa mhusika na labda jamii yake. Hueleza mikinzano ya ndani ya mhusika kinafsi, kiakili na kijinsia. Baadhi ya riwaya za aina hii ni: Rosa Mistika (Kezilahabi, 1971), Kiu (Mohamed, 1972), Ukiwa (Mkangi, 1973), Kichwamaji (Kezilahabi, 1974), Tata za Asumini (Mohamed, 1990), na Mhanga Nafsi Yangu (Mohamed, 2012).

(c) Riwaya za sira

Hizi ni riwaya ambazo husimulia habari za maisha ya mtu. Riwaya za aina hii zimegawanyika katika makundi mawili: riwaya za kitawasifu na za kiwasifu.

(d) Riwaya za kitawasifu

Riwaya za kitawasifu ni zile zinazotumia nafsi ya kwanza, yaani mwandishi anaeleza mwenyewe kuhusu maisha yake tangu kuzaliwa kwake hadi muda wa kuandika riwaya husika; au hueleza kipande cha maisha yake ambacho sio lazima kiwe hadi anapoandika. Mwandishi hueleza matukio ambayo huona yanasisimua na huenda hayatokei kwa wengine. Kwa kuyaeleza, anadhani yanaweza kuwasaidia wasomaji. Riwaya za aina hii huweka kumbukumbu au historia ya maisha ya mtu binafsi. Mifano ya riwaya za aina hizi ni Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (Robert, 1949 na 2003), Mbali na Nyumbani (Shafi, 2013) na Nasikia Sauti ya Mama (Walibora, 2015).

(e) Riwaya za kiwasifu

Riwaya za kiwasifu ni zile zinazotumia nafsi ya tatu, yaani mwandishi husimulia maisha ya mtu mwingine. Mfano wa riwaya za wasifu ni Wasifu wa Siti Binti Saad (Robert, 1967).

(f) Riwaya za istiara

Hizi ni riwaya za mafumbo ambazo umbo lake la nje ni ishara au kiwakilishi tu cha jambo jingine. Mifano mizuri ni riwaya za Kusadikika (Robert, 1991) na Kufikirika (Robert, 1968) ambazo huenda ni istiara kuhusu utawala wa mabavu wa kikoloni.

(g) Riwaya za kingano

Hizi ni riwaya yenye umbo na mtindo wa ngano. Mathalani, huweza kuwa na wahusika wanyama, visa vya ajabuajabu, mandhari ya kubuni na visa vyenye kutendeka nje ya wakati wa kihistoria. Mfano wa riwaya za kingano ni Adili na Nduguze (Robert, 1952) na Lila na Fila (Kiimbila, 1966).

(h) Riwaya teti

Hizi ni riwaya zinazosimulia vituko na masaibu ya maayari (watu wapuuzi, laghai, wajanja, na kadhalika) kwa njia inayosisimua na kuchekesha. Aghalabu maayari hao huwa watu wanaovutia (si wahusika wawi/waovu), wanatokea tabaka la chini, na bapa. Matukio ya riwaya hii hayana msuko ulioshikamana vizuri.

(i) Riwaya barua

Hizi ni riwaya ambazo sehemu yake kubwa husimuliwa kwa njia ya barua wanazoandikiana baadhi ya wahusika. Mfano ni riwaya ya Barua Ndefu kama Hii (Mariama Bâ, 2009).

(j) Riwaya za kihistoria

Riwaya hizi huchanganya historia halisi na ubunifu ili kutoa maudhui fulani. Mara nyingi, riwaya hizi zinajikita kwenye matukio makuu ya kihistoria yaliyoathiri mwenendo na mwelekeo wa jamii au taifa linalohusika. Riwaya ya kihistoria huchanganya wahusika wa historia na wa kubuni, matukio ya kweli na ya kubuni. Hata hivyo, riwaya hizo huzingatia zaidi namna matukio makuu ya kihistoria yalivyomwathiri mtu binafsi aliyeyashiriki. Riwaya ya kihistoria ina dhamira zinazogusa watu wengi, ni muhimu kwa sababu masimulizi yake yanahusu mambo yaliyotokea, na inawezekana yaliwahi kuwapata hata wasomaji. Ni kumbukumbu nzuri ya kipindi kilichopita. Baadhi ya riwaya mashuhuri za kihistoria ni Uhuru wa Watumwa (Mbotela, 1934), Kuli (Shafi, 1979), Zawadi ya Ushindi (Mtobwa, 1987), Kwa Heri Iselamagazi (Mapalala, 1992) na Pambazuko Gizani (Mboneko, 2004). Pia, kuna riwaya za Mulokozi za Ngome ya Mianzi (1990), Ngoma ya Mianzi (1991) na Moto wa Mianzi (1996). Nyingine ni Miradi Bubu ya Wazalendo (Ruhumbika, 1992) na Wachamungu wa Bibi Kilihona (Ruhumbika, 2014).

(k) Riwaya za kimaadili

Hizi ni riwaya yenye nia ya kufundisha maadili fulani yahusuyo mwenendo mwema katika maisha. Ni riwaya zinazowapa watu maadili, na mara nyingi, maadili hayo huwa ya kidini. Wahusika wakuu huwa na sifa na tabia nzuri bila udhaifu. Sifa hizo ni za kudumu; kama ni mwenendo mwema huwa mwema tangu mwanzo hadi mwisho wa hadithi. Mabadiliko yakitokea, huwa ya kimaadili na hutokea ghafla. Mifano ya riwaya za aina hii ni *Adili na Nduguze* (Robert, 1952) *Kisa cha Mrina Asali na Wenzake Wawili* (Mnyampala, 1961) na *Mtu ni Utu* (Mhina, 1971).

(l) Riwaya za kimapinduzi

Hizi ni riwaya zinazojadili matatizo yanayosababisha migogoro fulani katika jamii kwa lengo la kuleta mabadiliko. Mabadiliko hayo huweza kuwa ya kisiasa, kiutamaduni au kiuchumi. Aghalabu, lengo la riwaya hizi ni kuuewezesha umma kushika hatamu kwa njia ya mapambano. Mifano ya aina hii ya riwaya ni *Ubeberu Utashindwa* (Kiimbila, 1971), *Kasri ya Mwinyi Fuadi* (Shafi, 1974), *Kabwela* (Saffari, 1976), *Dunia Mti Mkavu* (Mohamed, 1979) na *Kuli* (Shafi, 1979).

(m) Riwaya za kifalsafa

Riwaya za kifalsafa ni zile zinazojadili masuala anuai kuhusu maisha. Aghalabu, masuala hayo ni yale yanayohitaji tafakuri ya kina. Hii inamaanisha kuwa riwaya hizi zinajadili kwa kina na kwa kufanya tafakuri makini kuhusu mambo ambayo hayaonekani kwa urahisi. Muundo wa riwaya hizi ni changamani. Riwaya hizi hujadili maswali kuhusu maana ya ukweli, maisha au kifo kama vile ukweli ni nini? Maisha ni nini? Kifo ni nini? Kuwapo na kutokuwapo ni nini? Mifano ya riwaya za kifalsafa ni *Mzingile*, *Kichwamaji* (Kezilahabi, 1974), *Dunia Uwanja wa Fujo* (Kezilahabi, 1978), *Mafuta* (Mkangi, 1984), *Kiza katika Nuru* (Mohamed, 1988), *Nagona* (Kezilahabi, 1989), *Ziraili na Zirani* (Mkufya, 1999), na *Babu Alipofufuka* (Mohammed, 2001).

(n) Riwaya za vitisho

Hii ni riwaya yenye visa vya kutisha na kusisimua. Mara nyingi, visa hivyo huambatana na mambo ya ajabu au miujiza. Mambo hayo ni kama vile mauaji ya kishirikina, uchawi, uganga na vita. Mifano ya riwaya hii ni *Mbojo Simba Mtu* (Kuboja, 1971), *Mirathi ya Hatari* (Mung'ong'o, 1977) na *Janga Sugu la Wazawa* (Ruhumbika, 2002). Kwa mfano riwaya ya *Mirathi ya Hatari*, imeeleza visa na mikasa ya kisihiri katika jamii za Njombe. Msanii amemtumia Gusto ambaye anarithishwa mirathi ya hatari (uchawi) kutoka kwa baba yake, Kazembe. Mirathi hiyo inasababisha vifo visivyokuwa vya kawaida. Miongoni mwa vifo hivyo ni kile cha mama yake Gusto, dada yake (Nandi) na mjomba wake Gusto (Kapedzile). Kuwapo kwa matukio mengi ya kichawi kunaleta hofu kwa wasomaji wa riwaya hii. Zaidi, matendo yanayotendeka wakati Gusto akila kiapo cha uchawi yanatisha mno.

(o) Riwaya za watoto na vijalunga

Riwaya za watoto na vijalunga hutofautiana na riwaya za watu wazima kwa sifa kadhaa, zikiwamo za aina za wahusika, muundo, msuko, uchache wa visa, michoro na picha, matumizi ya fantasia na fonti zinazotumika. Vilevile, riwaya za watoto huepuka kusawiri matukio hasi kama vile ya mauaji, masuala ya ngono, na mahusiano ya jinsia moja. Mifano ya riwaya hizo ni *Safari ya Prospa* (Lema, 1995), *Kimbia Helena Kimbia* (Mnyaka, 1995), *Moto wa Mianzi* (Mulokozi, 1996) na *Marimba ya Majaliwa* (Semzaba, 2008).

2. Riwaya pendwa

Riwaya pendwa ni zile ambazo hutumia fani inayojichomoza na kusisimua zaidi kiasi cha kuweza kufunika maudhui. Hali hii huifanya riwaya hizi zionekane kuwa na lengo la kustarehesha au kuburudisha wasomaji tu. Mambo yanayosawiriwa sana na waandishi wa riwaya za kundi hili ni mapenzi, upelelezi, ujasusi, ugaidi, ujambazi na mauaji. Waandishi wa riwaya pendwa huyasawiri mambo hayo kwa ufundi mkubwa; na hupangilia visa na vituko kwa namna inayosisimua. Nchini Tanzania, aina hii ya riwaya iliandikwa kwa mara ya kwanza na Mohamed Said Abdulla (MSA) alipoandika riwaya ya *Mzimu wa Watu wa Kale* (1957). Mifano mingine ya riwaya hizi ni *Simu ya Kifo* (Katalambula, 1965), *Kisima cha Giningi* (Abdulla, 1968) na *Njama* (Musiba, 1981). Uandishi wa riwaya za aina hii uliongezeka maradufu katika miaka ya 1980, kutokana na matatizo ya kiuchumi.

Sifa za riwaya pendwa

Riwaya pendwa zina sifa zifuatazo:

(i) Hutumia taharuki kwa kiasi kikubwa

Taharuki ni hamu kubwa anayokuwa nayo msomaji kutaka kujua mambo yatakayotokea na yatakavyotokea katika hadithi. Taharuki hutumiwa kwa kiasi kikubwa katika riwaya pendwa kupitia matukio ya kusisimua yanayojibainisha kupitia migogoro iliyosukwa kwa ufundi. Taharuki inafikia kilele wakati fumbo linapofumbuliwa kwa kujibiwa maswali kadhaa yaliyojitokeza akilini mwa msomaji. Kwa mfano, katika riwaya ya *Mzimu wa Watu wa Kale* (Abdulla, 1957) swali linalojitokeza ni: nani amemuua Bwana Ali Bomani? Mbinu za awali zamsanii za kumfanya msomaji awatuhumu watu wasiohusika ndizo zinazojenga maswali akilini mwa msomaji.

(ii) Hutumia wahusika wa kimwendelezo

Riwaya pendwa zina sifa ya kutumia wahusika walewale; hivyo, huwa na uwezo wa kujiendeleza katika vitabu kadhaa. Karibu kila mwandishi maarufu wa riwaya pendwa ameandika vitabu zaidi ya kimoja. Sifa hiyo ya kuwatumia wahusika walewale hufanya kitabu kimoja katika mfululizo wa vitabu kadhaavya mwandishi mmoja kionekane kama tukio linalojitegemea katika mfululizowa matukio mengi. Mifano ya watunzi waliowatumia wahusika wa jinsi hiini Aristablus Elvis Musiba. Huyu amemtumia mhusika Willy Gamba katikariwaya zake. Pia, Muhammed Said Abdulla amemtumia mhusika Bwana Msakatika riwaya zake takribani zote. Mwandishi mwingine ni Ben Mtobwa ambayeamemtumia mhusika Joram Kiango katika baadhi ya riwaya zake.

(iii) Huwa na mhusika mkuu mkwezwa

Mhusika wa riwaya pendwa mara nyingi hupewa sifa zisizo za kawaida kitabiana kiutendaji. Mhusika mkuu wa riwaya pendwa hukwezwa juu ya wahusikawengine; hivyo, anatawala na ana sifa ya ubabe. Wahusika hawa huwa na sifaya kuwa kielelezo chenye ukamilifu, yaani kutokuwa na dosari. Mifano mizuriya wahusika wa namna hii ni Bwana Msa, Willy Gamba na Joram Kiango. Marakwa mara, mhusika mkuu ndiye mshindi hata akipitia katika taabu na mashakaya aina gani, tunajua, hatimaye ataibuka kuwa mshindi katika mapambano yake.Wahusika hawa wakuu hutenda na kuendesha mambo yao kama miungu wadogopasi na kukosea. Huwa hodari sana katika kutenda mambo yao. Mambo hayoni kama vile kuchunguza, kufanya mapenzi, kuwindana, kupigana kwa silahana kwa mikono mitupu. Kwa hiyo, ufundi wa utendaji unaojitokeza humohuwa unaziteka nafsi za wasomaji na, wakati mwingine, kuwasahaulisha hatamaudhui. Mfano mzuri ni mhusika mkuu wa riwaya ya Njama (Musiba, 1981).Msomaji anapoendelea kuisoma riwaya hii, anajikuta anamezwa na ufundi wakupeleleza na kupambana unaooneshwa na Willy na wenzake kiasi cha kupotezakiini cha simulizi yenyewe, ambacho kinahusu ukombozi wa nchi za Afrika. Halihii inasababishwa na hali ya kukwezwa kwa wahusika wa riwaya, hususani WillyGamba, katika tabia na matendo yao.

(iv) Hupendwa na watu wengi

Riwaya hizi zina wasomaji na wapenzi wengi, hasa vijana. Hii ni kwa sababuwasanii wake wameupatia vizuri utunzi wa kisasa ambao umeletwa na utamaduni wa kigeni unaofuatwa kwa makini na vijana na baadhi ya watu wazima. Kwa hivyo, watu wanaposoma riwaya hizi, wanasisimka na kuburudika.

(v) Hutumia mandhari ya mijini

Wasanii wa riwaya pendwa hutumia mandhari halisi au ya kubuni, hususan katika miji au majiji. Hali hii ndiyo inayooonesha upekee wa mandhari ya riwaya pendwa.Wasanii hutumia mandhari ya namna hii ili kukidhi malengo ya usukaji wa visana maisha ya wahusika. Mandhari ya namna hii hubeba matukio kama vile ufujajimkubwa wa fedha kwenye sehemu za starehe, kama vile baa, hoteli kubwa nafukwe za bahari. Kwa mfano, kwenye riwaya ya Salamu Toka Kuzimu (Mtobwa,1987), kuna ufujaji mkubwa wa fedha unaofanywa na mhusika Joram na mpenziwake. Vilevile, mandhari ya mjini yanaoneshwa kupitia tukio kama la uchezajiwa kamari linalojitokeza kwenye riwaya ya Simu ya Kifo (Katalambula, 1965).Aidha, mandhari ya mjini au jijini yanathibitishwa na kuwapo kwa kampuni namashirika makubwa. Kampuni hizi huajiri watu. Waandishi huumba wahusikawenye vyeo kwa kuhusianisha na kampuni na mashirika hayo. Mfano mzuri nimhusika Kalulu katika riwaya ya Pesa Zako Zinanuka (Mtobwa 1984). Huyu nikiongozi katika kampuni mojawapo ya kusambaza dawa za Oxton. Mzee Jacobokwenye Simu ya Kifo (Katalambula, 1965) ni mfanyakazi katika shirika la reli.

Mandhari ya mijini pia hudhihirika kupitia matumizi ya vyombo vya mawasilianokufanikisha matukio ya ujambazi, ujasusi, uporaji na uhusiano wa kimapenzi.Mathalani, katika riwaya ya Najisikia Kuua Tena (Mtobwa, 1985), mhusikaKwame anatega chombo cha kunasa mawasiliano ofisini kwa Kombora. Chombohiki kinamsaidia kunasa maongezi yote ya mipango ya kuwasaka wahalifu(Kwame na kundi lake). Kwa njia hii, Kwame na kundi lake wanang'amuamikakati ya kukamatwa, hivyo, wanafanikiwa kuwakimbia askari.

(vi) Matumizi ya wanawake kama nyenzo ya mafanikio

Kwa ujumla, wahusika wakuu wa kiume wa riwaya pendwa husawiriwawakifanikiwa katika mambo yao kupitia mbinu ya kuwatumia wanawakewarembo. Warembo hao hutumiwa kwa njia za mapenzi, kuwa chambo chakufanyia uhalifu, au chambo cha kumnasia adui. Mapenzi, kwa upande wake,huonekana kuwa jambo muhimu sana katika riwaya pendwa. Huonekanakwamba, upelelezi au shughuli yoyote inayofanyika haiwezi kusisimua walakufanikiwa bila mapenzi. Katika riwaya za Musiba, kwa mfano, mhusika WillyGamba huwa na wasichana warembo ambao ndio wapenzi wake wanaomsaidiakufumbua mafumbo mazito na mitego mikubwa. Baadhi yao ni Zabibu kwenyeriwaya ya Njama, (Musiba 1986), Tete na Mwadi kwenye riwaya ya Kikosi cha Kisasi, (Musiba 2018), pamoja na Nyaso kwenye riwaya ya Hofu (Musiba 2018).

(vii) Huiga mawazo na matendo ya filamu za kigeni

Riwaya pendwa nyingi za Kiswahili, hasa za miaka ya 1980, ni mwigo wa maandishi ya Kimagharibi pamoja na filamu za Kizungu na Kiasia zinazohusu upelelezi, ujasusi, uhalifu na mapenzi. Wasomaji wengi wameifanya riwaya pendwa kama kibadala au kijalizo cha filamu. Kwa mfano, Musiba kwenye riwaya zake amemchora mhusika mkuu, Willy Gamba, kwa kumpa ujuzi wa kupigana kininja katika mapambano dhidi ya majasusi. Kupigana kwa kufuata sheria za kininja, mara nyingi, ni mbinu zinazotumiwa na filamu za Kimagharibi na Kimashariki.

Shughuli 2.15

Soma riwaya na hadithi fupi teule, kisha eleza tofauti ya tanzu hizo.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

1. Kwa kutumia mifano, tofautisha dhana zifuatazo:

  1. melodrama na farsa
  2. utao na ukwapi
  3. riwaya za kihistoria na za sira
  4. mashairi na tenzi
  5. riwaya za kifalsafa na za kisaikolojia

2. "Riwaya ni zao la fasihi simulizi." Jadili

3. "Tamthiliya ya Kitanzania za sasa ni zao la tamthiliya za Kimagharibi." Jadili.

4. Eleza kwa ufupi namna dhana ya utendaji inavyojitokeza katika tamthiliya.

5. Kwa kutumia mifano, eleza aina za tamthiliya na namna zinavyotofautiana.

6. Kwa kutumia mifano, jadili mabadiliko ya ushairi wa Kiswahili katika vipindi mbalimbali.

7. "Hadithi fupi ni utanzu usioeleweka" Jadili kauli hii kwa mifano.

8. Jadili maendeleo ya riwaya ya Kiswahili baada ya Uhuru.

9. Eleza mchango wa mapinduzi ya viwanda katika kuzuka na kukua kwa riwaya.

10. Kwa kutumia mifano thabiti, jadili kauli kuwa fasihi simulizi ni malighafi ya fasihi andishi.

Uhusiano baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi

Licha ya kutofautiana, aina za fasihi zina uhusiano wa mwingiliano. Kwa mfano, kazi za fasihi andishi zina vipengele vya kifasihi simulizi kama vile semi, nyimbo na mazungumzo au dayalojia, wahusika wasio wanadamu (kwa mfano wanyama, mazimwi, wadudu na vinginevyo) na mbinu za uwasilishaji (mianzo na miisho ya hadithi, mianzo na miisho ya tenzi na nyinginezo). Mbali na mwingiliano, aina hizi za fasihi hutofautiana, kama inavyoonyeshwa katika jedwali lifuatalo:

Tofauti kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi

Na.

Kigezo

Fasihi simulizi

Fasihi andishi

1.

Utunzi

Huweza kutungwa mapema na kukaririwa kabla ya uwasilishaji. Huweza pia kutungwa papo hapo wakati wa utendaji.

Hutungwa kwa kipindi kirefu kabla ya kuwasilishwa kwa hadhira.

2.

Uwasilishaji

Huwasilishwa kwa njia ya mdomo, ishara na vitendo. Uwasilishaji huo hutumia viambato kama vile maleba, miondoko na sauti.

Huwasilishwa kwa njia ya maandishi.

3.

Umri

Ni kongwe kwa sababu ilianza kabla ya ugunduzi wa maandishi.

Ilianza baada ya mwanadamu kugundua maandishi.

4.

Umiliki

Tanzu nyingi za fasihi simulizi ni mali ya jamii nzima.

Ni mali ya mtunzi na mdhamini wake.

5.

Uhifadhi

Huhifadhiwa kichwani na kuendelezwa kwa njia ya kupokezana, ijapokuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, huweza kuhifadhiwa katika vinasa sauti, kompyuta na hata maandishi.

Huhifadhiwa katika nyaraka au kwa njia za kidijiti.

6.

Tanzu na vipera

Idadi ya tanzu na vipera vya fasihi simulizi ni kubwa kuliko ilivyo katika fasihi andishi. Aidha, huwa na mwingiliano mkubwa wa vipera.

Idadi ya tanzu na vipera vya fasihi andishi ni ndogo. Aidha, vipera vyake havina mwingiliano mkubwa.

7.

Mabadiliko

Hubadilika kwa haraka kutegemeana na mahitaji ya hadhira, tukio la kijamii na wakati.

Haibadiliki kwa haraka kwa sababu ipo katika hali ya kudumu.

8.

Hadhira

Hadhira yake ni hai ambayo hushiriki katika utendaji kama kuitikia, kupiga vigelegele na makofi.

Ni wasomaji; hivyo hawashiriki katika utendaji, isipokuwa katika tanzu chache zinazowasilishwa kiutendaji kama vile mashairi na tamthiliya.

9.

Wahusika

Hutumia wahusika mchanganyiko (kwa mfano binadamu, wanyama, mimea na vitu visivyo na uhai).

Hutumia zaidi wahusika binadamu. Wahusika wasio binadamu hutumika mara chache.

10.

Muundo

Huwa na muundo wa moja kwa moja, aghalabu bila utata.

Huweza kuwa na muundo wa moja kwa moja au changamani kutegemeana na utanzu.

Shughuli ya 2.16

Kwa kutumia vyanzo vya maktabani na mtandaoni, eleza namna fasihi simulizi ilivyochangia kupatikana kwa fasihi andishi.

Mchango wa fasihi simulizi katika maendeleo ya fasihi andishi

Maendeleo ya fasihi andishi kabla ya uhuru yana uhusiano mkubwa na wamisionari na watawala wa kigeni. Wageni hawa walipofika pwani ya Afrika Mashariki, waliwakuta wenyeji wakiwa na fasihi yao. Kwa mfano, baadhi ya tenzi za zamani kama vile Fumo Liyongo zilikuwa zikisimuliwa kabla ya maandishi na ziliwekwa katika maandishi baadaye. Pia, tenzi hizi zilitokana na nyimbo ambazo ndizo fasihi ya awali.

Halikadhalika, kuna athari za mashairi na fani nyinginezo kama tarihi, masimulizi ya wasafiri, ngano na hekaya mbalimbali. Ngano na hekaya hizi ndizo zilitafsiriwa na kuwa msingi wa hadithi za awali za Kiswahili. Miongoni mwa hadithi hizo ni Swahili Tales as Told by the Natives of Zanzibar (1870) zilizotafsiriwa na Edward Steere. Ngano nyingine zimechapishwa katika Kitabu cha Prosa und Poesie der Suaheli (1907) kilichohaririwa na Carl Velten, Mazungumzo ya Alfu Lela Ulela Juzuu (1-4) (1928) kilichotafsiriwa na Edwin Brenn na kuhaririwa na Frederick Johnson na Hekaya za Abunuwasi (Chiponde, 1928). Kisiwa chenye Hazina (Johnson, 1929), Safari za Gulliver (Swift, 1932), Mashimo ya Mfalme Suleimani (Haggard, 1937) na Safari ya Msafiri (Bunyan, 1925).

Kama ulivyojifunza kuhusu tanzu na vipera vya fasihi simulizi, fasihi hii inajumuisha hadithi, semi, ushairi na sanaa za maonesho na vipera vyake. Baadhi ya tanzu hizi hujitokeza katika fasihi andishi kwani vipengele mbalimbali vya tanzu hizo huweza kutumika kama mbinu za kisanaa katika kazi za fasihi andishi. Mfano wa vipengele hivyo ni wahusika wasio binadamu kama vile wanyama, mashetani na mazimwi, kama wanavyojitokeza katika riwaya za titisho na za kingano. (Senkoro, 2011).

Kuanzia miaka ya 1940 hadi 1960, riwaya nyingi za Kiswahili zilifuata mkondo wa hekaya na ngano. Kimaudhui, riwaya hizo zilielezea mambo ya mila na desturi kama njia ya kutunza maadili. Mifano ya riwaya hizo ni Adili na Nduguze (Robert, 1952), Kusadikika (Robert, 1991) na Kufikirika (Robert, 1968).

Kimsingi, fasihi simulizi imekuwa nguzo ya fasihi andishi katika kueneza tamaduni mbalimbali za kijamii. Waandishi mbalimbali wamechota fikra kutoka katika kazi mbalimbali za kifasihi simulizi na kuzitumia katika tungo za fasihi andishi.

Shughuli ya 2.17

Chunguza vipindi vya fasihi simulizi vinavyorushwa na vituo vya runinga au sikiliza vipindi kutoka katika vituo viwili vya redio, kisha eleza athari zinazotokana na vipindi hivyo kurushwa kwa njia hizo.

Athari za sayansi na teknolojia katika maendeleo ya fasihi simulizi na fasihi andishi

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamesaidia sana katika uwasilishaji na uenezaji wa fasihi simulizi. Maendeleo haya yamewezesha kuwapo kwa vyombo mbalimbali vya uwasilishaji kama redio, runinga na simu. Redio na runinga zimekuwa na mchango mkubwa katika uwasilishaji na uenezaji wa kazi za fasihi simulizi. Kwa mfano, Redio Tanzania (kwa sasa TBC Taifa) imekuwa na vipindi ambavyo vimesaidia sana fasihi simulizi kuwafikia watu wengi. Kipindi kama vile Mama na Mwana kilipendwa na watu wengi, hasa watoto, kwa sababu ya masimulizi ya hadithi mbalimbali. Kipindi kingine ni Cheichei Shangazi ambacho kimekuwa na masimulizi ya hadithi, vitendawili na nyimbo. Baadaye, vilianzishwa vituo vingine vya redio na kuongeza mawanda ya uwasilishaji na uenezaji wa kazi za fasihi simulizi. Kwa mfano, Redio One Stereo hurusha kipindi cha Watoto Wetu ambacho hupambwa na wimbo maarufu wa “Watoto Wasafi Moyoni”. Kipindi hiki hurushwa kila Jumamosi, ambapo watoto walioko studio na nyumbani huweza kushiriki katika uwasilishaji wa hadithi, methali, vitendawili, mafumbo na nyimbo.

Pamoja na watoto kutoonana ana kwa ana, wanaweza kushiriki kwa njia ya kusikiliza. Hivyo, hadithi ambazo awali zilisimuliwa kwa watu wachache, zinaweza kujulikana kwa wote wanaosikiliza. Mbali na vipindi vya watoto, redio zimekuwa zikirusha vipindi vingine vya fasihi simulizi. Baadhai ya vipindi hivyo ni Mkoa kwa Mkoa, Malenga Wetu, Ngoma Zetu, Zilipendwa, (TBC Taifa), Hizi Nazo (Redio One Stereo), Kwa Raha Zetu (Redio Clouds FM) na Mitikisiko ya Pwani (Times FM).

Kwa upande wa runinga, uwasilishaji umekuwa tofauti kidogo. Katika runinga washiriki wana fursa ya kuona matendo yanayotendwa. Kuna vipindi vya watoto ambavyo huwasilisha kazi za fasihi simulizi. Mfano wa vipindi hivyo ni kipindi cha Watoto kilichoandaliwa na TET ambacho hurushwa na TBC1 na TBC2. Kipindi hiki kinachorushwa siku za Jumamosi na Jumapili, husimulia hadithi na michezo ya watoto. Pia, kuna kipindi cha Ubongo Kids (TBC1) ambacho kinahusu somo la hisabati na kusoma. Kipindi hiki huwa na matumizi ya nyimbo, usimulizi wa hadithi, na maigizo mbalimbali. Aidha, kituo cha ITV hurusha kipindi cha Watoto Show ambacho hujumuisha nyimbo, ngoma, methali, vitendawili na hadithi. Halikadhalika, runinga zimekuwa zikirusha vipindi kama vile, Mizengwe, Sanaa na Msanii, Mashamshamu ya Pwani na Hawavumi lakini Wamo (ITV). Vipindi vingine ni Futuhi, Bongo Beats na Msanii Wetu (Star TV). Aidha, kuna Fataki, Ngoma Zetu, Mchikicho wa Pwani Club Raha Leo Show (TBC1), na Mirindimo ya Pwani (Channel Ten). Vipindi vyote hivyo vimekuwa vikisaidia uwasilishaji na uenezaji wa fasihi simulizi.

Matumizi ya simu nayo yana mchango mkubwa katika jamii. Watu wengi hutumia simu kwa mawasiliano ya mazungumzo. Kuwapo kwa mawasiliano ya mitandao ya kijamii kwa kutumia simu kumewezesha uwasilishaji na uenezaji wa fasihi simulizi. Baadhi ya simu zina uwezo wa kurekodi na kutuma nyimbo, masimulizi na picha. Pia, zina uwezo wa kunasa vituo mbalimbali vya redio na runinga na, hivyo, kuwawezesha watumiaji wake kusikiliza kazi za kifasihi. Vilevile, vifaa kama vile vishikwambi, na kompyuta vimerahisisha uhifadhi, ubebaji, na usomaji wa kazi za fasihi andishi. Zaidi, teknolojia imesaidia kupatikana kwa majukwaa ya kidijiti kama vile mitandao ya kijamii ambayo waandishi wa kazi za fasihi simulizi na andishi huitumia kuwasilishia au kuuzia kazi zao.

Kadhalika, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, fasihi simulizi pia imekuwa ikiwasilishwa kwa njia ya maandishi. Hii inatokana na kuongezeka kwa viwanda vya uchapaji ambavyo vimerahisisha mchakato wa uzalishaji wa machapisho ya kazi mbalimbali za fasihi, zikiwamo zinazotokana na fasihi simulizi.

Shughuli ya 2.18

(a) Kusanya semi kumi (10) za Kiswahili kulingana na makundi yafuatayo:(i) Methali tano (5) zinazoonyesha kuhusu utovu wa nidhamu.(ii) Misemo mitano (5) inayohamasisha umoja na ushirikiano katika jamii.

(b) Jadili mchango wa semi ulizozikusanya na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii.

Mchango wa fasihi simulizi na fasihi andishi katika maendeleo ya jamii

Fasihi simulizi na andishi zimekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ambao umesaidia katika kuigeuza na kuibadilisha jamii. Mchango huo umeweza kujidhihirisha kama ifuatavyo:

(a) Kuelimisha jamiiMchango mkubwa wa fasihi simulizi na andishi ni kuelimisha jamii. Fasihi huufumbua macho umma na kupiga vita matatizo ya njaa, maradhi, umaskini na mengineyo. Aidha, fasihi huipa jamii maarifa na stadi za kukabiliana na mazingira ambayo jamii inaishi. Kwa mfano, kuna nyimbo mbalimbali zinazotoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira. Kutokana na nyimbo hizo jamii imeweza kuelimika na kupata maarifa ya namna ya kutunza mazingira pamoja na kuendeleza shughuli za maendeleo binafsi na ya kitaifa. Jamii inasisitiza kuwa mazingira yasipotunzwa husababisha mabadiliko hasi ya tabia nchi.

(b) Kuburudisha jamii

Mchango mwingine wa fasihi simulizi na andishi ni kuburudisha jamii. Katika kutimiza jukumu hili, fasihi hustarehesha, huliwaza na kutuliza mwili na akili ya hadhira. Kwa mfano, watu wanapotazama vichekesho na maigizo ya "Mizengwe" (katika ITV Tanzania) hufurahia vituko, kejeli na mizaha inayoigizwa.

(c) Kuutambulisha na kuendeleza utamaduni

Fasihi simulizi na andishi husaidia kuutambulisha, kuutangaza na kuendeleza utamaduni. Kwa mfano, kazi mbalimbali za fasihi simulizi na fasihi andishi ya Kiswahili huakisi vipengele mbalimbali vya utamaduni wa Mswahili. Mifano ya vipengele hivyo ni desturi, dini, mavazi, mila, vyakula, na namna ya kuhusiana. Vilevile, mchango mwingine ni kuchangia katika kutunza amali na kumbukumbu nyingine za jamii. Mifano ya amali hizo za kijamii ni mila, desturi, historia na sanaa. Tamthiliya za Kiswahili kama vile *Kinjeketile* (Hussein, 1969) na *Ngoma ya Ng'wanamalundi* (Mbogo, 1988) zimebeba vyema jukumu hili la kuhifadhi na kurithisha amali za jamii. Pia, zinafafanua masuala ya kijadi kama vile imani na uganga.

(d) Kuadibu na kunasihi jamii

Mara nyingi, fasihi hutumika kama nyenzo ya kuasa na kuadibu kuhusu mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii. Kwa mfano, tamthiliya ya *Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe* (Semzaba, 1988) inawaadibu na kuwaasa watu kufanya kazi kwa nidhamu. Kwa ufupi, tamthiliya hiyo inatoa funzo kwamba mtaka yote kwa pupa, hukosa yote. Katika fasihi simulizi, nyimbo hutumika kukamilisha jukumu hili. Kwa mfano, baadhi ya nyimbo za bongo fleva zina wasihi watu kupambana na harakati za maisha kwa kutafuta fursa za kiuchumi, bila kujali umbali unaoweza kusababisha utengano wa kifamilia.

(e) Kukuza na kuhifadhi lugha

Fasihi simulizi na andishi ina mchango mkubwa katika kuikuza lugha. Lugha haiwezi kudumaa kwa sababu inakuwa kwenye matumizi. Mwanafasihi hutumia maneno kuibua na kueleza dhana mbalimbali katika utunzi wa kazi zake. Uandishi na usimulizi wa kazi za fasihi huibua misemo mipya mara kwa mara; kwa njia hii lugha huweza kukua. Kwa mfano, katika riwaya ya *Kusadikika* (Robert, 1991) kuna uibuaji wa msamiati kama vile 'ali ali' (tukufu) 'azali' (asili au kiini) 'kitali' (mapigano) na 'mlizamu' (chemchem).

(f) Kutia hamasa jamii

Fasihi hutia hamasa kuhusiana na mambo mbalimbali yanayotendeka katika jamii. Mathalani, riwaya ya *Pepo ya Mabwege* (Mwakyembe, 1980) inatia hamasa kwa vijana kusimamia kile wanachokiamini. Mhusika Kalenga alisimama kidete kufichua uozo uliomo kwenye jamii, na hatimaye alipandishwa cheo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya. Vilevile, kazi nyingine za fasihi kama nyimbo zimekuwa zikitumika kutia hamasa ya wanawake kufanya kazi ili kujiletea maendeleo bila kuwa wategemezi katika jamii.

(g) Kukosoa jamii

Fasihi ina mchango katika kukosoa jamii kuhusiana na mambo mbalimbali ya maisha. Kwa mfano, katika riwaya ya *Kufikirika* (Robert, 1968), mwandishi anakosoa tabaka tawala linalotumia rasilimali nyingi kwa manufaa ya watu wachache ilihali wanamajimii wengine wanateseka. Halikadhalika, methali katika fasihi hutumika kukosoa au kuonya jamii. Methali kama vile "Mkataa pema, pabaya panamwita" inakosoa mtu anayekataa wosia mzuri kwani kuna madhara yanaweza kumpata. Aidha, methali kama "Tamaa mbele, mauti nyuma" imekusudiwa kuwaonya wanajamii kuepuka tamaa kwani mtu mwenye tamaa anaweza kukabiliwa na madhara.

(h) Kukomboa jamii

Fasihi simulizi na fasihi andishi imechangia sana kupiga vita masuala mbalimbali yanayokwamisha maendeleo ya jamii kama vile ujinga, maradhi na umaskini. Tamthiliya ya *Hawala ya Fedha* (Lihamba, 1985), kwa mfano, inaeleza mambo yanayosababisha umaskini ambayo ni ujinga na uvivu. Aidha, wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika, baadhi ya bendi za muziki wa dansi zillipiga nyimbo za kuwaunganisha watu kwa ajili ya ukombozi. Mfano mzuri wa wimbo wa "Mwenyekiti Mwalimu Nyerere" ulioimbwa na bendi ya *Urafiki Jazz miaka ya 1970* wimbo huo ulikuwa ukimsihi mwenyekiti wa nchi tano zilizo mstari wa mbele kupigania ukombozi wa Kusini mwa Afrika azidishe mapambano kwani maadui wa Afrika walilisumbua sana Bara la Afrika.

Shughuli ya 2.19

(a) Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, jadili mchango wa fasihi andishi ya Kiswahili katika jamii.

(b) Jadili uhusiano uliopo baina ya fasihi simulizi na fasihi andishi.

www.learninghubtz.co.tz

Tamrini

1. Kwa kutumia mifano, eleza namna sayansi na teknolojia zinavyochangia katika kukuza fasihi simulizi na andishi.

2. Fafanua tofauti kati ya maigizo na tamthiliya andishi ya Kiswahili.

3. Jadili jinsi utanzu wa semi unavyosaidia kuimarisha tanzu nyingine za fasihi simulizi.

4. Kwa kutumia mifano, eleza namna fasihi simulizi na fasihi andishi zinavyochangia kukuza maendeleo ya kijamii.

5. Eleza namna ushairi simulizi ulivyochangia katika kukua kwa ushairi andishi.

6. Kwa kutumia mifano, eleza namna sayansi na teknolojia inavyokuza fasihi simulizi na andishi.

7. Jadili maendeleo ya ushairi kwa kuzingatia vipindi mbalimbali.

8. "Bila fasihi simulizi hakuna fasihi andishi". Jadili kauli.

9. Katika orodha uliyopewa, chagua waandishi wawili wa tanzu tofauti kisha ueleze mchango wa kila mmoja wao katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

  1. Shaaban Robert
  2. Euphrase Kezilahabi
  3. Mugyabuso Mulokozi
  4. Mohammed Said Abdulla
  5. Eric Shigongo
  6. Gabriel Ruhumbika
  7. Zainabu Mwanga
  8. Penina Muhando
  9. Muhammed Seif Khatib

10. "Michezo ya watoto haina umuhimu wowote katika makuzi yao". Jadili kauli hii kwa kutumia mifano maridhawa.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256