Sura Ya 01 : Historia utambulisho na maadili ya taifa
| Utangulizi Taarifa za kihistoria, utambulisho na maadili ya taifa ni sehemu muhimu katika kufahamu hatua mbalimbali za kimaendeleo zilizopitiwa na taifa. Katika sura hii, utajifunza kuhusu uhusiano wa kinadharia kati ya historia, utambulisho na maadili ya taifa, misingi ya historia iliyounda utambulisho na maadili ya taifa na nafasi ya historia na maadili katika kujenga fahari ya taifa. Vilevile, utajifunza kuhusu nafasi ya tunu za taifa na maadili katika kuijenga misingi ya uongozi bora na mikakati ya kuilinda historia, utambulisho na maadili ya taifa. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuithamini historia, utambulisho na maadili ya taifa la Tanzania na kuishi kwa kuyafuata |
| Dhana za historia, utambulisho na maadili ya taifa Dhana za historia, utambulisho na maadili ya taifa ni pana na zinatofautiana kulingana na historia ya taifa linalohusika. Kwa upande wa taifa la Tanzania, dhana hizi zinamaanisha yafuatayo: |
Historia ya taifa
Historia ni maarifa yanayotokana na shughuli na matukio yaliyoathiri jamii fulani kwa sehemu kubwa wakati uliopita. Athari hizo zinaweza kuwa chanya au hasi. Pia, historia ni simulizi za utaratibu wa matukio ya zamani kama yanavyohusiana na mtu au watu wa aina fulani, nchi au kipindi fulani, ambazo zilitolewa kwa njia ya masimulizi. Siku hizi matukio hayo tunayasoma kwenye vitabu na majarida mbalimbali. Aidha, historia ni uchambuzi au uchunguzi wa yale yaliyotokea siku za nyuma ili kujua ni lini yalitokea na ni nini kilisababisha kutokea kwake na matokeo yake yalikuwa ni nini. Kwa mantiki hii, historia inakuwa ni uchambuzi wa matukio yanayoweza kuepukika na yaliyoweza kukubalika katika maisha ya binadamu huko nyuma. Kwa maneno mengine, historia ni jitihada za binadamu kufikiria upya yaliyopita kwa nia ya kuboresha maisha ya kizazi kilichopo. Historia ya taifa haihusishi tu simulizi au maarifa ya kuanza na kukua kwake bali inahusisha pia matukio mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo ama yalilijenga, yalilidhoofisha au yalilisambaratisha taifa au jamii. Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na maisha na maendeleo ya watu wa kale, vita, njaa, biashara ya utumwa, ukoloni, na uhuru.
| Fikiri Unavyoweza kujitofautisha na watu wa mataifa mengine. |
Utambulisho wa taifa
Utambulisho ni hali, ishara au alama zinazobainisha tofauti kati ya kitu kimoja na kingine, mtu mmoja na mwingine au jamii moja na nyingine. Kwa ngazi ya mtu binafsi, utambulisho ni jumla ya vigezo mbalimbali kama vile jina, ukoo, mila na desturi, uzoefu, muonekano, maumbile, uhusiano na maadili ambayo huunda utu wa mtu kama alivyo yeye mwenyewe kwa ndani na si kama watu wanavyosema juu yake. Kwa ngazi ya jamii au taifa, utambulisho unahusisha masuala mengi yakiwemo masuala ya mipaka ya nchi, tunu za taifa, utamaduni wa wananchi wa taifa linalohusika, itikadi ya taifa, rangi, makabila, dini, asili ya taifa au jamii, hatua za maendeleo, uwezo wa kisayansi na teknolojia ya taifa na hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Utambulisho wa taifa unajumuisha pia sanaa, lugha, mavazi, michezo, dini pamoja na mila na desturi. Taifa la Tanzania linatambulishwa na alama mbalimbali ikiwa ni pamoja na bendera ya taifa, wimbo wa taifa, nembo ya taifa, na fedha.
Maadili ya taifa
Dhana ya maadili inahusisha sheria, kanuni, misingi, ukweli, na imani au namna ya kufikiri ambayo inaongoza au inayosadikiwa kuongoza matendo ya watu katika jamii au taifa. Hivi karibuni, hasa baada ya kushamiri kwa usasa kupitia utandawazi, neno hili maadili limekuwa likitumika pia kuelezea jitihada za binadamu za kutumia akili, na si imani, ili kujua anavyopaswa kuishi kama binadamu na wala si kama wanyama wasiokuwa na utashi. Kwa maneno mengine, maadili yana maana ya kile kinachopaswa kufanyika ili watu wawe na tabia za kibinadamu na ili waishi kama binadamu. Katika muktadha huu, tunu za jamii zinakuwa na umuhimu wa pekee katika dhana ya maadili ya taifa. Tanzania, kama taifa, lina sheria, kanuni na misingi ya maadili inayofanana na mataifa mengine. Kwa mfano, ujasiri, ukweli, uaminifu, upendo, uwajibikaji na uwazi, haviko Tanzania tu bali pia katika mataifa mengine. Lakini pamoja na hayo, Tanzania kama taifa limekuwa likiweka mkazo kwenye taratibu, sheria na misingi inayojenga umoja, usawa, ushirikiano, utu, uhuru na amani.
| Kazi ya kufanya 1.1 Tafuta taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya taarifa ikiwamo mitandao, kisha fafanua maadili mengine ya taifa la Tanzania ambayo hayajaelezwa. |
Uhusiano wa kinadharia kati ya historia, utambulisho na maadili ya taifa
Ingawa dhana za historia, utambulisho na maadili zinaweza kuainishwa tofauti, haina maana kwamba dhana hizo hazihusiani. Kinadharia, kuna uhusiano wa karibu sana kati ya historia na utambulisho wa taifa, historia na maadili ya taifa, na utambulisho na maadili ya taifa.
Uhusiano kati ya historia na utambulisho wa taifa
Kinadharia kuna uhusiano wa karibu sana kati ya historia na utambulisho wa taifa. Ili kuuelewa uhusiano huu kwa usahihi zaidi ni muhimu kufahamu kwanza baadhi ya hali au vitu vinavyolitambulisha taifa la Tanzania. Utambulisho wa taifa letu unahusisha masuala mengi. Hata hivyo, msisitizo utakuwa katika utambulisho wa mipaka, tunu, utamaduni, itikadi, hali ya uchumi, na Bendera ya Taifa.
Jina na mipaka ya nchi
Mojawapo ya vitu vinavyolitambulisha taifa letu ni mipaka ya nchi yetu. Taifa letu, kama ilivyo kwa mataifa mengine, lina ardhi ambayo ina mipaka inayotambulika kimataifa. Jina Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaweza kuwa na maana nyingine lakini kijiografia hurejelea sehemu maalumu yenye mipaka ambayo inapakana na nchi nyingine. Mipaka inayotambulisha nchi yetu ina chimbuko lake katika historia. Mwishoni mwa karne ya 19, mataifa ya Ulaya yalikutana katika mji wa Berlin nchini Ujerumani na kuligawa bara la Afrika. Baadaye, yalifanyika makubaliano kati ya Uingereza na Ujerumani mnamo mwaka 1886 na 1890 ya kuigawa Afrika Mashariki ambapo iliwekwa mipaka iliyotambulisha nchi ya Ujerumani ya Afrika Mashariki (Ruanda-Urundi na Tanzania Bara). Jina hilo lilibadilika kuwa Tanganyika wakati wa utawala wa Waingereza ambapo baada ya uhuru iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania mwaka 1964.
Tunu za Taifa
Tunu ni hali au mambo ya msingi ambayo jamii au taifa linayazingatia na kuyaheshimu. Pamoja na kuzienzi tunu kama vile uhuru na haki, ambazo zinakubalika pia kwa mataifa mengine duniani kuwa ni tunu za ubinadamu, Tanzania imekuwa ikitilia mkazo zaidi tunu za Kiafrika, kama vile umoja, ushirikiano, usawa, undugu, ukarimu, uhuru, na heshima kwa kila mtu. Tunu zote hizi, pamoja na nyingine ambazo hazikutajwa hapa, zilikuwepo tangu zamani katika jamii za mababu na mabibi zetu wa Kiafrika na ndizo ziliwawezesha kuyashinda matatizo yote ya maisha ya wakati wao. Kwa maneno mengine, tunu hizo zimechotwa kutoka katika historia ya mababu na mabibi zetu ili zitusaidie kuboresha maisha yetu ya sasa. Kwa muktadha huu, historia inakuwa ndiyo chimbuko la Tunu za Taifa letu.
Utamaduni
Utamaduni ni mfumo mzima wa maisha ya watu katika jamii au taifa. Kwa ufupi, utamaduni ni mfumo wa maisha ya watu katika jamii inayohusika. Kwa mfano, Watanzania wanaishije? Wanafuata utaratibu upi wa maisha ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii? Wanakula nini? Wanavaaje? Wanaongea lugha gani? Wakifurahi wanafanya nini? Utamaduni ni majibu sahihi ya maswali haya. Aidha, utamaduni unahusisha njia zote za maisha ikiwa ni pamoja na sanaa, imani, kanuni, heshima, mavazi, miiko, lugha, mila na desturi, na taasisi ambazo hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Vilevile, uhusiano kati ya utambulisho wa utamaduni na historia ni rahisi kueleweka kwa sababu utamaduni wa taifa au jamii unatokana na historia ya jamii au taifa lenyewe. Kwa hiyo, historia ndiyo chimbuko la utamaduni wa taifa letu. Kupitia historia, jamii inapata maarifa na thamani ya utamaduni wake. Kwa mfano, ngoma na vyakula vya asili, mavazi, michezo na sanaa, vina historia ndefu inayochangia utambulisho huu wa taifa.
Itikadi ya taifa
Wakati mwingine utambulisho wa taifa unakuwa na itikadi yake. Itikadi ni falsafa inayoongoza maisha ya watu katika jamii au taifa. Kwa kawaida, itikadi inahusisha mawazo, imani, na mitazamo inayokubalika katika jamii inayohusika ambayo inaathiri uelewa wa jamii hiyo kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Tanzania, kwa mfano, iliwahi kutambulika duniani kote kwa itikadi yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Watu walijua kuwa Tanzania ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea. Baadhi ya wasomi wanaandika makala na vitabu kuhusu itikadi hiyo mpaka leo. Uhusiano kati ya ujamaa na historia uko wazi kwani itikadi ya ujamaa ilikuwa na chimbuko lake katika maisha ya familia za Kiafrika za zamani. Maadili na nguzo za itikadi ya ujamaa zilitoka katika historia ya mababu na mabibi zetu ambao waliishi maisha ya kijamaa, maisha ya pamoja na kwa kusaidiana kufanya kazi na kugawana matokeo ya kazi hizo kwa usawa. Kwa hiyo, kwa mara nyingine, historia inajitokeza hapa kama chimbuko la utambulisho wa itikadi ya ujamaa.
Ni muhimu kuzingatia kwamba itikadi ya ujamaa kwa Tanzania iliibuka dhidi ya itikadi ya ubepari ambayo iliwafanya Watanzania wawe watumwa katika nchi yao. Ubepari ulisimamiwa na kutekelezwa na wakoloni wa Kijerumani na Kiingereza. Ubepari uliwanyonya Watanzania, uliwakandamiza, uliwanyanyasa, na kuwapunja. Ndiyo maana Azimio la Arusha la mwaka 1967 liliamua kuachana na ubepari na kuanza kujenga nchi kwa misingi ya kijamaa (ujamaa wa Kiafrika). Hapa pia inaonekana dhahiri kwamba utambulisho wa itikadi yetu ya ujamaa ulikuwa na chimbuko lake katika historia ya ubepari katika nchi yetu ulioletwa kwa kasi na wakoloni wa Kizungu.
Hali ya kiuchumi
Hivi karibuni, na hasa baada ya kukua kwa utandawazi, imekuwa jambo la kawaida kuyatambua mataifa duniani kutokana na uchumi wake. Utambuzi huu uko wa aina mbili: Kuna nchi zilizoendelea (mara nyingi huitwa nchi za ulimwengu wa kwanza, au nchi za viwanda), na kuna nchi maskini (ambazo wakati mwingine huitwa nchi zinazoendelea). Taifa letu linatambulika kama nchi inayoendelea. Mwanzoni mwa miaka ya 1960 hadi mwaka 1985 Tanzania ilitambulika kama nchi maskini. Watu wake walikuwa hawana elimu ya kutosha, hawana mahali pazuri pa kulala, hawana nguo za kutosheleza, chakula, elimu, na huduma za afya zilikuwa duni.
Pamoja na umaskini huo wa uchumi na viwanda, nchi yetu ilikuwa na rasilimali nyingi, kama ilivyo sasa. Hali ya umaskini inatokana na historia ndefu ya unyonyaji na mataifa ya nje kwa miaka mingi pamoja na kuendekezwa kwa vitendo visivyo vya kimaadili kama vile rushwa. Vitendo hivi vinajenga matabaka katika jamii ya walionacho, ambao wanajilimbikizia mali kwa njia ya rushwa na wasionacho, ambao rasilimali zao zinachukuliwa na wala rushwa. Kiuhalisia, unyonyaji na vitendo vya rushwa vinaendelea hadi leo kupitia ukoloni mamboleo na watu wachache wanaendelea kujilimbikizia mali na kuwa na matumizi mabaya ya ofisi. Kwa hiyo, utambulisho wetu wa umaskini wa viwanda na uchumi una chimbuko lake katika matukio ya kihistoria.
| Kazi ya kufanya 1.2 Tafuta taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwamo mitandao, kuhusu Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 – 1885 uliogawa bara la Afrika, kisha eleza mchango wake katika kuujenga utambulisho wa taifa la Tanzania. |
Uhusiano kati ya historia na maadili ya taifa
Kinachoitwa maadili ya taifa ni sheria, kanuni, ukweli, misingi, mawazo na tunu zinazoongoza maisha, matendo na tabia za watu katika taifa letu. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya historia na maadili ya taifa hususani sheria, kanuni na misingi inayosimamia uhuru. Maadili ya taifa ni mengi lakini mkazo utakuwa katika tunu za taifa zifuatazo: uhuru, usawa, umoja, utu na undugu, uadilifu, uwazi na uwajibikaji na amani.
Uhuru
Kwa upande mmoja uhuru una chimbuko lake katika historia ya ukoloni na kwa upande mwingine uhuru ndiyo chimbuko la historia. Uhuru, ambao ni hali ya mtu au watu wa jamii moja kutotawaliwa na mtu au kikundi cha watu wengine, ulitafutwa na Watanzania wenyewe. Sababu ni kwamba, huko nyuma, kuanzia karne ya 16 hadi mwanzoni mwa nusu ya pili ya karne ya 20, tulikuwa tumepuuzwa, tumenyanyaswa, na kudharauliwa kwa sababu ya biashara ya utumwa na ukoloni mkongwe. Uhuru ulikuja kama jibu la kukataa hali mbaya ya kutawaliwa na Wazungu. Kwa mtazamo huu, inaonekana wazi kwamba uhuru una chimbuko lake katika historia ya utumwa na ukoloni mkongwe katika kipindi cha karne ya 19 na 20.
Vilevile, uhuru ni matokeo ya historia yenyewe. Historia ina chanzo chake katika matendo au matukio ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na binadamu. Watu wanapoona maisha fulani ni mabaya hupenda kuyabadilisha ama kwa njia za amani au kwa njia ya vita. Watanzania walipoona maisha ya kutawaliwa na Uingereza ni mabaya, waliamua kupigania uhuru, ambao hatimaye wakaupata kutoka kwa Waingereza. Uamuzi na matendo ya kuutafuta uhuru yalikuwa uamuzi mzuri na huru. Hakuna mtu aliyewalazimisha waasisi wa taifa letu kufanya uamuzi wa kuupigania uhuru, au kuweka mikakati ya kuomba uhuru. Wapigania uhuru walitekeleza mikakati hiyo kwa uhuru, bila shuruti wala kulazimishwa na watu wengine. Aidha, baada ya Tanzania kuwa huru ilikuwa kinara wa kuzisaidia kutafuta uhuru nchi nyingine zilizopo kusini mwa bara la Afrika kama vile Msumbiji, Angola, Namibia, Zimbabwe na Afrika ya Kusini.
Kwa kufanya uamuzi huru na kushiriki kwa hiari na utashi wao katika shughuli za kutafuta uhuru, waasisi wa taifa letu walitengeneza historia ya nchi yetu. Kuliangalia suala hili kwa mtazamo huu, kunasaidia kuelewa kwamba uhuru ni chimbuko la historia. Hivyo, historia na maadili ni maarifa yanayotegemeana kwa sababu uhuru una chimbuko lake katika historia na historia ina chimbuko lake katika uhuru. Uhusiano baina ya dhana hizi si uhusiano tegemezi, bali ni uhusiano wa kutegemeana.
Usawa
Hii ni hali ya kutokubaguana kwa misingi ya rangi, ukabila, dini, au itikadi. Katika taifa letu, hii ni tunu muhimu na ya kuenzi kwa sababu ya historia yetu ya kutengwa na kubaguliwa kwa sababu ya rangi yetu. Watawala wa kikoloni walijenga matabaka kwa misingi ya rangi. Tabaka la kwanza lilikuwa la Wazungu, la pili lilikuwa tabaka la Waasia (Wahindi na Waarabu), na tabaka la tatu lilikuwa la Waafrika (Watanzania). Waafrika walinyanyaswa, walidharauliwa, na walipuuzwa kwa sababu tu ya rangi yao nyeusi. Baada ya uhuru matabaka hayo yote yalifutwa kwa kuamini kwamba binadamu wote ni sawa, licha ya tofauti za rangi yao. Hata hivyo, tusipokuwa makini kama taifa na tunu hii ya usawa isipolindwa kwa kupambana na vitendo vya rushwa, matabaka yaanza kujitokeza tena. Hii ni kutokana na watu wachache kuendelea kuhodhi utajiri unaotokana na mali zilizopatikana kwa njia za rushwa na kuwepo kwa tabaka lingine la wanyonge wasionacho. Hapa pia tunaona kwamba usawa, sheria na kanuni zinazolinda uhuru hutokana na historia ya kubaguliwa kwa sababu ya rangi. Hata hivyo, uamuzi wa kujenga jamii yenye usawa haukudondoka kutoka hewani. Waasisi wa taifa letu waliangalia katika mila na tamaduni za Kiafrika wakagundua kwamba mababu na mabibi zetu walikuwa hawana sera za kubaguana kwa misingi ya rangi, dini au wenye nacho na wasionacho. Katika hili tunaona pia kwamba historia, ama ya ukoloni au ya mila na desturi zetu, ndiyo chimbuko la maadili ya usawa.
Umoja
Umoja ni hali ya watu mbalimbali kuwa wamoja katika nia na matendo. Waswahili wana msemo usemao, "Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu." Maarifa na hekima hii hutokana na hekima za mababu na mabibi zetu huko nyuma, ambao umoja kati yao uliwasaidia kutatua changamoto nyingi katika mazingira yao ambapo mtu mmoja mmoja asinge weza kufanikiwa. Sera za kikoloni zilififisha umoja waliokuwa nao mababu na mabibi zetu. Hata hivyo, umoja ulitumika katika kupigania uhuru hadi ulipopatikana. Hii inaonesha kwamba
Ukurasa wa Kushoto:
maadili au tunu ya umoja ina chanzo chake katika historia ya mababu na mabibi zetu na katika historia ya kudai uhuru. Umoja ulitokea kama jibu kwa jamii ambayo huko nyuma ilikuwa imeparaganyika na ambayo ilikuwa imegawanyika kwa sababu ya sera za kikoloni. Waasisi wa taifa letu waliamua kuliunganisha taifa ili liwe na umoja na mshikamano, ambao ulikuwa nguzo muhimu katika kuleta maendeleo mara baada ya uhuru. Kama zilivyo tunu zingine, umoja na mshikamano vinaweza kuharibiwa na ukosefu wa maadili na kuendekezewa vitendo visivyo vya kimaadili kama rushwa, ubinafsi na wizi, ambayo vinaweza kuleta utengano katika taifa la Tanzania.
Utu na undugu
Kabla ya ukoloni, jamii zetu zilikuwa zikiishi kama ndugu wanaoyajali pamoja katika familia. Watu waliishi pamoja katika familia au ukoo na kufanya kazi pamoja kwa faida ya kila mmoja. Palipokuwa na shida walisaidiana na palipokuwa na matatizo makubwa walishirikiana kuyatatua. Kila mmoja alishiriki katika shughuli za kifamilia au ukoo. Aidha, walikuwa wanajaliana sana; kwa mfano, kama msiba ukitokea, basi ulikuwa msiba wa wote na kila mmoja alishiriki kwa hali na mali. Jamii ilishiriki katika malezi ya watoto na vijana wote, bila kujali hali ya kiuchumi na kisiasa ya anayehusika. Watoto walikuwa wa jamii na yeyote aliyekiuka maadili yale alirekebishwa. Mfumo huu wa maisha una asili yake katika historia ya mila na desturi za Watanzania. Kwa hiyo, inaonekana wazi kabisa kwamba historia ndiyo chimbuko la maadili, ambayo yakienziwa vizuri yatalisaidia taifa na jamii katika kuleta maendeleo. Hii ni kwa sababu, kama ilivyokuwa zamani, watakaokiuka maadili watarekebishwa na jamii nzima. Hivyo, jamii yenyewe inapaswa kusimama imara na kushiriki katika kukemea vitendo vya wale wanaokiuka maadili kama vile wezi wa mali ya umma na wala rushwa.
Aman
Hii ni hali ya watu kuishi bila mafarakano ya kivita, vurugu au fujo. Ni hali ya kuishi katika taifa kwa maelewano bila migogoro, uadui au chuki. Pia, ni hali ya watu kuishi kwa usalama. Hii hali ya amani ina sheria, kanuni, taratibu na misingi yake. Tunu ya amani na sheria na kanuni zake ina chanzo chake pia katika historia. Uzoefu unaonesha kwamba palipo na umaskini, ukatili, njaa, ubaguzi, rushwa, utawala wa mabavu, na uvunjaji wa haki za binadamu hapana amani. Amani iliyopo sasa katika taifa letu ina chimbuko lake kihistoria kwani wazee wetu waliishi kwa upendo na kutobaguana. Makabila mbalimbali yalifanya biashara bila kudhulumiana wala kuoneana. Vilevile, waasisi wa taifa letu waliunganika taifa na kukataa misingi ya unyonyaji au ubaguzi kwa kuangalia dini, kabila au eneo la kijiografia. Hivyo, ni dhahiri kwamba amani ya taifa letu chanzo chake ni historia ya Watanzania.
Kwa ujumla, uhusiano kati ya historia na maadili ya taifa ni sawa na uhusiano wa wazazi na wana wao. Kama vile baba na mama wanavyozaa mtoto na kumlea hadi anakuwa mtu mzima ndivyo ilivyo katika maadili na historia. Historia ni chimbuko na nguzo imara katika kuyaendeleza na kuyadumisha maadili ya taifa. Kupitia historia ya taifa, watu wanapata ufahamu wa thamani ya maadili yao ya asili na kuyaweka katika vitendo katika maisha yao ya kila siku.
| Kazi ya kufanya 1.3 Tafuta taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwamo mitandao, kisha fafanua kwa nini uhuru, usawa, umoja, undugu na amani ni sehemu ya maadili ya taifa la Tanzania. |
Uhusiano kati ya utambulisho na maadili ya taifa
Utambulisho wa taifa kama ulivyoainishwa hapa ni pamoja na zile sheria, kanuni na misingi inayolinda mipaka, tunu za taifa, utamaduni, itikadi, na hali ya uchumi. Ili kuelewa vizuri na kwa ufasaha uhusiano uliopo kati ya utambulisho na maadili, itakuwa vyema kulinganisha utambulisho ulioainishwa hapa na maadili yaliyobainishwa hapa, ambayo ni uhuru na mipaka, usawa na utamaduni, na umoja na hali ya uchumi.
Uhuru na mipaka
Mara nyingi si rahisi kuona uhusiano uliopo kati ya uhuru na mipaka ya taifa letu kwa haraka haraka. Hata hivyo, ukiangalia kwa makini utaona kwamba kuna uhusiano wa karibu sana kati ya masuala hayo mawili. Uhuru ni hali ya mtu au watu wa jamii moja kutotawaliwa na mtu au kikundi cha watu wengine. Watu hao au jamii hiyo ni lazima iwe kwenye eneo lenye mipaka yake. Kwa upande wa taifa, mipaka hiyo lazima iwe inaonekana na kutambuliwa duniani.
Uhuru lazima uwe katika eneo maalum au nchi inayohusika na ni lazima kuwe na mipaka. Kwa hiyo, kwa maneno mengine, maana ya uhuru inatofautiana kutoka eneo moja hadi lingine, mathalani, namna Tanzania inavyotafsiri uhuru inaweza kuwa tofauti na namna Kenya inavyotafsiri uhuru wake. Kinachofunga uhuru ndani ya eneo maalumu liitwalo Tanzania ni mipaka. Kwa lugha nyingine, mipaka inaulinda uhuru wetu. Hata hivyo, mipaka ya kijiografia inaweka uzio au ukuta tu bali walinzi halisi wa uhuru wa Tanzania ni Watanzania wenyewe. Kwa kuwa Watanzania wako ndani ya mipaka inayoeleweka na kwa kuwa mipaka hiyo inawafanya wajisikie wamoja, wanakuwa na shauku ya kulinda uhuru wao ndani ya mipaka ya nchi yao. Kwa hiyo, ni sahihi kusema uhuru na mipaka ni dhana zinazotegemeana. Dhana moja haiwezi kufanya kazi bila kuwapo kwa dhana nyingine. Hivyo, uhusiano kati ya utambulisho wa taifa na maadili ya taifa si uhusiano tegemezi, ambapo kimoja kinategemea tu kingine, bali ni uhusiano wa kutegemeana.
Usawa na utamaduni
Sheria na kanuni zinazolinda usawa zina uhusiano wa karibu sana na utamaduni, hasa pale utamaduni unapoeleweka kama namna au jinsi Watanzania wanavyoyakabili maisha katika taifa lao. Usawa kama dhana inayosititiza zaidi haki za binadamu unasaidia kuhakikisha kuwa utamaduni unaolitambulisha taifa letu hauvunji haki za binadamu kama vile kunyanyasa watoto, kubagua watu kwa misingi ya rangi, au hata kuwanyima baadhi ya wananchi haki ya elimu kwa sababu yoyote ile. Kwa mantiki hii, usawa unaufanya utamaduni wetu uwe na maadili yanayokubalika duniani. Hivyo, usawa ni chanzo cha maadili katika utambulisho wa utamaduni. Pia, ni muhimu kuelewa kwamba utamaduni wetu ndio chimbuko la maadili ya usawa. Kama ilivyogusiwa hapo awali, tunu ya usawa imetoka kwenye historia ya mababu na mabibi zetu pamoja na uzoefu wetu wa ukoloni. Kwa hiyo, uhusiano kati ya usawa na utamaduni ni uhusiano unaotegemeana. Uhusiano kati ya usawa na utamaduni hauwezi kukamilika bila kuwapo kwa kimojawapo. Hivyo, utambulisho na maadili vinategemeana pia.
Umoja na hali ya uchumi
Imeelezwa hapo mwanzo kwamba kuna wakati taifa letu liliwahi kujitambulisha na kutambuliwa ndani na nje ya nchi kwamba ni taifa maskini. Hata hivyo, Tanzania imekuwa ikijitambulisha na kutambuliwa na watu wa nje na ndani ya nchi kwamba ni taifa tajiri, hasa kwa kuzingatia utajiri wa maliasili uliopo nchini. Uhusiano wa utambulisho huu na umoja si mgumu kuuelezea. Sheria na kanuni za umoja zina uwezo wa kubadilisha hali ya uchumi kutoka hali ya umaskini hadi utajiri. Kwa wakati umoja na katika nia na matendo unaweza kuuondoa umaskini. Kwa kushirikisha vipawa na karama za kila mmoja katika taifa, inawezekana kupata utaalamu na uwezo wa kuitoa nchi katika dimbwi la umaskini. Kwa mantiki hii, umoja unakuwa nguzo na chimbuko la maendeleo, kwa maana ya utajiri. Pia, umoja ni kigezo cha kupima hali ya uchumi kwani unagawa watu katika taifa, kwenye tabaka la walionacho na wasionacho. Ikiwa uchumi haujengi matabaka na unawasaidia watu wote katika taifa kuishi maisha bora, basi uchumi wa aina hiyo unaosadikiwa kwanza ni mzuri. Katika hili, inaonekana pia kwamba umoja na hali ya uchumi vinategemeana. Umoja unajenga na kulinda uchumi na uchumi unaweza kulinda umoja au kuusambaratisha.
Zoezi
1. "Uhusiano kati ya utambulisho wa taifa na maadili ya taifa si uhusiano tegemezi". Fafanua maana ya kauli hii.
2. Kwa kutumia mifano, eleza dhana ya utambulisho wa taifa la Tanzania.
3. Eleza kwa nini maadili ni suala la kihistoria.
4. Tathmini mchango wa historia katika ujenzi wa tunu za taifa la Tanzania.
5. Kwa kutumia mifano mbalimbali, eleza ni kwa namna gani Watanzania wanaweza kunufaika kwa kutumia historia ya taifa.
6. Kwa kutumia mifano, eleza mchango unaotokana na misingi ya historia ya utambulisho na maadili ya taifa.
7. Fafanua namna vitendo vya rushwa vinavyoweza kuleta umaskini, matabaka katika jamii, na kuathiri amani na kuvunja haki za binadamu.
8. "Taifa lolote lisilo na historia ni sawa na binadamu ambaye hajajitambua." Jadili ukweli wa hoja hii.
Misingi ya kihistoria iliyounda utambulisho wa taifa
Taifa letu linatambulishwa na linatambuliwa ndani na nje ya nchi na vitu mbalimbali. Baadhi ya vitu hivyo ni mipaka yake, utamaduni, bendera, lugha ya Kiswahili, na wimbo wa taifa.
www.learninghubtz.co.tz
Zoezi
1. "Uhusiano kati ya utambulisho wa taifa na maadili ya taifa si uhusiano tegemezi". Fafanua maana ya kauli hii.
2. Kwa kutumia mifano, eleza dhana ya utambulisho wa taifa la Tanzania.
3. Eleza kwa nini maadili ni suala la kihistoria.
4. Tathmini mchango wa historia katika ujenzi wa tunu za taifa la Tanzania.
5. Kwa kutumia mifano mbalimbali, eleza ni kwa namna gani Watanzania wanaweza kunufaika kwa kutumia historia ya taifa.
6. Kwa kutumia mifano, eleza mchango unaotokana na misingi ya historia ya utambulisho na maadili ya taifa.
7. Fafanua namna vitendo vya rushwa vinavyoweza kuleta umaskini, matabaka katika jamii, na kuathiri amani na kuvunja haki za binadamu.
8. "Taifa lolote lisilo na historia ni sawa na binadamu ambaye hajajitambua." Jadili ukweli wa hoja hii.
Misingi ya kihistoria iliyounda utambulisho wa taifa
Taifa letu linatambulishwa na linatambuliwa ndani na nje ya nchi na vitu mbalimbali. Baadhi ya vitu hivyo ni mipaka yake, utamaduni, bendera, lugha ya Kiswahili, na wimbo wa taifa.
Mipaka ya nchi
Mipaka ya nchi yetu, ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo utambulisho wa nchi yetu, inatokana na tukio la kihistoria. Kati ya mwaka 1884 na 1885 mataifa ya Ulaya Magharibi yaliligawa bara la Afrika katika vipande vipande kama nchi, katika mkutano uliofanyika katika mji wa Berlin huko Ujerumani. Wakati nchi nyingi za Afrika zikigawanywa katika mkutano huo, kama ilivyosemwa hapo awali, Afrika Mashariki iligawanywa baada ya mkutano huo kupitia makubaliano ya Uingereza na Ujerumani mwaka 1886 na 1890. Katika miaka hii Tanzania Bara ya sasa iligawiwa kwa Ujerumani kama moja ya sehemu ya Ujerumani ya Afrika Mashariki na mara baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilikuwa koloni la Uingereza na kubadili jina kuwa Tanganyika mnamo mwaka 1920. Zanzibar iligawiwa kwa Uingereza. Kama ilivyokuwa kwenye Mkutano wa Berlin, mipaka waliyoiweka haya mataifa ya Ulaya ndiyo ikawa mipaka ya nchi za Afrika na Tanzania ya leo inayotambulika kimataifa. Baada ya uhuru, jitihada zilifanyika kuvunja athari mbaya za mipaka ya kikoloni na kuunda Afrika moja. Pamoja na kusuasua kwa umoja wa Afrika, Tanganyika iliweza kuvunja mipaka ya kikoloni na kuungana na Zanzibar, tukio ambalo liliondoa kabisa mipaka ya kikoloni baina ya nchi hizi mbili na kuunda utambulisho wa taifa jipya la Tanzania mwaka 1964. Kwa hiyo, tunaweza kusema kuwa utambulisho (kwa maana ya mipaka ya nchi) wa taifa letu umeundwa na matukio ya kihistoria ya mataifa ya Ulaya Magharibi kwa kuigawa Afrika na Afrika Mashariki pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Utamaduni
Kipengele kingine cha utambulisho wa taifa ni utamaduni. Tanzania ni nchi mojawapo inayojivunia aina mbalimbali za tamaduni. Hii ina maana kwamba Tanzania ni nchi yenye utamaduni mseto, kwa maana kwamba imeundwa na watu wenye tamaduni mbalimbali zinazotokana na jamii mbalimbali kuishi pamoja bila kujali tofauti zao. Inasadikiwa kwamba Tanzania ina makabila zaidi ya 150, ambapo kila moja lina utamaduni wake. Hata hivyo, kuna baadhi ya mila na desturi katika makabila haya zinazofanana.
Misingi ya kihistoria iliyofanya Tanzania ijulikane kama taifa lenye tamaduni nyingi ni uhamiaji wa makundi mbalimbali ya watu kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Uhamiaji huo, uliotokea katikati ya milenia ya 2 kabla ya zama za sasa na milenia ya kwanza ya zama za sasa na kuendelea.
Wakati Wakichembe wakiaminika kuwa ni wenyeji na wazawa wa maeneo haya, makundi yaliyowasili nchini kutoka maeneo mengine, na ambayo yanaifanya Tanzania iwe ni nchi ya makundi yote ya Afrika, ni pamoja na Wanilo, Wakushito na Wabantu. Kundi la Wabantu linawakilishwa na jamii kama vile Wagogo, Wasukuma, Wamakonde, Wahehe, Wachaga na makabila mengine. Wakichembe wanajumuisha makabila ya Wasandawe na Wahadzabe, ambao wanapatikana katika bonde la ufa, kandokando ya Ziwa Eyasi na mbuga ya Serengeti. Aidha, Wanilo chimbuko lao ni mto Nile huko Sudan. Hapa Tanzania Wanilo ni Wamasai, Wajaluo na Wadatoga. Wakushito wanawakilishwa na makabila kama vile Walawa, Wagorowa, Waburungi, Wafyomi na Wairaqw ambao waliingia nchini kutoa pembe ya Afrika, yaani Ethiopia, Eritrea na Somalia.
Bendera ya Taifa
Bendera ni alama ya utambulisho wa taifa. Mataifa karibu yote duniani yana bendera zake na hujitambulisha kupitia bendera hizo. Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine, ina bendera yake ambayo inatambulika kwa rangi zake. Bendera yetu ni sehemu ya utamaduni au mapokeo ya siku nyingi kwamba nchi huru lazima iwe na bendera yake.
Bendera kama utambulisho wa taifa ina misingi yake katika historia. Tukio la kwanza la kihistoria lilikuwa mwisho wa ukoloni mkongwe na tukio la pili la kihistoria lilikuwa mwanzo wa uhuru wa kujitawala kama taifa huru. Kama alama au utambulisho wa taifa, bendera ina ujumbe mzito sana. Upeperushaji wa bendera unatoa ujumbe kwamba taifa liko hai na kwamba taifa au nchi siyo kitu bandia bali ni kitu halisi kinachojitegemea na hakuna kitu kingine cha kufanana nacho.
Utambulisho wa bendera unatumika katika matukio maalumu ya kitaifa na katika taasisi za kiserikali na binafsi kama vile shule na hospitali. Matumizi na utunzaji wake huashiria kwamba bendera ni kitu cha kudumu na chenye thamani na kwamba, kama nchi au taifa litakuwepo, basi na utambulisho huo utakuwepo siku zote. Isitoshe, bendera ni kitu kinachoheshimika sana kwa taifa. Hali hii ndiyo inayofanya iwe na sheria na kanuni zake. Sheria na taratibu zote zinazohusu bendera zinakusudia kuwaeleza wananchi kuhusu heshima yake. Kwa kuisimamisha bendera juu ya ardhi kuipeperusha juu kabisa ya mlingoti, kuwataka wananchi waiheshimu, kusimama wima mbele yake inapopandishwa au kushushwa, na kuapa utii kwenye bendera humaanisha kwamba taifa linatangaza kuwa na madaraka ya mwisho juu ya watu wake na kuwa ni dola huru.
Ukiacha ujumbe unaotolewa na rangi, bendera pia ni alama ya uhai wa taifa, kudumu kwake, heshima na madaraka yake. Haya yote yana misingi yake katika historia kwani huko nyuma nchi zilikuwa zinachukuliwa kama kitu cha bandia, kisichokuwa na uhai, na ambacho kinapita. Kwa hiyo, nchi zilionekana kuwa hazina madaraka wala heshima yoyote. Hali hii ilisababisha vita ya mara kwa mara na ya muda mrefu huko Ulaya hata kusababisha kuwapo kwa Mkataba wa Westphalia wa 1648. Katika mkataba huo, pamoja na mambo mengine, viongozi wa nchi na dini waliazimia kutenganisha dini na siasa pamoja na nchi moja kuacha kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Kwa maneno mengine, walikubaliana kuheshimu mipaka ya nchi zao na kuondoa masuala ya dini katika uendeshaji wa nchi za Ulaya.
Lugha ya Kiswahili
Lugha ya Kiswahili ni alama muhimu sana inayoitambulisha Tanzania. Ingawa Kiswahili ni lugha ya Kibantu na inazungumzwa na watu wengi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, Tanzania ndiyo inatambulika zaidi kwa Kiswahili sanifu. Utambulisho huu maalumu haukuzuka tu bali una chimbuko lake katika historia ya Tanzania. Mwingiliano ulichangia kukieneza na kukikuza zaidi Kiswahili ambacho tayari kilikuwapo na kuzungumzwa kwa lahaja mbalimbali. Kiswahili kilienea zaidi Tanzania kwani Waarabu walitumia zaidi Kiunguja kilichozungumzwa Unguja ambacho ndicho kilisanifishwa na kuwa sanifu. Kwa hiyo, tukio la kihistoria lililochangia kukieneza na kukikuza Kiswahili, utambulisho wa taifa letu, ni mwingiliano wa kibiashara kati ya Waarabu na watu wa pwani ya bahari ya Hindi, hasa visiwa vya Zanzibar, maeneo ya Bagamoyo na Kilwa. Pamoja na Waarabu, uhusiano na mataifa mengine ya Ulaya umechangia pia katika kukuza msamiati wa lugha hii adhimu na alama muhimu kwa nchi ya Tanzania.
| Kazi ya kufanya 1.4 Soma matini kuhusu makubaliano ya mkutano wa Westphalia kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwamo mitandao, kisha fafanua makubaliano ya mkutano huo na umuhimu wake katika ujenzi wa utaifa. |
Misingi ya kihistoria iliyounda maadili ya taifa
Misingi ya kihistoria iliyojenga maadili ya taifa iko mingi, lakini hapa inaelezewa misingi ifuatayo: utumwa, ukoloni, na Azimio la Arusha.
Utumwa
Kati ya matukio ya kihistoria yaliyochangia sana uundaji wa maadili ya taifa ni biashara ya utumwa wa Waafrika iliyofanyika kwenye karne ya 16 hadi 19. Biashara hii iliwahusisha Waarabu na Wazungu wa Ulaya Magharibi na washirika wao wengine. Biashara hii iliwadhalilisha sana watu wenye rangi nyeusi na ikawanyima utu wao kama binadamu wengine. Watumwa walisafirishwa kwa ukatili wa kutisha ndani (Zanzibar kwenye mashamba ya minazi na karafuu) na nje ya bara la Afrika ili wakafanye kazi kwenye mashamba ya miwa, katani, pamba, kahawa na chai bila ujira wowote. Vilevile, watumwa walisafirishwa kwenda Uarabuni kufanya kazi za ndani. Kiuhalisia, watumwa walikosa haki zao zote za msingi kama binadamu.
Mfumo huu wa maisha ambao uliwatumikisha watu wengine uliwachukiza sana wapigania uhuru wa Afrika. Baada ya kupata uhuru, waasisi wa taifa letu walipiga marufuku mfumo huu wa maisha na walitunga sheria ambazo zililikataza mtu au kikundi cha watu kuwatumikisha watu wengine kwa kuwafanya watumwa. Ili kuzuia utaratibu huo kuigwa, waasisi walitilia mkazo matendo ya haki, usawa, na heshima kwa watu wote. Kwa namna ya pekee kabisa, walitilia mkazo tamko rasmi la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu ambalo lilikuwa linasisitiza uhuru wa kila binadamu.
Ukoloni
Ujio wa wakoloni ulikuwa tukio kubwa la kihistoria ambalo liliathiri kwa kiasi kikubwa maadili ya Watanzania. Wakoloni walipofika walichukua madaraka yote ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kijamii, wakoloni walianzisha elimu ya kikoloni yenye mtazamo wa kimagharibi, walisaidia kuenea kwa dini ya Ukristo, na mambo mengi yenye mrengo wa kimagharibi. Kisiasa, wakoloni ndio walikuwa watawala na wenye madaraka ya mwisho katika koloni. Walianzisha majeshi mbalimbali kama jeshi la polisi, jeshi la kulinda nchi, usalama wa taifa, na jeshi la magereza. Pia, walianzisha bunge na mahakama. Kiuchumi walikuja na utaalamu wa taasisi za mabenki na viwanda. Vilevile, walipora ardhi iliyokuwa inamilikiwa na wenyeji na kuanzisha mashamba makubwa ya mkonge, kahawa, chai, miwa, pamba, pareto, na mengineyo. Kwa kifupi, ukoloni ulikamata njia zote kuu za uzalishaji mali, madini, misitu, na maji. Mfumo wote huu wa ukoloni, ulimwacha Mtanzania akiwa mnyonge na asiyejiamini.
Waasisi wa taifa letu hawakupendezwa na mfumo wa maisha ulioanzishwa na wakoloni. Hivyo, baada ya uhuru jitihada za dhati zilifanyika kubadili mtindo huo wa maisha na kuanzisha mfumo mwingine wa haki na usawa. Kisiasa, madaraka yote yalichukuliwa na Watanzania. Watanzania ndio wakawa na madaraka ya mwisho katika nchi. Jeshi la kikoloni lililokuwa linajulikana kama King's African Rifles (KAR) lilibadilishwa na kuitwa Tanganyika African Rifles, mara tu baada ya uhuru, na baadaye lilibadilishwa kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) la mwaka 1964. Polisi na vyombo vyote vya usalama vikawa chini ya Watanzania ili kulinda usalama wa Watanzania na mali zao. Bunge na mahakama vikawa chini ya Watanzania ili kuwahudumia Watanzania.
Aidha, taratibu zilibadilika kwenye mabenki na viwanda zikawa na lengo la kuwahudumia Watanzania na siyo wakoloni. Ubaguzi uliokuwa umeshamiri katika elimu, afya, makazi na ajira ulipigwa marufuku na msisitizo ukawekwa katika maadili ya usawa. Kijamii, hatua zilichukuliwa kufufua utamaduni wa Watanzania na kuuheshimu. Haya yote yalichangia kuunda maadili yaliyotufikisha hapa. Hii inaonesha dhahiri kuwa ukoloni ulichangia kuunda maadili ya taifa. Kufanyika kwa hayo yote baada ya uhuru kunafanya tufikie hitimisho kwamba tukio la kihistoria la uhuru lilichangia kuunda maadili ya taifa.
Azimio la Arusha
Miongoni mwa matukio ya kihistoria yaliyochangia kuunda maadili ya taifa letu ni Azimio la Arusha. Azimio hili lilipitishwa wakati wa mfumo wa chama kimoja na Halmashauri Kuu ya TANU, mwezi Januari 1967. Mnamo tarehe 5 Februari 1967 Azimio hilo lilithibitishwa na Mkutano Mkuu wa TANU. Azimio hilo lilikuwa tamko la kimapinduzi na la kihistoria ambalo lilionesha mwelekeo mpya wa Tanzania huru katika nyanja za siasa, uchumi na kijamii. Lilikuwa tamko rasmi la Watanzania wenyewe kuhusu maendeleo ya nchi yao. Hivyo, ni tukio lililobadili mwelekeo wa nchi kimaadili katika siasa, uchumi, na jamii na ndiyo maana linaitwa "Azimio la Utu." Azimio la Arusha lilikuwa linawaelekeza Watanzania jinsi ya kuishi maisha ya utu na ubinadamu.
Kisiasa:
Azimio la Arusha lilitangaza itikadi mpya ya taifa iliyokuwa inajulikana kama siasa ya 'Ujamaa na Kujitegemea'. Hili lilikuwa tangazo la nia ya kujenga taifa ambalo watu wake wanaishi pamoja na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote. Ilikuwa siasa iliyokuwa inapinga kabisa itikadi au imani za kibepari. Uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa Tanzania nzima ulikuwa na nia ya kulielekeza taifa katika maisha ya maadili ya kijamaa, ambayo ni maisha ya umoja, ushirikiano, usawa, ukarimu, na kujaliana kama ndugu wa familia moja badala ya maisha ya ubinafsi yaliyokuwa yanashabikiwa na ubepari. Kwa ujumla, Azimio la Arusha liliturudisha katika mfumo wa maadili wa jamii za Kitanzania kabla ya ukoloni. Kwa sasa baadhi ya misingi hiyo imeingizwa kwenye sheria mbalimbali ili kuendelea kuyalinda maadili, ikiwemo Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 inayokataza mambo yafuatayo: hongo, limbikizo la mali, kujipatia manufaa yasiyostahili, ubadhirifu na kuchepusha mali, na matumizi mabaya ya mamlaka.
Katika jitihada za kulielekeza taifa katika maadili ya ujamaa, Azimio la Arusha liliweka misingi ya kwanza ya maadili ya viongozi wa chama na serikali. Ilikuwa lazima kiongozi awe mkulima au mfanyakazi, asiwe na mawazo au imani za kibepari, asiwe mkurugenzi wa kampuni binafsi au kuwa na hisa katika makampuni. Isitoshe Azimio hilo halikutaka kiongozi wa chama au serikali awe na nyumba ya kupangisha au mshahara miwili. Lengo lilikuwa kuzuia viongozi na watumishi wa serikali na chama kujilimbikizia mali na kukuza mwanya wa wenye nacho na wasionacho.
Kiuchumi:
Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilipiga marufuku mfumo wa maisha ambao unawanyonya watu wengine. Matabaka ya mabwana na watwana yalifutwa na kusisitiza kila mtu afanye kazi kwa akili na bidii. Ili kuondoa unyonyaji, serikali ilipewa jukumu la kumiliki njia kuu zote za uchumi, zikiwemo ardhi, viwanda, mabenki, usafiri na usafirishaji na makampuni makubwa yaliyokuwa yamejimilikisha nchini. Kwa hiyo, serikali ilibinafsisha mali nyingi zilizokuwa zinamilikiwa na watu au taasisi binafsi na kuwekwa chini ya umma ili kuufaidisha umma wote wa Tanzania. Azimio lisisitiza pia maisha ya kujitegemea ambayo hayategemei misaada wala fedha kama chanzo cha maendeleo.
Kijamii:
Azimio la Arusha liliwasisitiza wananchi kubadilika kimawazo kwa kuacha mila na desturi za Wazungu na kukumbatia mila zetu za Kiafrika zilizo nzuri ambazo tuliziacha baada ya wakoloni kututawala. Huu ulikuwa mwito wa kujivunia Uafrika wetu, maadili yetu, na utamaduni wetu. Kwa kuliona hilo, mkazo mkubwa uliwekwa kwenye ukuzaji wa lugha yetu ya Kiswahili. Kiswahili kikawa ndiyo lugha ya taifa na kikaanza kufundishwa shuleni, na ikawa ndiyo lugha ya kufundishia elimu ya msingi. Ili kuendeleza utamaduni wetu, waasisi walianzisha wizara ya utamaduni ambayo kazi yake haikuwa tu kukuza ngoma za jadi bali kusimamia masuala yote ya utamaduni wa Watanzania. Ili kuhakikisha itikadi ya ujamaa inarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, serikali ilianzisha Sera ya Elimu ya Kujitegemea, ambayo kimsingi ilikuwa ililenga kumuandaa kijana wa Kitanzania kusoma kwa vitendo na siyo kwa nadharia. Vilevile, elimu hiyo ililenga kuwawezesha vijana kujitegemea baada ya elimu ya shule ya msingi. Aidha, ililenga kuwashirikisha wanafunzi wa ngazi zote nchini katika shughuli za uzalishaji mali katika taifa.
| Kazi ya kufanya 1.5 Soma matini kutoka katika vyanzo mbalimbali vya taarifa, ikiwamo mitandao, halafu eleza namna misingi ya Azimio la Arusha inavyoendana na juhudi za mapambano dhidi ya rushwa nchini |
Nafasi ya historia na maadili katika kujenga fahari ya taifa
Nafasi ya historia na maadili katika kujenga fahari ya taifa haiwezi kueleweka vizuri kama fahari ya taifa haileweki. Kwa hiyo, ni muhimu kujiuliza maswali yafuatayo: Maana ya fahari ya taifa ni nini? Tanzania inajivunia nini hasa au ni nini fahari ya taifa letu?
Kuna maana mbili za fahari ya taifa: Maana ya kwanza, ni hali ya kujivunia aliyonayo mtu au watu kwa ajili ya taifa lao. Hapa chanzo cha kujivuna ni mambo yote au baadhi ya mambo yaliyofanywa na yanayofanywa na taifa. Kwa mfano, siku ambayo timu ya mpira ya Tanzania itachukua kombe la dunia au la Afrika, Watanzania wengi wataona fahari kwa timu yao na taifa lao kushinda. Maana ya pili inahusisha ufahari au majivuno ya mtu au watu wanayopata kutokana na utambulisho wa taifa. Hapa chanzo cha ufahari na majivuno ni utambulisho wa taifa na si mambo yanayofanywa na serikali. Kwa mfano, Watanzania wengi wanajivunia mlima Kilimanjaro au mbuga za wanyama kama vile Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Mikumi, Ruaha na nyinginezo. Huu ni ufahari unaotokana na utambulisho wa taifa, ambao wakati mwingine unaweza kuwa umeundwa na serikali.
| Kazi ya kufanya 1.6 Kwa kutumia vyanzo tofauti vya taarifa, chunguza jinsi matukio muhimu katika historia ya Tanzania yanavyojenga fahari ya taifa. |
Taifa letu linajivunia mambo mengi lakini hapa tutajikita kwenye uchambuzi wa nafasi ya historia na fahari zifuatazo za taifa:
Amani na utulivu
Amani na utulivu ni miongoni mwa fahari kuu za taifa letu. Japokuwa Tanzania ina mjumuiko au mchanganyiko wa makabila zaidi ya 150 na watu wake wana dini na itikadi mbalimbali za kisiasa, wananchi wanaishi kwa amani na utulivu. Hali hii ya maisha ya amani ndiyo imeipa Tanzania sifa ya kuwa "Kisiwa cha Amani" tofauti na nchi nyingine ambazo zimekuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, mauaji ya kimbari, mafarakano ya tofauti za kidini, na fujo za uroho wa madaraka.
Hali hii ya utulivu na amani haijaja yenyewe bali imetengenezwa na maarifa ya historia. Tanzania ni nchi ya amani na tulivu kwa sababu waasisi wa taifa hili walijifunza katika historia kwamba vita ni mbaya na kwamba jamii zinazoundwa kwa ncha ya upanga pia husambaratishwa kwa ncha ya upanga. Japokuwa mababu zetu kama vile Mkwawa wa Wahehe, Machemba wa Wayao, Mangi Sina wa Wachaga, na wengine walipigana vita ili kulinda uhuru wao, walishindwa kupata uhuru kwa njia ya vita. Hivyo, waasisi wa taifa letu waliona ni vizuri kutafuta uhuru kwa njia ya amani na mazungumzo ambayo ilikuwa imejikita kwenye hoja za maadili. Hata baada ya uhuru, viongozi wetu wa serikali walichukua hatua mbalimbali za kuleta amani na utulivu kama vile kuleta umoja kwa kuamua kuua ukabila. Kwa hiyo, historia imechukua nafasi kubwa sana katika kujenga ufahari huu wa taifa letu.
Pamoja na hayo, amani na utulivu havikujengwa na historia tu bali pia na maadili. Amani na utulivu ni nadharia ambazo hazijijengi zenyewe. Ili kuweza kuishi kwa amani na utulivu ni lazima kuwapo na sheria, kanuni na misingi inayolinda amani. Msingi mkubwa wa amani ni haki. Pasipokuwa na haki hakuna amani. Aidha, mahali fulani hapawezi kuwa na haki kama kuna ukiukaji wa maadili, ikiwemo kujihusisha na vitendo vya rushwa. Katika hali hizo watu watapigana kutafuta haki zao na wengine watanyimwa haki zao kwa sababu ya rushwa ambapo matokeo yake ni kukosekana kwa amani na utulivu. Msingi mwingine wa amani ni utii wa sheria. Sheria zinazolinda amani ni muhimu kuheshimiwa. Kama katika nchi
fulani watu hawatii sheria na kutumia ofisi za umma kwa manufaa yao, basi katika nchi hiyo kutazuka fujo na mafarakano. Mifano hii inatosha kuonyesha kwamba historia pekee yake haiwezi kujenga amani bali, ili amani iwepo, historia inapaswa kushirikiana na maadili, yaani haki na utii wa sheria.
Umoja na mshikamano
Miongoni mwa mambo mengi ambayo Tanzania inajivunia ni hali ya umoja na mshikamano. Katika nchi ambayo ina makabila mengi, dini nyingi, tamaduni mbalimbali, na itikadi mbalimbali si rahisi watu wake kushikamana na kuwa wamoja. Lakini pamoja na tofauti zote hizo, Tanzania imeweza kuonesha umoja na mshikamano miongoni mwa watu wake. Wananchi wanashirikiana katika harakati za maendeleo na kusaidiana katika nyakati za shida na raha. Tabia hii inawapa watu wengi fahari ya kujivunia taifa lao. Umoja na mshikamano huu una misingi yake katika historia. Licha ya kufuata misingi na mshikamano waliokuwa nao mababu na mabibi zetu, waasisi wa taifa letu pia walisisitiza umoja. Azimio la Arusha, ambalo tumelielezea, lilikuwa tukio la kihistoria ambalo lilisisitiza umoja, yaani ujamaa. Uamuzi wa kuondoa matabaka ya mabwana na watwana, kutaifisha njia kuu za uchumi na kuziweka chini ya serikali, kuondoa unyonyaji, kuwaelekeza wananchi waishi na kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya wote, na uondoaji wa ubaguzi kwa misingi ya rangi ni baadhi ya jitihada za mwanzo za kihistoria ambazo zimechangia sana watu wa nchi hii kuishi kwa umoja na mshikamano. Ubaguzi kama vile wa rangi, ukabila, na dini ungeendekezwa na matabaka ya matajiri na maskini yakaachwa yashamiri na Kiswahili kikapuuzwa ingekuwa vigumu sana leo hii kwa taifa letu kuwa na umoja na mshikamano. Kwa hiyo, umoja upo nchini kwa sababu ya mchango mkubwa wa historia ya taifa letu.
Kwa nyongeza, lazima ikumbukwe kwamba umoja na mshikamano haujengwi na historia tu bali na maadili pia. Historia pekee yake itaujenga umoja lakini bila maadili umoja huo utadhoofika na kupotea. Ili kuwa na umoja na mshikamano ni lazima kuwe na sheria na taratibu zinazolinda umoja na mshikamano. Umoja, kama ilivyo kwa amani, unalindwa na misingi ya haki, ambapo haki za kila mwananchi zinaheshimiwa na kulindwa. Kama katika taifa haki za kila mmoja zinalindwa na kama kila mmoja anajiona ni sawa na mwingine, hapo umoja utakuwepo. Isitoshe, sheria zile zinazolinda umoja lazima ziheshimiwe na kila mmoja katika taifa. Pale tu mambo haya yanapofuatwa ndipo tunaweza kuwa na umoja. Aidha, tunaona pia kwamba historia pekee yake haiwezi kujenga umoja ikiwa umoja huo hausaidiwi na maadili ya kuheshimiana, kujaliana, kupendana, kushirikiana, na kutii sheria.
Lugha ya Kiswahili
Kama kuna kitu ambacho Watanzania wanajivunia sana basi ni lugha ya Kiswahili. Kuna sababu nyingi za ufahari huu: Kwanza, Kiswahili ni lugha ya Kibantu ingawa ina maneno mengi pia ya Kiarabu, Kiingereza, Kireno na lugha nyinginezo; pili, ni rahisi kujifunza; tatu, inatumika sehemu nyingi duniani ikiwa ni pamoja na Afrika ya Mashariki na Kati; nne, ni lugha inayokua kwa kasi katika Afrika, Ulaya, Asia na Amerika; tano, ni lugha ambayo inafundishwa katika mataifa ya nje kwa muda mrefu sasa; sita, ni miongoni mwa lugha za kimataifa zinazotambuliwa na UNESCO na ina siku yake maalumu ya kuiadhimisha kidunia (tarehe 7 Julai); na saba, ni lugha ambayo imewaunganisha Watanzania na kuwafanya wajione ni wamoja.
Kama zilivyo fahari nyingine za taifa, lugha hii ya Kiswahili nayo imepata ufahari wake kwa sababu ya historia. Ikumbukwe kwamba Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, "kilitokana na mwingiliano wa lugha za Kibantu za pwani na baadaye kikapata athari za Kiarabu na lugha nyingine za kigeni" kama ilivyo kwa lugha yoyote inayogusa. Lugha hizo ni pamoja na Kihindi, Kireno, Kiingereza na Kiarabu. Kilicholeta mwingiliano huo uliochangia kukua na kuenea kwa Kiswahili ni masuala ya biashara kati ya Waarabu na watu wa pwani, masuala ya ukoloni na utandawazi. Ili kukieneza, wapigania uhuru kama Mwalimu Nyerere walikitumia katika harakati zao za kisiasa, na hasa katika mikutano ya hadhara. Baada ya kupata uhuru, Kiswahili kilipandishwa hadhi na kuwa Lugha ya Taifa. Hapa tunaona kwamba historia ya mwingiliano na watu wengine, historia ya harakati za uhuru, na historia ya baada ya uhuru, vilichangia sana kuujenga ufahari huu wa taifa, yaani Kiswahili.
Hata hivyo, mkazo unaowekwa kwenye nafasi ya historia katika kujenga Kiswahili unapaswa pia kuwekwa kwenye nafasi ya maadili kwa sababu bila maadili Kiswahili kisingejengeka hata kufika kilipo sasa. Kiswahili kimejengeka hivi kwa sababu watu wanakipenda. Kupenda ni msingi muhimu sana katika ujenzi wa lugha. Kama watu wasingekipenda Kiswahili, ingekuwa vigumu sana kukijenga na kukiendeleza. Aidha, maadili yalichangia kukijenga Kiswahili pale watu walipokiheshimu. Japokuwa wakati wa ukoloni, na hata baada ya ukoloni, kulikuwa na kasumba ya kudharau lugha za Kiafrika na kuthamini lugha ya Kiingereza, lugha ya Kiswahili haikudhraulika kwa sababu kwa kiasi kikubwa ilikuwa tayari inaheshimika.
Pamoja na dharau walizokuwa nazo wakoloni juu ya utamaduni wa Mwafrika bado walikiheshimu Kiswahili kwani waliona kina umuhimu katika kutekeleza malengo yao. Kwa mfano, ili wakoloni wawasiliane na kuelewana na manamba, yaani vibarua, waliokuwa wanatoka sehemu mbalimbali za Tanzania kwenda kufanya kazi katika mashamba yao, ilibidi pande zote mbili zitumie Kiswahili. Hali kadhalika, Kiswahili kilitumika katika shughuli za utamaduni (mfano, ngoma na muziki), shughuli za dini, kusikiliza kesi za Waafrika, kilimo, majeshi, vyombo vya habari, mfumo wa elimu na hata katika harakati za uhuru. Mifano hii yote inaonesha jinsi maadili kama upendo, na heshima yalivyochangia kuijenga lugha ya Kiswahili, ambayo leo tunajivunia.
Urithi wa asili
Urithi wa asili ni rasilimali kama vile miti, misitu, madini, maporomoko au hifadhi za wanyama ambazo binadamu amezikuta. Kuwapo kwake hakukumtegemea binadamu bali zimekuwapo kwa sababu Mungu aliziumba. Urithi wa asili ni rasilimali ambazo hazijatengenezwa na binadamu. Urithi wa namna hii hapa Tanzania ni mwingi. Hata hivyo, Watanzania wengi wanajivunia zaidi mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama kama vile Ngorongoro, Tarangire, Mikumi, na Ruaha ambazo zina wanyama wengi na mandhari ya kuvutia.
Aidha, visiwa vya Zanzibar vina fukwe nzuri, kina kirefu cha bahari, bahari yenye aina mbalimbali za samaki na visiwa vingi vidogovidogo vinavyovutia. Tanzania ya leo inajivunia urithi huu ambao tumepewa na Mungu kwa sababu mababu na mabibi zetu waliotutangulia hawakuuharibu. Hakukuwa na vitendo vya ukiukaji wa maadili kama vile kutumia rushwa ili kuharibu urithi wa asili bali waliutunza hadi sisi tukajaliwa kuuona. Wangechoma misitu moto, wakaua wanyama wote kwenye hifadhi, wakalima kwenye vyanzo vya maji, au wakapulizia sumu kwenye maziwa na mito ya asili, kizazi chetu kisingeweza kuziona rasilimali hizi. Vilevile, kama hayo yangefanyika, kusingekuwepo kitu cha asili cha kuonea fahari. Hivyo, tunaona wazi kabisa kuwa maadili na historia ya utunzaji wa mazingira vimekuwa na mchango mkubwa sana katika kujenga fahari ya urithi wa asili.
Mchango wa historia katika ulinzi wa urithi wa asili unakamilika pale maadili yanapozingatiwa na kufanya mambo kadhaa ikiwemo kutoruhusu watu wachache watumie vishawishi mbalimbali kama rushwa kuharibu mazingira yaliyotunzwa na vizazi vilivyopita. Kama urithi wa asili ungelindwa na historia tu bila maadili, basi usingekuwepo. Bila maadili hakuna kitu kizuri ambacho kingeendelea kuwapo mpaka sasa. Urithi wa asili wa nchi yetu umeendelea kuwapo hadi sasa kwa sababu watu wanaupenda urithi huo na unawasaidia. Mathalani, mito, maziwa, mabonde, na milima hupendwa kwa sababu husaidia kujenga maisha bora kwa watu. Kwa mfano, mito na maziwa huwapa watu maji na samaki, mabonde yanawasaidia watu kwa shughuli za kilimo ambacho kinawapa chakula na uwezo wa kibiashara, na milima kama vile Kilimanjaro hupendwa kwa sababu ni kivutio cha utalii, ambacho kinaliingizia taifa fedha za kigeni.
Mbali na maadili ya upendo, ufahari wetu katika urithi wa asili unajengwa pia na maadili ya heshima kwa watu na viumbe wote. Mababu na mabibi zetu waliyaheshimu mazingira pamoja na viumbe vilivyopo juu na chini ya ardhi au majini. Heshima kwa urithi wa asili ndiyo iliwezesha mababu na mabibi zetu kuutunza urithi huo. Waliutunza kwa kutoharibu mazingira yao ya kuishi na kuutumia kwa njia endelevu. Mababu na mabibi zetu waliwaheshimu wanyama na hata mimea kwa namna sawa na viumbe hai wengine ambao wameumbwa na Mungu. Hivyo, urithi wa asili tulionao hadi sasa ulitunzwa na kuendelezwa kwa sababu katika mila na desturi za Kiafrika viumbe vyote vilichukuliwa kama vitu muhimu na vinavyotakiwa kutunzwa. Aidha, baadhi ya urithi wa asili tulio nao kama vile wanyama, misitu, miti, mito, maziwa, na milima vilichukuliwa kuwa ni vitu vyenye nguvu za kiroho na za kimungu. Tena vilionekana kuwa na uwezo wa kulinda na kutoa maisha ya binadamu; kwa hiyo, viliheshimiwa. Kwa mfano, kuna baadhi ya misitu ambayo ilikuwa haiguswi kwa sababu ilisadikiwa kuwa ni makazi ya miungu na sehemu takatifu za kufanyia matambiko. Pia, kuna wanyama ambao kimila ni ndugu wa familia, ukoo na hata kabila. Urithi wa asili kama wanyama, wadudu, majani, na hata miti wenye undugu na familia haukuguswa au kuvunwa. Katika hili pia tunaona kwamba maadili ya heshima, upendo na undugu yalichangia sana kujenga na kulinda urithi wetu wa asili.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Kitendo cha waasisi wa nchi yetu kuunganisha nchi mbili huru, yaani Tanganyika na Zanzibar, mwaka 1964 kililetea sifa kubwa sana nchi yetu. Pamoja na kwamba jitihada za kuunganisha Afrika ili iwe nchi moja zimekuwa zikisikitisha, Tanzania ni nchi pekee ya mfano iliyoweza kulichukulia wazo la muungano kwa umuhimu wake na kuungana. Mpaka leo, Tanzania ndiyo nchi pekee ya Afrika ambayo imeungana. Muungano unawafanya Watanzania wengi wajivunie na kuwastaajabisha wageni wa ndani na nje ya Afrika. Kitendo cha kuunganisha nchi mbili si mafanikio madogo. Watanzania wanapaswa kujivunia muungano huu ambao ni wa mfano. Pamoja na kuufurahia na kujivunia, ni muhimu kukumbuka daima kwamba hata huu muungano wenyewe umejengwa na historia. Kama wakoloni wasingeligawa bara la Afrika katika vipande vipande, na kama Waafrika wasomi wa mwanzo wasingeona umuhimu wa Waafrika kuungana na kuwahamasisha kufanya hivyo; na kama waasisi wetu, baada ya uhuru wasingeona umuhimu wa kuunganisha nchi hizi mbili ili kujenga umoja zaidi, basi ufahari tulionao leo kupitia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar usingekuwapo.
Ikumbukwe kwamba muungano haujengwi na historia tu bali kuwepo na kuzingatiwa kwa maadili. Bila kuwapo kwa maadili, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pengine ungekuwa umeshavunjika. Muungano huu upo mpaka leo kwa sababu ya upendo uliopo baina ya wananchi wa nchi hizi mbili. Isitoshe, muungano umedumu kwa sababu ya maadili ya heshima. Wananchi wa sehemu zote mbili wanaheshimiana bila kujali wanatoka upande gani wa nchi na wanashirikiana bila kubaguana. Pia, muungano umedumu kwa sababu ya utii wa sheria, kanuni na misingi inayolinda muungano. Kama kusingekuwa na utii wa sheria hizo, pengine muungano huo ungekuwa umeshavunjika.
Maelezo haya yanatosha kuonyesha kwamba si historia tu yenye mchango katika ujenzi wa fahari za nchi yetu bali maadili pia yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga na kulinda fahari hizi.
www.learninghubtz.co.tz
Zoezi
1. Eleza ni kwa namna gani utumwa ulikuwa kinyume cha maadili ya Kitanzania?
2. Chambua maadili ya viongozi wa chama na serikali kama yalivyoainishwa katika Azimio la Arusha.
3. Fafanua ni kwa namna gani alama za taifa zinatumika katika kudumisha maadili ya taifa.
4. Je, ni namna gani misingi ya Azimio la Arusha inaweza kutumika katika mazingira ya sasa?
5. Eleza namna vitendo vya rushwa vinavyoweza kuathiri mambo yafuatayo:
6. Eleza ni kwa namna gani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kielelezo cha maadili ya Tanzania.
7. Jadili ni kwa namna gani maadili ya Kitanzania yamechangia katika kutunza fahari yetu.
8. Je, ni kwa njia gani lugha ya Kiswahili imechangia katika kuimarisha utambulisho na maadili ya taifa?
Nafasi ya Tunu za Taifa na maadili katika kujenga misingi ya uongozi bora
Tunu za Taifa zina nafasi kubwa sana katika kujenga misingi ya uongozi bora. Dhana ya uongozi bora imejengeka juu ya misingi ifuatayo: uadilifu, uwajibikaji, uwazi, utii wa sheria, uzalendo na utu.
Uadilifu
Uadilifu ni uaminifu, na uaminifu ni tabia ya kuzingatia kanuni za maadili. Mtu mwenye uadilifu hana tabia ya kukiuka kanuni, sheria au maadili. Tunu za taifa zina nafasi kubwa katika kujenga misingi ya uadilifu; kwa mfano, uhuru ndio chimbuko la uadilifu. Uadilifu si tabia ya lazima au ya kushurutishwa. Hujengwa na familia, ukoo na hata kabila tangu utotoni mpaka katika utu uzima na huwa sehemu ya utu wa mtu. Kwa hiyo, uadilifu wa kweli unatoka kwenye utashi wa mtu aliye huru na anayejitambua. Uadilifu wa kulazimisha si endelevu kwani huwa haudumu kwa muda mrefu kwa sababu ni wa bandia; hivyo, hupotea baada ya muda mfupi. Isitoshe, uadilifu wa bandia au wa kinafiki hauwezi kufanikisha malengo ya mtu binafsi au ya jamii kwa sababu ni rahisi kwa jamii kuutambua. Uongozi bora unaleta tija pale ambapo kiongozi ana uadilifu unaotoka moyoni mwake, ambao umeshakuwa sehemu ya utu wake na si uadilifu wa kinafiki au wa kuigiza ili kupata masilahi binafsi.
Maadili pia yana nafasi yake katika kujenga uadilifu. Tabia ya ukweli, heshima kwa watu na viumbe, na upendo ni nguzo muhimu sana katika kujenga uadilifu. Kiongozi muongo, asiye na upendo na ambaye hana heshima kwa watu na mazingira yao hawezi kwa namna yoyote ile kuwa kiongozi mwenye uadilifu. Uongozi kama huo husambaratisha jamii; na mara nyingi kuwa chanzo cha mafarakano katika jamii. Kwa ufafanuzi huu, ni wazi kuwa tunu za taifa na maadili vina mchango katika kujenga misingi ya utawala bora.
Uwajibikaji
Hii ni tabia ya kiongozi kuwa tayari kujibu hoja na changamoto, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa anaowaongoza kuhusu uamuzi au matendo aliyoyafanya katika kuyatekeleza majukumu yake kama kiongozi. Usawa unasaidia sana kujenga misingi ya uongozi kwani kiongozi anayeamini katika usawa anawajibika kwa watu wake. Hii ina maana kwamba kiongozi hajioni kama yeye ni tofauti na anaowaongoza. Pia, hajioni kama yeye ni wa juu zaidi kuliko wengine, au yeye ni bora zaidi kuliko wengine na kwamba ana haki zaidi kuliko anaowaongoza. Hapa tunaona nafasi ya usawa katika uwajibikaji, ambao ni msingi muhimu wa utawala bora. Kama zilivyo tunu za taifa, ndivyo maadili yalivyo pia. Maadili yana nafasi kubwa na ya muhimu sana katika kujenga misingi ya uwajibikaji.
Kuwajibika ni kubeba dhamana ya watu na vitu. Lakini, ili uweze kubeba dhamana ya watu lazima uwapende, uwajali, na uwaheshimu bila kuwa na upendeleo au kutumia rushwa. Kiongozi hawezi kuwajibika kama hawapendi watu wake na kama atajihusisha na vitendo visivyokuwa vya kimaadili. Akiwapenda watu wake, atawajali, atawaheshimu, atawasikiliza na kuwashirikisha katika uamuzi unaogusa maisha yao. Bila tabia ya kuwapenda watu, kuwajali na kuwaheshimu hakuna uwajibikaji. Uwajibikaji utakuwepo pale tu kiongozi anapowapenda watu wake. Kwa hiyo, maadili kama upendo, na heshima si tu kwamba yanachangia kujenga misingi ya uwajibikaji bali pia ndiyo chanzo au nguzo kuu ya uwajibikaji. Maadili ya upendo kwa watu ndiyo yanamsukuma kiongozi kuwajibika kwao.
Uwazi
Uwazi ni hulka ya kuwashirikisha watu kutoa maoni na ushauri wao kuhusu namna ya kutenda jambo fulani au matumizi sahihi ya rasilimali kwa maendeleo yao binafsi na kwa na maendeleo ya nchi yao. Uwazi pia ni tabia ya kuwashirikisha wananchi katika uamuzi unaogusa maisha yao au masilahi ya nchi. Tunu za taifa kama umoja ina nafasi kubwa sana katika kujenga misingi ya uwazi, ambayo ni nguzo muhimu ya utawala bora. Umoja ni muhimu katika uwazi kwa sababu unapunguza majungu ya mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu. Uamuzi unaotolewa kwa pamoja na kwa kushirikiana unakuwa kwa ajili ya wote na si kwa ajili ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Jambo la muhimu ni kwamba, ushauri wa wengi una nafasi kubwa ya kuwa sahihi kuliko wa mmoja au wachache. Isitoshe, sauti ya umoja huwa inasikika zaidi kuliko sauti ya mtu mmoja mmoja. Kwa maneno mengine, sauti ya umoja iko wazi zaidi, inasikika zaidi na ina nguvu zaidi kuliko sauti ya mtu mmoja. Hapa tunaona kuwa umoja una nafasi kubwa katika kujenga misingi ya uwazi. Kama zilivyo tunu za taifa, maadili pia yana nafasi muhimu katika uwazi kwa sababu maadili ndiyo chanzo cha uwazi. Kinachomsukuma kiongozi kushirikisha watu katika uamuzi unaohusu maisha yao si rushwa au umaarufu bali upendo alionao kwa hao anaowaongoza. Kiongozi asiposukumwa na upendo hawezi kujali kuwashirikisha watu katika masuala yao. Pia, kiongozi asiyeheshimu watu wake hawezi kuwashirikisha katika uamuzi kwa sababu atakuwa anawadharau. Kwa hiyo, maadili kama upendo na heshima kwa watu ndiyo chimbuko na nguzo ya kujenga na kuimarisha uwazi, ambao ni nguzo muhimu katika utawala bora.
Utii wa sheria
Kiongozi bora ni yule anayeongoza kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo na si kwa akili zake mwenyewe. Kiongozi ana wajibu wa kujua sheria zinazomwongoza, kuziheshimu na kuzitii. Pia, ana wajibu wa kuwasaidia walio chini yake kuishi kwa kufuata sheria na kanuni za maisha katika nchi au jamii. Kwa ufupi, utii wa sheria ni msingi muhimu unaowezesha taifa kuishi kwa amani na salama.
Tunu za taifa kama vile undugu ndiyo chanzo cha utii wa sheria. Watu wanaoishi kama ndugu na kwa kujaliana wanasaidiana kutii sheria za nchi. Iwapo mmoja kati ya ndugu hao atakiuka sheria ataonywa ili asikiuke tena sheria zilizowekwa. Watu waishio kama ndugu hawaishi kwa kufuata sheria za msituni au zile zinazoruhusu mwenye nguvu aishi au atumie nguvu ya fedha aliyonayo kutoa rushwa bali wote huishi kwa kufuata sheria zinazotoa haki sawa kwa wote. Kiongozi anayetii sheria, hutoa huduma bila kujali jinsia, kabila, ukanda, dini na uwezo wa kifedha. Hii husaidia kuwa na jamii inayosimamia haki na usawa kwa maendeleo ya wote. Kwa hiyo, tunu kama undugu ndiyo chanzo cha utii wa sheria. Watu wasipojiona kama ni ndugu watatunga sheria mbovu za ubaguzi na unyanyasaji wa mtu mmoja na mwingine au wa kikundi kimoja dhidi ya kingine.
Maadili ya taifa pia yana mchango mkubwa sana katika kukuza watu waadilifu. Inawezekana kukawa na sheria zinazoongoza jamii, lakini kama hakuna maadili sheria haziwezi kufanya kazi. Sheria huwasaidia watu kuwa waadilifu. Kwa mfano, pasipo sheria wananchi watashindwa kuwajibika kulipa kodi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, haki zitapindishwa na urithi wa asili utaharibiwa au kupotea. Hivyo, bila kuzingatia maadili, sheria zitapindishwa kwa sababu ya rushwa, wenye haki watafungwa, na sheria zitawasaidia wenye fedha na wenye nguvu na si watu wote. Kwa ufupi, sheria zinafanya kazi pale palipo na maadili, na pasipo na rushwa hutawala. Kwa upande mwingine, maadili ndiyo chanzo cha sheria. Sheria zipo ili kuyalinda na kuyaendeleza maadili ya jamii. Kwa hiyo, sheria zinatokana na maadili. Hapa ndipo tunaona kwa mara nyingine nafasi ya maadili katika kujenga misingi ya utii wa sheria, ambao ni msingi muhimu wa utawala bora.
Uzalendo
Uzalendo ni sifa muhimu ambayo kiongozi yoyote anapaswa kuwa nayo. Hii ni hali ya kuipenda nchi yako na ikibidi kuwa tayari hata kufa kwa ajili yake. Kiongozi ambaye ni mzalendo anajituma kwa ajili ya manufaa ya taifa lake, anatunza rasilimali za taifa lake na si mla rushwa hata akishawishiwa na watu wengine. Aidha, wananchi wanapofahamu kiongozi wao ni mzalendo huwa wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa kuamini kuwa yanayofanywa na kiongozi wao ni kwa ajili ya manufaa ya umma. Uzalendo unawatia moyo wananchi kushirikiana katika kutatua changamoto za kitaifa na kujenga mustakabali mwema. Mtazamo wa kizalendo huhimiza uvumbuzi, ushiriki wa wananchi katika kutafuta maendeleo. Hii inasaidia kukuza ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na utawala bora. Uzalendo unaweza kuunganisha watu mbalimbali karibu na maadili na taasisi za kidemokrasia. Wakati utaifa unawaunganisha watu, uzalendo unajenga fahari, umoja na ujasiri kwa raia.
Utu
Utu ni sifa muhimu katika kuongoza watu, husaidia katika kujenga mazingira ambayo raia wanaheshimiwa na kulindwa haki zao. Utu ni ile hali ya mtu kuthamini, kuheshimu na kuwajali watu kama anavyojipenda yeye. Kimsingi mtu mwenye utu hafanyi mambo ambayo yeye hapendi kufanyiwa na watu wengine. Mtu mwenye utu husaidia na kuwa mlinzi wa haki za binadamu hivyo huhakikisha kwamba watu wote wanatendewa kwa usawa na bila ubaguzi na kwa kuzingatia haki za binadamu na uhuru pamoja na haki za msingi. Hii inajumuisha haki ya kushiriki katika masuala ya umma, haki ya afya, na haki ya kuishi katika mazingira yenye afya. Vilevile, mtu mwenye utu huwa mwepesi na mwajibikaji pamoja na kulinda haki za wanyonge kama walemavu, wazee, masikini, wanawake na watoto. Tunu ya utu husaidia katika utoaji wa huduma za umma zenye ufanisi na kwa usawa. Utawala unaozingatia utu unalenga katika kutoa huduma bora za umma zinazokidhi mahitaji ya wananchi wote, na kuimarisha ustawi na utu wao kwa ujumla pamoja na kupambana na rushwa.
| Kazi ya kufanya 1.7 Tunu za taifa la Tanzania ni pamoja na uhuru, umoja, amani, mshikamano, uzalendo, utu na undugu. Tafuta taarifa kuhusu tunu hizo kutoka katika vyanzo mbalimbali, kisha eleza mchango wake katika kujenga uongozi bora. |
Mikakati ya kulinda historia, utambulisho na maadili ya taifa
Historia, utambulisho na maadili ya taifa ni sehemu muhimu ya urithi wa taifa lolote. Ni muhimu kulinda urithi huo ili vizazi vya sasa na vijavyo viweze kuelewa na kuthamini asili na misingi ya taifa lao. Katika ulimwengu wa leo wenye mabadiliko ya haraka, ni muhimu kuweka mikakati madhubuti ya kulinda historia, utambulisho na maadili ya taifa. Tanzania ina mikakati mbalimbali yenye lengo la kulinda historia, utambulisho na maadili ya taifa kwa kutumia mihimili yake, ikiwemo bunge linalotunga sheria, mahakama inayotafsiri sheria zilizotungwa
pamoja na serikali inayotekeleza sheria kwa kutumia vyombo vyake vinavyosimamia urithi wa kihistoria na maadili vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria. Vyombo hivyo ni kama vile Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali National Audit Office of Tanzania - NAOT, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Ethics Secretariat - ES, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika African Liberation Heritage Centre - ALHC, Mamlaka ya Mapato Tanzania Tanzania Revenue Authority - TRA, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Drug Control and Enforcement Authority - DCEA na zinginezo.
Mikakati ya kuhifadhi historia
Baadhi ya mikakati ya kuhifadhi historia ya Tanzania ni hifadhi za nyaraka, uendelezaji wa makumbusho ya taifa, elimu ya historia, kuanzishwa kwa taasisi za utamaduni, na utafiti wa kihistoria.
Uhifadhi wa nyaraka za kihistoria
Uhifadhi wa nyaraka za kihistoria ni moja ya mikakati muhimu ya kulinda na kuitunza historia ya taifa. Tanzania imeanzisha makavazi ya taifa yenye jukumu la kuzihifadhi nyaraka za kihistoria kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo. Makavazi haya huhifadhi nyaraka mbalimbali kama vile picha za zamani, barua za kihistoria, makabrasha ya taarifa za kihistoria, rekodi za serikali, vitabu vya kumbukumbu, na filmu za kihistoria. Nyaraka nyingine ni pamoja na vitu vya kale, sanaa za jadi, mikataba na nakala za magazeti na majarida ya zamani, urithi na ukombozi wa bara la Afrika. Uhifadhi wa nyaraka hizi hutusaidia kuelewa matukio muhimu ya zamani na maendeleo ya taifa letu. Pia, nyaraka hizi hutumika katika tafiti, elimu, na maendeleo ya taifa. Kwa kufanya hivyo, historia yetu inabaki salama na itaendelea kuwapo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, Tanzania baada ya kupewa dhamana ya kulinda na kuhifadhi urithi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika mwaka 2011, ilianzisha Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambacho kinahifadhi nyaraka mbalimbali zikiwemo vitabu, picha, vifaa, hotuba za viongozi, ramani, magazeti na majarida ya harakati za ukombozi wa Tanzania na maeneo mengine ya Afrika. Pamoja na kuthamini mchango mkubwa wa hali na mali uliofanywa na Tanzania wakati wa harakati za ukombozi, kituo hiki kinasimamia maeneo zaidi ya 200 ambayo yalitumiwa wa wapigania uhuru kutoka nchi mbalimbali, ambayo sasa yanatumika kama vituo vya utalii wa historia ya ukombozi.
Uendelezaji wa makumbusho ya taifa
Uendelezaji wa makumbusho ya taifa ni muhimu katika kulinda na kuhifadhi historia ya taifa letu. Makumbusho hutoa fursa ya kipekee kwa jamii kujifunza asili ya kihistoria na vitu vya kipekee kama vile mabaki ya akiolojia na nyaraka adimu. Uendelezaji wa makumbusho ya taifa ni moja ya mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kuhifadhi historia, utambulisho na maadili ya taifa. Tanzania ina makumbusho mbalimbali kama vile Kijiji cha Makumbusho, Makumbusho ya Taifa, Nyumba ya Sanaa iliyopo Dar es Salaam na Jumba la Makumbusho Zanzibar. Pia, kuna Makumbusho ya Azimio la Arusha, Makumbusho ya Vita ya Maji Maji, Songea na Makumbusho ya Daktari Livingstone yaliyopo Ujiji, Kigoma. Uendelezaji wa makumbusho ni muhimu katika kuielimisha jamii na kusambaza uelewa wa historia yetu kwa vizazi vijavyo.
Elimu ya historia
Elimu ya historia ni muhimu katika kulinda, kuhifadhi, na kuendeleza historia ya taifa letu. Husaidia kuyaelewa matukio muhimu, viongozi wa zamani, utamaduni, na mila zetu. Historia ni msingi wa utambulisho wetu wa kitaifa na inatuwezesha kujenga uzalendo. Kupitia elimu tunajifunza asili yetu na jinsi tulivyofika hapa tulipo leo. Elimu ya historia inawawezesha wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali kutambua mchango wa historia na kuwafanya kuwa mabalozi wazuri wa taifa letu. Elimu ya historia inajenga umoja, mshikamano, na kuwawezesha vijana kuwa raia wema na wazalendo. Pia, serikali imeanzisha somo la Historia ya Tanzania na Maadili kama somo la lazima. Somo hili linafundishwa katika ngazi za elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Lengo ni kuongeza uelewa kwa wanafunzi, wadau na wananchi kuhusu historia, utambulisho na maadili ya taifa la Tanzania. Pia, somo hili linawawezesha Watanzania kutamini mchango wa mababu na mabibi zetu katika maendeleo ya nchi yetu ili kujenga uzalendo kwa nchi yetu.
Kuanzishwa kwa vyombo na taasisi za kiutamaduni
Vyombo na taasisi mbalimbali zimeanzishwa ili kulinda historia, utambulisho na maadili ya taifa. Baadhi ya vyombo hivyo ni:
(a) Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA): BASATA ni chombo kinachosimamia na kuikuza sekta ya sanaa nchini Tanzania. Chombo hiki kinafanya kazi ya usimamizi wa shughuli za sanaa, kuendeleza vipaji vya wasanii, na kusaidia maendeleo ya sekta ya sanaa kwa ujumla.
(b) Bodi ya Filamu Tanzania: Hii ni bodi inayosimamia tasnia ya filamu nchini Tanzania. Ina jukumu la kudhibiti na kusimamia uzalishaji wa filamu, kutoa leseni kwa waandaaji wa filamu, na kusimamia ubora wa kazi za filamu. Bodi hii huhakikisha kwamba filamu zote zinazozalishwa ndani ya nchi au zile zinazotoka nje ya nchi hazikinzani na maadili, mila na desturi za Kitanzania.
(c) Idara ya Maendelo ya Utamaduni: Idara hii ni sehemu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Inajihusisha na mipango na sera za kuukuza na kuulinda utamaduni wa Mtanzania. Hufanya kazi katika maeneo kama vile kudumisha urithi wa kitamaduni, kukuza tamaduni za makabila mbalimbali, na kusaidia matamasha na matukio ya kitamaduni.
(d) Makumbusho ya Taifa: Chombo hiki, pamoja na kuwa na aina mbalimbali za makumbusho katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini, kina jukumu la kuukusanya, kuuhifadhi, na kuukuza urithi wa kitamaduni wa Tanzania. Hutoa elimu kuhusu utamaduni wa Tanzania kupitia maonyesho ya kisanii, makumbusho, na shughuli nyingine za elimu.
(e) Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika: Kituo hiki kipo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Jukumu lake ni kuutunza, kuulinda na kuuhifadhi urithi wa ukombozi wa bara la Afrika. Kituo hiki kimeanzishwa baada ya Tanzania kupewa dhamana ya kuulinda na kuuhifadhi urithi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) tangu mwaka 2011 kupitia Azimio la kuanzishwa programu mahususi ya kuhifadhi kumbukumbu za ukombozi wa Afrika. Kielelezo 1.1 kinaonesha jengo la Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.
|
Kielelezo 1.1: Jengo la Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika |
Utafiti wa kihistoria na uchapishaji
Utafiti wa kihistoria na uchapishaji ni muhimu katika kulinda na kuendeleza historia ya taifa letu. Utafiti husaidia kuchunguza matukio muhimu ya watu mashuhuri, jamii, taasisi au nchi na kusambaza maarifa haya kwa jamii. Utafiti ni njia ya kuimarisha urithi wetu wa kihistoria na kuelimisha vizazi vijavyo. Kwa kufanya hivyo, tunajenga msingi imara kwa mustakabali wetu. Utafiti wa kihistoria na uchapishaji huhakikisha kuwa historia yetu inaendelea kudumishwa na kupatikana kwa wote. Njia hii pia husaidia kujivunia tamaduni zetu za zamani. Kupitia tafiti za kihistoria, tunaimarisha ufahamu wetu juu ya asili na tamaduni zetu na kuongeza maarifa kuhusu tulikotoka, tulipo na tunakoelekea katika maendeleo kama taifa.
| Kazi ya kufanya 1.8 Tafuta taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwamo mitandao, kisha bainisha mikakati mingine ya kuhifadhi historia ya Tanzania. |
Mikakati ya kulinda maadili
Maadili ni muhimu sana katika maendeleo ya taifa. Bila jamii kuwa na maadili ni vigumu kupata maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Ili kufanikiwa katika hilo, serikali, taasisi zisizo za serikali na jamii kwa ujumla zimeandaa mikakati mbalimbali kuhakikisha maadili ya jamii yanalindwa. Baadhi ya mikakati ya kulinda maadili ni pamoja na elimu kwa umma, uanzishwaji wa taasisi kama TAKUKURU, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Utoaji wa elimu kwa umma
Maadili ni eneo mtambuka linalosimamiwa na wadau mbalimbali. Serikali imekuwa inatumia majukwaa mbalimbali ili kuufikisha ujumbe wa maadili kwa jamii. Mathalani, inatoa elimu ya mlipa kodi inayotolewa na kusimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na Mahakama ya Tanzania inatumika kutoa elimu kuhusu mambo ya sheria pamoja na elimu inayotolewa na taasisi mbalimbali zinazosimamia maadili na urithi wa historia. Aidha, baadhi ya taasisi za umma zinazosimamia maadili zimekuwa zikishirikiana kwenye matukio mbalimbali kama vile kwenye Siku ya Maadili na Haki za Binadamu inayoadhimishwa kitaifa tarehe 10 Desemba kwa kila mwaka. Siku ya Maadili imetokana na uamuzi wa serikali ya kuunganisha Siku ya Kimataifa ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inayoadhimishwa tarehe 9 Desemba na Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inayoadhimishwa tarehe 10 Desemba ili kupisha tarehe 9 Desemba ambayo ni siku ya Uhuru wa Tanganyika. Taasisi zinazoshirikiana kuadhimisha Siku ya Maadili ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka ya Manunuzi ya Umma, Tume ya Utumishi wa Umma, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mahakama, Polisi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nyinginezo.
Taasisi hizi zinashirikiana katika matukio anuai kwa lengo la kuelimisha na kushirikisha umma katika kujenga na kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa. Mbinu za uelimishaji ni pamoja na kushiriki katika vipindi vya redio na televisheni, kuchapisha habari na makala magazetini, kuwa na wiki maalumu ya kutoa huduma kwa wananchi na kuchapa na kusambaza machapisho mbalimbali. Kwa upande mwingine, kutokana na umuhimu wa kujenga maadili kwa vijana, somo la Historia ya Tanzania na Maadili limeingizwa kwenye mitaala ya elimu kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Vilevile, elimu inatolewa kupitia vyombo vya habari kama vile redio, runinga, magazeti, mitandao ya kijamii na taasisi za kiraia. Aidha, kumekuwa na vipindi maalumu vinavyofundisha umuhimu wa umoja, heshima, usawa na mshikamano katika jamii ambapo mambo yasiyo ya kimaadili yamekuwa yakibainishwa na kukemewa. Jamii imekuwa ikielemishwa umuhimu wa maadili na madhara ya kudharau maadili ya taifa.
Kuanzishwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Kuanzishwa kwa TAKUKURU ni mwendelezo wa juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya rushwa. Msingi wa mwelekeo huo umejengwa katika falsafa ya aliyekuwa Rais wa awamu ya kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa analihutubia Bunge jipya Mwaka 1965 na kusema: RUSHWA ishugulikilwe bila huruma kwa sababu mimi naamini kuwa RUSHWA na HONGO ni adui mkubwa zaidi kwa ustawi wa wananchi wakati wa amani kuliko wakati wa vita. Mimi ninaamini kuwa rushwa katika nchi inatakiwa ishugulikilwe karibu sawa sawa na unavyoshugulikilwa UHAINI. Wakati maadili ni mwendendo mwema, rushwa ni zao la uozo wa kimaadili unaomsukuma mtu kufanya jambo lenye sura ya uhalifu. Serikali imeweka mikakati ya kuanzisha taasisi mbalimbali zinazosimamia maadili ikiwemo TAKUKURU inayosimamia mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Aidha, mwelekeo wa serikali kwenye vita dhidi ya rushwa umejengwa katika masharti ya Ibara ya 8 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayosema: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo, lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi. Ibara ya 9 (h) ya Katiba ya Tanzania inaelekeza kwamba: Taasisi na Vyombo vyote nchini kuhakikisha tunaondoa rushwa katika jamii yetu. Kwa kuitikia agizo la katiba, serikali ilitunga Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, ambayo ndiyo ilianzisha TAKUKURU mwaka 2007 baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa Na. 16 ya Mwaka 1971 na baada ya kufanyiwa marekebisho Sheria ya Kuzuia Rushwa (Cap.400) ya mwaka 1970 iliyokuwa imerithi sheria ya kikoloni, yaani Sheria ya Kuzuia Rushwa (*The Prevention of Corruption Ordinance Cap.400*) ya Mwaka 1958. Kifungu cha 5 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 kinaipa TAKUKURU jukumu la kuongoza na kuratibu mapambano dhidi ya rushwa na Kifungu cha 4 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 7, kimeainisha majukumu mawili ya TAKUKURU ambayo ni kuzuia rushwa na kupambana na rushwa. Majukumu hayo mawili yanatekelezwa na TAKUKURU kwa kufanya kazi zifuatazo:
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya serikali iliyoanzishwa kama taasisi ya kitaifa iliyo na jukumu la kukuza na kuzilinda haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania. Tume hii hufuatilia utendaji kazi wa taasisi mbalimbali kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jukumu la tume hii ni kukuza ulinzi na haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na makubaliano ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeridhia. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pia hupokea malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hufanya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa kanuni za utawala bora. Vilevile, tume hufanya utafiti na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na mambo yanayohusiana na utawala bora. Pia, tume huanzisha kesi kwa viongozi wanaokiuka miongozo ya kimaadili. Mwisho, tume hii huzirekebisha sheria zinazokiuka haki za binadamu katika jamii.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Hii ni idara ya maadili ya viongozi wa umma ambayo ina mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa viongozi na watumishi wa umma kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa masharti ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma yanazingatiwa ipasavyo. Idara hii imeundwa mahususi kama mkakati wa kudumisha maadili ya viongozi wa umma kulingana na nafasi zao. Kiongozi wa umma anatakiwa kuwa mwadilifu, mhapakahazi, mwenye ujuzi, muungwana na mvumilivu. Kama kiongozi anashindwa kufuata miongozo hii, atakuwa amekiuka sheria ya maadili ya umma; na hivyo, yuko hatarini kuchukuliwa hatua au kuwajibishwa.
| Kazi ya kufanya 1.9 Fanya utafiti katika jamii unamoishi, kisha ainisha mikakati mingine ya kuyalinda maadili ya Kitanzania. |
www.learninghubtz.co.tz
Zoezi la marudio
1. Kwa kutumia mifano katika mazingira unamoishi, eleza umuhimu wa tunu za taifa kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.
2. Eleza madhara ya rushwa katika utoaji haki, uwajibikaji, uwazi na utii wa sheria.
3. “Taifa lisilokuwa na sheria ni sawa na wanyama mwituni.” Jadili sentensi hii kwa kutumia mifano dhahiri...
4. Ni kwa namna gani utamaduni wa kujitolea unathiri utambulisho wa taifa?
5. Ni namna gani misingi ya historia ya utambulisho na maadili ya taifa la Tanzania imechangia katika kuleta heshima na sifa nzuri kwa nchi yetu?
6. Eleza chimbuko la utambulisho wa taifa la Tanzania.
7. Jadili ni kwa namna gani Serikali ya Tanzania imefanikiwa kujenga umoja na mshikamano nchini.
8. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, "Azimio la Arusha lilikuwa azimio la utu." Jadili sentensi hii kwa mifano dhahiri.
9. Ni kwa namna gani elimu inaweza kutumika kama njia ya kulinda historia, maadili na utambulisho wa taifa?
10. Jadili mchango wa TAKUKURU katika ujenzi wa maadili ya taifa la Tanzania.
11. Ni changamoto gani Tanzania inakabiliwa nazo katika uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka za kihistoria?
12. Ainisha faida za kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu kwa taifa la Tanzania.
13. Eleza namna maliasili za taifa zinavyoweza kutumika kama sehemu ya utambulisho wa taifa.